Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Morogoro Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu ya Wizara ya Mipango na Wizara ya Fedha. Nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika nchi yetu ya Tanzania, katika kuimarisha uchumi katika sekta mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha kwa kazi kubwa anayoifanya yeye na msaidizi wake, ndugu yangu Mheshimiwa Chande na Mheshimiwa Waziri wa Mipango ndugu yangu Mheshimiwa Profesa Kitila na msaidizi wake, ndugu yangu Mheshimiwa Stanslaus Nyongo na watendaji wenu wote kwa kazi kubwa ambayo mnaifanya katika kumsaidia Mheshimiwa Rais ili ndoto yake na azma yake katika kuwatumikia Watanzania iweze kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono hoja na sababu kubwa ya kwanza ya kuunga mkono hoja, wakati tunapitisha bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kulikuwa kuna suala la ujenzi wa Barabara ya Bigwa – Kisaki, kilometa 78 kutoka Morogoro – Mvuha, lakini vilevile kulikuwa kuna ujenzi wa Barabara ya Ubena Zomozi – Ngerengere, kilometa 11 tukiwa tunakwenda Mvuha – Matemele Junction, kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere na Hifadhi ya Mwalimu Nyerere. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 5 Februari Barabara ya Bigwa – Kisaki iliwekwa saini ya shilingi bilioni 132 na point, lakini tarehe 7 Februari tuliweka saini na mkandarasi kujenga Barabara ya Ngerengere – Ubena Zomozi, kilometa 11. Kwa hiyo, yote haya kwa sasa hivi ninachojua wakandarasi wameshakamilisha document, kinachosubiriwa ni advance payment ili kazi ianze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wana-Morogoro kwa Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan kila kitu tushakamilisha kilichobaki ni barabara tu. Sasa kusema kwamba unataka kupinga bajeti itakuwa ni kitu ambacho hakiwezekani, maana yake nakwenda kusema kwamba barabara hizi hazijengwi. Kwa hiyo, nikuombe tu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, nikupongeze kwa kazi kubwa ambayo ameifanya. Kwanza, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu, nianze na suala la kusikia kilio cha Kamati wakati tunazungumzia suala la fedha ya wharfage iendelee kubaki TPA na itoke kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiuhalisia bandari ndiyo lango la uchumi wa nchi yetu hii na katika misingi ya kuweza kupata fedha lazima tuwe na magati mengi ambayo yataweza kusaidia kukusanya fedha. Tuliambiwa kwenye Kamati, gati moja linajengwa kwa thamani ya kati ya shilingi milioni 150 mpaka shilingi milioni 180, lakini gati moja kwa mwaka lina uwezo wa kukusanya kodi kwenda TRA na TPA karibu shilingi trilioni moja kila mwaka kwenye wharfage zinazokusanywa tunaweza hata kujenga magati matano mpaka sita. Ni nini maana yake? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakuwa na uwezo wa magati mengi ambayo yataingiza fedha nyingi na kuweza kutusaidia kwenye bajeti ya Taifa. Ninajua kabisa, ndugu yangu Mheshimiwa Mtenga hapa, kule Mtwara kuna suala la ujenzi wa Gati la Mwigalo, gati ambalo linakwenda kusaidia kupokea makaa ya mawe na kuondokana na uchafu kwenye Mji wa Mtwara. Kwa hiyo, ninaamini kabisa kwa TPA kukaa na fedha hii wao wenyewe wataweza kufanya mambo makubwa katika bandari zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu tu kwa Mheshimiwa Mwigulu, hebu tuangalie, maana tumesema fedha hizi zitakwenda kwenye Benki Kuu na kutakuwa na utaratibu maalum wa kuzichukua. Hebu tuangalie kusiwe na urasimu kwenye kuchukua fedha hizi, ili TPA iruhusiwe ikafanye kazi ambayo, sisi kama kamati tumeomba, lakini Watanzania wanaomba fedha ipatikane na iingie kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia nafasi hii vilevile kumpongeza Mheshimiwa Mwigulu na Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo wameifanya katika ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Sasahivi tunakwenda kwenye 90% naa, lakini katika Bwawa la Mwalimu Nyerere, mimi nitaendelea kuwa mtetezi wa Wanamorogoro na Wanapwani, mpaka tunafikia dakika hii hakuna CSR ambayo imetoka kwenye mikoa hii miwili.
Mheshimiwa mwenyekiti, ombi langu wakati tunakuja kwenye ku-wind-up, hebu tuambiwe Wana-Morogoro na Wanapwani haki yetu tutaipata vipi? Tulichoambiwa na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kwamba, kinachotakiwa ni watu wa Morogoro na watu wa Pwani wakae na TANESCO na wakae na Wizara, ili kuona ni jinsi gani ambavyo fedha hii itapatikana na ni kitu gani kifanyike kwa maendeleo ya wananchi wa mikoa hii miwili? Naomba, tunapokwenda kwenye ku-wind-up kwenye bajeti, najua Waheshimiwa Mawaziri wengi watasema, basi tuambiwe Wanamorogoro na Wanapwani haki yetu ya CSR ya Bwawa la Mwalimu Nyerere tunaipata lini?
Mheshimiwa mwenyekiti, mimi nachelea, kama tutakuwa hatuna majibu yaliyokuwa sahihi basi, Bunge lijalo, sisi Wanamorogoro na Wanapwani tutaleta hoja binafsi ya kudai CSR yetu. Naomba tusifike huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine ninapongeza, mimi ni mkandarasi naomba ni-declare interest. Nampongeza Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kwenda kwenye suala la kuwajali wakandarasi wazawa. Nakupongeza Mheshimiwa Mwigulu na Mheshimiwa Bashungwa, Waziri wa Ujenzi, kwa kutimiza maono ya Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwenu ni kiuhalisia kuna mambo ambayo sisi Umoja wa Wakandarasi na Watoa Zabuni tumetoa kwenye Serikali tunaomba yafanyiwe kazi. Kuna suala la withholding tax wanayokatwa wakandarasi na watoa huduma, ni kubwa, tunakatwa asilimia tano ya contract, ndani ya nchi hii hakuna biashara yoyote unayoifanya ambayo utapata faida ya zaidi ya 10%. Ni nini maana yake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapopewa mkataba wa shilingi 1,000,000,000 unakwenda kukatwa withholding tax ya shilingi 50,000,000 wakati wewe matarajio yako ya faida ni shilingi 100,000,000, kodi ni 30%, ni shilingi 30,000,000. Serikali inachukua shilingi 50,000,000, shilingi 20,000,000 zaidi. Hapa tunawaua wakandarasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye hilohilo kuna suala lingine la maboresho ambayo tumeyaleta sisi, kama wakandarasi. Kuna suala la malipo kwa haraka, wakandarasi wengi wamefilisiwa na benki kwa sababu, wanadai Serikalini muda mrefu. Asilimia ya riba inaongezeka, wanafika mahali mali zao zinauzwa na wanafilisika kwa hiyo, naiomba Serikali katika maboresho yake, hebu iangalie kipengele cha kuona tunafanyaje kuwalipa wakandarasi kwa haraka, ili waondokane na riba ya benki na kufilisika wanaposhindwa kulipa madeni hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine, kuna suala hili la withholding tax, badala ya kulipa asilimia tano tumependekeza asilimia mbili, lakini kama Serilkali inaona hapo ni padogo basi, twende kwenye asilimia tatu na tuachane na suala la wakandarasi. Wakishalipa kodi hiyo ya asilimia tatu ya withholding tax biashara iwe imekwisha, hakuna malipo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kingine, kuna suala mama yetu amezungumzia la kutokurejesha nyuma kufuatilia masuala ya kodi. Bado suala hili linaendelea, sisi kama wakandarasi tumelileta suala hilo. Naiomba Serikali, hebu liangalieni, mliafanyie kazi, ili tuweze kufikia pale Mama anapotaka. Badala ya fedha kwenda nje, China au India, ibaki nyumbani, uchumi uendelee kukua na sisi tutengeneze mabilionea wengi Wakandarasi wa Kitanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ambalo napenda kulizungumzia ni kwenye suala la utalii. Mimi natoka Morogoro Kusini, kule tuna hifadhi ya Mwalimu Nyerere, lakini ninachojua kwa sasa hivi ni utalii umeongezeka. Kwa ripoti ambayo tumepewa, tulikuwa na watalii 928,000 sasa hivi tumekwenda 1,800,000. Kiuhalisia sisi Tanzania tuna vivutio vingi, ukijaribu kuangalia katika dunia, Morocco wana watalii 10,000 kwa mwaka, lakini hawana vivutio vingi vya asili kama tulivyokuwa navyo Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kwa sasahivi tuendelee kutangaza mbuga zetu, hasa kwa ukanda wa Kusini ambao kuna Morogoro – Hifadhi ya Mwalimu Nyerere, kuna Mikumi, kuna Udzungwa, kuna Katavi, kuna Ruaha Mkuu, ili mapato yatakayopatikana upande wa utalii wa Kusini yaingie kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na kuongeza pesa za kigeni kwenye nchi ziweze kusaidia kuleta maendeleo katika Tanzania. Baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)