Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba hizi nzuri tulizonazo mbele yetu. Nianze kwa kuwapongeza Mawaziri, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, Mheshimiwa Profesa Kitila na Naibu Mawaziri, kwa hotuba nzuri waliyotuletea; hotuba ya wananchi ambayo inaenda kumalizia pale palipobaki lakini na kuanza miradi ambayo inaenda kuchechemua uchumi wa wananchi wetu katika majimbo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza watendaji wote wa Wizara hizi na makatibu wakuu kwa jinsi ambavyo wanaendelea kuwapa ushirikiano ili tuweze kufanikiwa katika nchi yetu kuweza kupata maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo anaendelea kuwaletea wananchi maendeleo lakini kwa jinsi ambavyo anaendelea kuwa na maamuzi thabiti lakini kuwa na Serikali iliyo imara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Neno la Mungu katika kitabu Mithali 14 linasema; “Pasipo mashauri Taifa huanguka.” Ili Taifa liweze kusonga mbele lazima Serikali iwe na maamuzi na siyo sifa kuwa kwenye kiti umeaminiwa ukaogopa kufanya maamuzi kwa sababu utafanya makosa, siyo sifa. Sifa ni fanya maamuzi sahihi kwa ajili ya wananchi ili Serikali iweze kusonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1975 nchi yetu ilipata uhaba wa mahindi. Mwalimu Julius Nyerere aliambiwa soko la mahindi liko kwa makaburu lakini kwa sababu wananchi wake walikuwa na... nam-quote Mheshimiwa Rais Nyerere alisema kwamba; “Niko tayari kwenda kununua mahindi kwa mashetani ili wananchi wangu wasife.” Alificha hisia zake na alificha chuki yake ili wananchi wake wasife.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni miezi miwili, mitatu tulikuwa hapa na sote tulikuwa tunapiga kelele kwa ajili ya wananchi wetu hawana sukari. Kule kwangu Muhambwe sukari ilifika shilingi 7,000. Serikali kwa kuona kwamba hawawezi kukaa kimya wananchi wao wakafa na kupiga kelele walifanya maamuzi. Nampongeza Mheshimiwa Bashe, Waziri wa Kilimo na nampongeza Mheshimiwa Dkt. Mwigulu kwa kuja na mpango na sheria ambayo itatusaidia kutoka kwenye hali hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sukari hii kwa wnanchi wetu ndiyo kila kitu. Asubuhi akipata chai yake na mihogo atakutana na mlo mwingine jioni baada ya kutoka shamba lakini muuza maandazi bila hii sukari hawezi kuuza maandazi ili aweze kupata uchumi. Kwa hiyo, tukifanya masihara kwenye hii sukari kwa kweli hatuwatendei wananchi wetu waliotuleta humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimo humu ndani kwa sababu ya Wanamuhambwe walioniamini pamoja na changamoto kubwa ya mfumo dume lakini waliniamini wakasema nije niwatetee wananchi wangu wa Muhambwe. Leo nitawatetea wananchi wangu wa Muhambwe ili wapate bei nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninavyokwambia sukari bado ni shilingi 3,500 mpaka 3,800. Kwa hiyo, kama tutakalia kimya suala hili ina maana wananchi wetu wataendelea kuumia. Nawapongeza Serikali kwa kuja na maamuzi sahihi kwa sababu maamuzi haya yatakwenda kuwakomboa wananchi wetu. Hatuna haja ya tuition. Kila mtu anafahamu supply and demand ndiyo ina control kila kitu...
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mathayo, Taarifa.
TAARIFA
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naungana kumpongeza mjumbe anayezungumza kwamba Serikali lazima iwe na maamuzi kwa maana kwamba haina sababu ya kuwaacha wananchi wake wanaumia. Kama hivyo ndivyo, sasa ni vizuri zaidi maadamu Waziri mwenyewe anasema kwamba wale wafanyabiashara wanaficha sukari na wanasababisha uhaba uwepo na kutokana na hali hiyo ni kwamba suala hilo limemshinda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini suala hilo sasa lije Bungeni, ili tujadili na tuone namna ya kulishughulikia. Kuliko pale tunapofika maamuzi ya kusema njia pekee ya kushughulika na hao ni kuruhusu sukari ambayo haina ushuru iingie nchini wakati huo tunaendelea kupoteza mapato na tunaendelea kupoteza ajira, nakushukuru. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Samizi unapokea Taarifa?
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa yake siipokei kwa sababu sasa hivi Serikali imeshakuja hapa na Muswada wa Finance tupitishe tusonge mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyo viwanda vingi hapa nchini vinavyoleta bidhaa na viwanda hivi pamoja na kuwa vinatengeneza bidhaa hapa nchini bado tunaingiza vitu. Simenti na mabati yanaingia hapa nchini. Tuna viwanda vya vitenge na vitenge bado vinaingia hapa nchini. Sisi watu watu Kigoma tunavaa vitenge vya Congo na siku zote vitenge vinaingia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko njia pekee ya kuvilinda hivi viwanda. Hatuna sababu ya kutengeneza njia ya kulinda viwanda vya sukari tofauti. Kwanza ni double standard; kama ambavyo viwanda vingine vya nchi hii vinalindwa kwa bidhaa zinzoingizwa kuwekewa ushuru wa forodha (import duty) na viwanda vya sukari navyo vilindwe hivyohivyo ili kuwe na uhuru tusiwe na monopoly ya watu wachache ambao watakuwa wanatuamulia bei kwa ajili ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali na naunga mkono hiyo finance bill ije mbele yetu tuweze kupitisha kwa ajili ya manufaa ya wananchi wetu lakini kwa sababu ya manufaa ya wananchi wa Muhambwe. Nimalizie kwa kusema...
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kandege, Taarifa.
TAARIFA
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ambayo naomba kumpa mjumbe ambaye anaongea vizuri sana, si vibaya kama tutaenda kujifunza kwa majirani zetu ambao wamefanya vizuri. Nchi ya Uganda walikuwa na shortage ya sukari. Walichofanya ni kuhakikisha kwamba wanajitosheleza kwa kuzalisha sukari ndani ya nchi yao na sasa hivi wa export. Kwa hiyo, kuna la kujifunza kwa jirani. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Samizi unapokea Taarifa ya Mheshimiwa Kandege?
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea Taarifa yake na naomba niendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikoa yote iliyopo pembezoni mipakani ndiyo mikoa inayofaidika na sukari ya bei rahisi kwa ajili ya sukari za magendo kutoka kwenye hizo nchi? Kwa nini isiwe Tanzania ambapo tuna viwanda?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kuwaambia Mawaziri hawa, Joshua aliambiwa uwe hodari na moyo mkuu na muwe mashujaa. Muwe mashujaa kwa sababu leo hii tunapata nguvu ya kujadili process kwa sababu wananchi wetu wametulia na wana sukari. Ingekuwa leo wananchi hawana sukari kelele zile za mwezi wa pili na wa tatu hapa ndani tusingeweza kujadili. Ingekuwa ni taarifa zinaendelea humu ndani kwa sababu wote tunafahamu kelele za wananchi zilivyokuwa kubwa na wananchi ndiyo wametuamini, wametuleta hapa ndani. Tuna raha leo tunajadili kwa sababu wananchi wana sukari, muwe na moyo mkuu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, muwe mahodari Mheshimiwa Bashe, muwe mashujaa, tupo pamoja na ninyi katika kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata sukari ya bei nafuu. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, muda wako umeisha, hitimisha tu Mheshimiwa.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba nihitimishe kwa kusema kwamba naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kazi nzuri na kwa jinsi ambavyo wanaendelea kutuletea maendeleo na sisi wananchi wa Muhambwe tuko pamoja kuunga mkono Serikali hii ili kazi iendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)