Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalenga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na mimi kupata nafasi ya kuchangia leo katika hoja hizi mbili zilizoko mezani. Nianze kwa kumshukuru sana Rais kwa kazi kubwa inayofanywa katika nchi hii katika kuimarisha miundombinu mbalimbali ikiwemo ya afya, barabara, maji na maeneo mengine yote katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwashukuru Mawaziri wawili ambao leo wana hoja zao mbele yetu; Waziri wa Fedha pamoja na Waziri wa Mipango, wameleta mipango mizuri ambayo tunaamini ikienda kutekelezwa kwa usahihi, nchi hii itapiga hatua kimaendeleo na itakuwa mahali pazuri sana pa kuishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuanze kuzungumzia suala la kodi; tunazungumzia Bajeti Kuu ya Serikali na tunazungumzia upungufu wa makusanyo ya kodi katika maeneo mbalimbali. Ningependa nianze kwa kushauri katika vyanzo vingine ambavyo Serikali hii inaweza kuviangalia, kwa mfano, kuna biashara kubwa sana ambazo zinafanyika kwenye mitandao na biashara hizi ambazo zinafanyika kwenye mitandao hazijaweza kuangaliwa vizuri. Kwa hiyo, tuwe na teknolojia au maarifa ambayo yatatuwezesha kutambua biashara mbalimbali zinazofanyika kwenye mitandao na namna gani tunaweza kupata kodi kutoka kwenye hizo biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo mengine ambayo pia tunapoteza kodi, kwa mfano, iko miradi mikubwa unakuta inafanyika na hawa mafundi wadogo wadogo. Anaweza akachukua mradi wa shilingi milioni 100, shilingi milioni 200, shilingi milioni 300 ukafanywa na mafundi tunawaita local fundi, lakini Serikali haipati kodi, unaweza ukaona fundi anachukua karibu 30% katika mradi ule, lakini haziingii kwenye Serikali, sasa tufanyeje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuwe na kusajili hii miradi, mradi ukiwa pengine unaanzia shilingi milioni 30, Serikali iweke mpango wa kusajili hii miradi ili iwe na sababu ya kulipa kodi na Serikali iweze kupata mapato yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka nichangie kwenye mipango ni kwenye upande wa elimu, tunafahamu kwamba elimu ni msingi na ndiyo uti wa mgongo. Nilikuwa najaribu kuangalia, tunaweza tukaweka mipango ya muda mrefu; kwa mfano, tunajua katika nchi hii tuna reserve pengine za madini ambazo tunaweza tukavuna kwa miaka 50 ijayo, reserve za gesi, mafuta na vitu vingine. Ni muhimu sana sasa tunavyoangalia vipaumbele vyetu vya elimu kwamba tupeleke watoto katika maeneo haya, twende tukawasomeshe katika maeneo haya ili sasa wakirudi watatusaidia kama nchi kufanya exploration, lakini tukawa na wataalamu wetu wa ndani ambao wanaweza kusaidia kuinua uchumi katika maeneo haya ambayo ni nyeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunavyoweka mipango ya muda mrefu, tuangalie kusomesha watoto katika haya maeneo kwamba katika miaka 50 ijayo tutasomesha watoto wangapi ambao baadaye watakuja kulisaidia Taifa, ni mataifa mengi yamefanya hivyo, China wamefanya hivyo, walipeleka watoto kusoma Marekani. Japan wamefanya hivyo na sasa wamerudi kujenga nchi zao, utaona trend ndivyo ilivyo, kwa hiyo, hilo tuliangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu sasa hivi imeanza kukua sana katika eneo la utalii, je, ni aina gani ya elimu ambayo tunatoa hasa katika eneo la kuhudumia wageni wetu. Sehemu hii tuko chini sana, ukiangalia katika nchi za Afrika Mashariki kwenye eneo la huduma kwenye hoteli, sisi tuko chini sana. Tatizo ni kwamba aina ya vyuo ambavyo vinatoa elimu hizi, walimu wake tunawatoa wapi? Hilo ni eneo ambalo pia lazima tuliangalie, kama tunataka kuboresha utalii ni lazima pia tuboreshe huduma kwa wale watalii wanaokuja katika nchii hii, kwa sababu mtu akija mara moja hajapata huduma nzuri ataipenda nchi, lakini ile kero tu ya huduma kesho harudi na ndiyo maana Tanzania inakuwa na wageni wengi ambao hawarudi kwa sababu ya huduma ambazo tunazitoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni upande wa viwanda, tumesema kwamba tunataka kujenga uchumi shindani wa viwanda kwa maendeleo ya watu. Ni mikakati gani ambao tumefanya kutoa incentives kwa watu wanaojenga viwanda hasa ukiangalia kwenye maeneo ya kilimo, eneo hilo tunasema, lakini hakuna uwekezaji mkubwa na punguzo la kodi ambalo tumetoa kwa watu wanaowekeza hata kwenye viwanda vidogo vidogo. Tulikuwa na mipango ya kujenga viwanda, kwa mfano kule Mafinga kuna eneo lilitengwa Nyororo kwa ajili ya kujenga viwanda vya parachichi na packaging, tumeishia wapi katika hiyo mikakati?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, unakuta kwamba tunakuwa na mipango mingi mizuri, lakini sasa utekelezaji wake, kama tunaweza kuweka vivutio vya kodi kwenye eneo la viwanda vidogo vidogo hasa katika eneo la kilimo tutaweza kuwa na viwanda na kuweza kuvutia ajira. Sasa suala la kununua bidhaa za ndani ni lazima liwekewe msisitizo maalumu. Tunavyo viwanda katika nchi hii, kwa mfano, katika mabomba ya maji, lakini tumezungumzia hapa katika viwanda vya sukari pia. Mwenzangu amezungumzia ni namna gani Uganda wameweza kujitegemea kwenye sukari, ni lazima wakati mwingine tupitie maumivu, tunavyotaka kutengeneza huu mchakato wa kuwa na viwanda vyetu tujitegemee, ni lazima tukubali kupitia maumivu wakati fulani ili sasa tufike kule tunakokwenda. Tukiwa na maamuzi rahisi kila wakati hatuwezi kufika, mambo mengine lazima tukubali kupitia katika mchakato mgumu ili tufike tunakokwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kwenye matumizi ya fedha za Serikali, ni muhimu sana tukawa na nidhamu ya matumizi ya fedha za Serikali. Kama tunaweza kuweka fedha nyingi kwenye OC, kwa mfano sasa hivi unakuta kwamba mtu anaweza akafanya kongamano la shilingi milioni 300, for what? Kwa sababu gani katika nchi hii maskini? Mnaelewa? Kwamba ni vizuri kufanya makongamano na semina, lakini ni kwa kiasi gani tunatumia fedha kwenye haya makongamano na ni tija ipi ambayo tunaipata kwenye Taifa kama hili maskini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nidhamu katika matumizi ya fedha za Serikali ni muhimu sana ili Taifa liweze kuendelea, vinginevyo, tutakuwa tunapiga mark time. Hapa alizungumza asubuhi dada yangu Mheshimiwa Rose Tweve, namna tunavyotumia fedha nyingi kwenye makongamano na warsha kwenye kuelimisha malaria wakati tuna kiwanda kikubwa na kizuri pale Kibaha ambacho kinaweza kutokomeza malaria, hatuna habari, tunazungumzia habari ya kuleta chanjo za malaria wakati tuna kiwanda hapa nchini. Wakati fulani sisi kama viongozi ndiyo tunaweza kutoa dira namna gani Taifa letu linavyokwenda na linaweza kustawi kwa michango yetu na maamuzi tunayofanya, ni muhimu sana hilo tukaweza kuliangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala hili la kuwa na indicators katika kutenda kazi, key performance areas ni muhimu sana. Huu mtindo wa kusema kwamba mfanyakazi akikaa kazini miaka miwili, mitatu, ndiyo apande daraja siyo mtindo ambao uko kwenye corporate world. Mimi nimefanya kazi huko kwenye mitandao, hupandi wewe mpaka umeonesha mchango wako kwenye hiyo kampuni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sikatai watumishi kupanda, lakini kila mtumishi afahamu kwamba ana mchango wake katika nchi hii. Mchango wa kuboresha uchumi na huduma za jamii, siyo tu nimekaa kwenye dawati sichangii chochote baada ya miaka miwili naanza kudai kupandishwa, hapana, ni lazima tuanze kuangalia uwajibikaji katika eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumzia habari ya uwekezaji kwenye mifuko, kwamba siyo suala geni, lakini ni wapi tunawekeza. Ukiangalia South Africa wanasema; “the social security corporation is the major investor in the tourism sector.” Kwa hiyo, uwekezaji kwenye mifuko ya jamii ni jambo la kawaida, lakini tuhakikishe tu kwamba watu wanaostaafu wanapata mafao yao, kwa hiyo, uwekezaji ni jambo la kawaida na tuwekeze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naona unavyoendelea kufunga naomba tu kwamba NEMC kwa maana ya Baraza la Mazingira, sisi kama Kamati tumetaka iwe mamlaka kwa sababu tunataka mazingira yasimamiwe, hakuna uchumi pasipo mazingira. Kwa hiyo, jambo hili wenzetu ambao wataliangalia katika hatua inayofuata ni lazima waliangalie jambo hili ili mazingira ya nchi hii yaweze kusimamiwa na uchumi wetu uweze kuwa endelevu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia, ahsante sana. (Makofi)