Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ushetu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, binafsi nakushukuru sana kwa jinsi unavyotuongoza, lakini mimi binafsi namshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema, kwa kibali cha pekee ambacho ametuwezesha kuendelea kuwepo hapa na kuendelea kujadili Bajeti ya Serikali. Nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Daktari, mtu bingwa kabisa, Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba, pamoja na Profesa, kwa kazi kubwa ambayo mnaifanya lakini pia kwa bajeti yenu nzuri sana iliyojaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambazo amewafanyia wananchi wa Jimbo la Ushetu, kwa miradi mikubwa aliyoileta kwa wananchi wa Ushetu. Nasema tu kwamba, kwa kweli, Mheshimiwa Rais anafanya kazi kubwa sana. Mheshimiwa Rais, Wananchi wa Jimbo la Ushetu, juzi tu wakati tuko pale tunazindua na kusaini mkataba wa shilingi 44,000,000,000 wa Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu alikuwa mgeni rasmi pale, aliwashuhudia wananchi wanavyomshangilia Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambazo amezifanya. Ni tukio la historia kubwa sana kwa Wananchi wa Ushetu kwa sababu ni miaka mingi sasa walikuwa wanalia na hicho ndicho kilikuwa kilio chao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, binafsi nampongeza sana Mheshimiwa Bashungwa kwa kweli, amefanya kazi kubwa kwa wananchi wa Ushetu. Barabara nyingi ambazo zilikuwa zimeshindikana toka uhuru, Barabara ya Uyogo – Ulowa ambayo ina kilometa 30 ilikuwa imeshindikana, lakini leo wananchi pale wanapita wanamshangilia tu Mheshimiwa Rais. Ni kazi kubwa Mheshimiwa Bashungwa umeifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, tuna Daraja la Ilangashiga ambalo mkandarasi yuko kazini nalo lilishindikana. Tuna Daraja la Ubagwe ambalo nalo lilishindikiana, lakini lina mkandarasi. Pia, tuna Daraja la Igombe River, nalo lilishindikana, lakini Mheshimiwa Bashungwa mifupa iliyoshindikana amekuja kuitafuna. Hongera sana, Mwenyezi Mungu akubariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuishukuru sana Serikali kwa kazi kubwa ambayo inaifanya. Kwa kweli, ni kazi kubwa sana Mheshimiwa Rais anafanya. Hapa najikita kwenye mada zangu, mwaka 2021, Sheria ya Withholding Tax ililetwa hapa Bungeni ambapo wakulima walilazimika wakatwe asilimia mbili, lakini kabla ya utekelezaji Sheria ikapita Bungeni na bahati nzuri Mheshimiwa Rais akaisaini, lakini utekelezaji wake ulikuwa mgumu sana kwa wakulima, kelele zilikuwa kubwa sana. Tuliirudisha tena hapahapa Bungeni mwaka 2022, tukaijadili tukaiondoa kwa sababu, utekelezaji wake ni mgumu, lakini leo hii tena wakulima hawa tumewaletea suala la kodi asilimia mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima hawa bado ni masikini sana. Wakulima hawa ninyi Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, mkulima huyu mdogo, ambaye anateseka na jembe la mkono kuanzia mwezi wa nane, mwezi wa tisa, mwezi wa 10, mwezi wa 11, mwezi wa 12, mwezi wa kwanza, mwezi wa pili mpaka mwezi wa sita mwaka unaofuata ndiyo anaanza kupokea pato lake ambapo mkulima mkubwa sana anaweza akawa na kipato cha shilingi milioni mbili, milioni tatu au milioni nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunampelekea tena makato ya asilimia mbili ambayo tuliyajadili sisi wenyewe humuhumu Mwaka 2021, Sheria ikatushinda tukaiondoa, tukairudisha mwaka 2022, leo tena tunaenda kuwakata hawa wakulima. Mimi naendelea kumuomba sana Mheshimiwa Waziri, hii kodi aiondoe kwa wakulima. Mazao yetu haya yote ya pamba, tumbaku, korosho, kahawa na mazao mengine, yote yamepitia katika wakati mgumu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji ulipungua mwaka 2018, 2019, 2021, katika mazao haya, yote yalipitia katika mtikisiko mkubwa. Mheshimiwa Rais ameingia madarakani, kwa miaka mitatu ya Mheshimiwa Dtk. Samia Suluhu Hassan, sasa mazao yameenda kutengemaa. Kutengemaa kwa mazao haya, tunaenda kuyaingizia kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaenda tena kuwavuruga wakulima wetu. Hatuwezi kuwapelekea kodi wakulima hawa wanaoteseka na jembe la mkono, hatuwezi kuwapelekea asilimia mbili wakulima hawa wanaohangaika shambani kwa kipato kidogo kwa miezi 12. Hatuwezi kuwapelekea kodi hawa wakulima ambao ni wachache, wako chini huko wanateseka ambako hata gharama za uzalishaji hawazijui.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunawapelekea kodi, tunaenda kutokuwatendea haki wakulima. Nikuombe mwaka 2019/2020 mfano tu kwenye zao la pamba hali ilikuwa ni ngumu sana, sasa leo ushindani umeongezeka, kabei kanachangamka, wanunuzi wanaendelea kuongeza bei, mkulima anaenda kufurahia tunanyanyuka tena kumwambia sasa atozwe asilimia mbili, hii bado haikubaliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa tumbaku hawa waliokuwa wameteseka na tozo nyingi 2018, 2019, 2020 uzalishaji ulitoka tani 200,000 mpaka ukaja tani 34,000 na Pato la Taifa lilipungua mpaka dola 148,000. Mheshimiwa Rais ameingia madarakani ameondoa baadhi ya kodi, amesamehe baadhi ya madeni, leo tena tunaibuka uzalishaji wa tumbaku umetoka tani 34,000. Leo kipindi cha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tumeenda tani 200,000. Pato la Taifa limetoka 148,000 limeenda kuwa dola 484,000 Pato la Taifa limeongezeka. Sasa tunaenda kuwanyang’anya hata kile kidogo ambacho wanakipata waweze kuendesha uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii naendelea kuisisitiza kwamba tukubaliane hii tuiondoe, tuiondoe kabisa kwa sababu tunaenda kuwaumiza wakulima wetu. Mimi niendelee kuwaomba Mheshimiwa Daktari na Profesa wako hapa sifa kubwa ya mtaalamu ni kutengeneza uchumi na kodi ambayo ni rafiki kwa wananchi wetu siyo kuwa na maumivu kwa wananchi. Ng’ombe lazima umchunge, umnenepeshe, umpe dawa, siyo kabla haujamlisha unaanza kumkamua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kukuomba suala hili tuweze kuliondoa kwa sababu leo utakapo mwekea kodi mkulima, mnunuzi anachokifanya ni kupunguza bei kwa mkulima. Wakulima hawa hawa ni wachangiaji wazuri mbona kwenye mapato? Leo hii asilimia tatu ya halmashauri si inaenda kwa mkulima? Mnunuzi unapomwekea tu yeye ataenda kupunguza bei kwa mkulima wala hahangaiki na kitu kingine. Kwa hiyo, niendelee kukuomba hili suala bado ni changamoto sana kwa wakulima wetu, tunaomba suala hili hata kwenye bajeti ya fedha tumelijadili sana kwamba vyama vya msingi navyo viwe na mashine ya EFD, hatuwezi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima hawa wanajiunga kwenye AMCOS ili waweze kupata soko, ni wale wakulima wadogo wadogo wanajadiliana wanajiunga kutengeneza chama chao cha msingi. Vyama vya msingi havina fedha, fedha hii ni ya wakulima hawa waliojiunga na inapoingia kwenye akaunti, ukiingia kwenye schedule unaweza ukaona ni bilioni mbili ziko kwenye AMCOS A, kumbe fedha hizi zinaenda kwa wakulima wadogo wadogo wote chama kinaachwa bila hela yoyote, kinaachiwa ushuru tu kidogo kwa ajili ya kujiendesha. Sasa unaenda kuwakata asilimia mbili, halafu unabeba tena unawaambia chukueni mashine ya EFD kwenye AMCOS zao, wakulima watakachofanya ni kusambaratika na kuvikimbia vyama, tunaenda kuua ushirika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kukuomba kupitia Bunge lako Tukufu, tuondoeni kodi kwa wakulima, waende kulima watengeneze fedha. Hakuna mkulima ambaye anazalisha zaidi ya shilingi 10,000,000 kwa mwaka, hayupo ni wakulima wachache mno hata tukifanya sensa hapa. Mimi nina declare interest mimi ni sehemu ya wakulima wale wadogo ambao wanateseka kule shambani. Tuondolee kodi wakulima kwa sababu tunapowaondolea kodi wanaenda kuzalisha, wanapozalisha kwa wingi ni Pato kwa Taifa, wanapozalisha kwa wingi ni utulivu kwa nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa pamba tu, ni Mikoa zaidi ya kumi na mbili inalima pamba, ni zaidi wilaya 29 zinalima pamba ni wakulima wangapi wako kule vijijini ambao wanasubiria kwamba je, tunaenda kuwekewa kodi asilimia mbili? Waheshimiwa Wabunge kelele yake tunapoenda tutaenda kui-solve kwa wananchi wetu? Mimi niendelee kwa usikivu huu Mheshimiwa Waziri, tuondoleeni hii kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nimeiongelea kwa uchungu sana, kwa sababu kelele tunazozipata kule kwa wakulima wetu ni kubwa sana, leo wakulima wa tumbaku bei ilishuka kuwa dola 1.5 kwa kilo. Kipindi cha Mheshimiwa Rais na tunavyoongea leo wastani wa bei na soko linavyoenda ni dola 2.5 ni Mheshimiwa Rais ametengeneza soko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niendelee kuomba tulindeni wakulima wetu wanaojenga uchumi wetu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa naomba uhitimishe…
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: …tunao watetea zaidi ya 70% ni wakulima wetu wa Tanzania na Mheshimiwa Rais amewatengenezea soko linazidi kupanda kila wiki, kila mwaka linaenda kuongeza, uzalishaji umepanda sana. Kwa huu utulivu ulipo kwa wakulima wetu ni mkubwa sana, tuendelee kuulinda, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)