Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha jioni hii ya leo. Napenda kuipongeza Serikali, Mheshimiwa Rais na Wasaidizi wake wote kwa bajeti hii nzuri na mipango mikakati ya maendeleo ya nchi yetu. Nawapongeza Mawaziri wote wawili Waziri wa Fedha, Waziri wa Mipango na Manaibu wao pamoja na watendaji wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najielekeza kwanza kwenye mpango; kwenye mpango kuna mipango mikakati ya kuhakikisha kilimo kina tija kwa maana ya mikakati ya kwamba tija katika kupata mbegu bora, kupata uwekezaji kwenye kilimo cha umwagiliaji, kuongeza maafisa ugani na mambo mengine, naipongeza kwa hatua hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naipongeza Serikali kwa kuongeza Bajeti ya Kilimo kwa maana ya kwenda kuhakikisha sasa kilimo kweli kinaleta tija kwa wananchi, wakulima na Taifa. Hapo hapo napenda kushauri, kuna mpango mkakati wa kuongeza viwanda vya mbolea nchini, nashauri viwanda vya mbolea viendelee kuongezeka kwa maana ya viwanda vikubwa, vya kati na vidogo na kwa maana ya kwamba tuweke pia mkakati kwenye mbolea zetu za asili ambazo hazitumii kemikali yoyote kwa maana ya kupata vyakula ambavyo vinahitajika duniani. Kwa sababu vyakula hivyo vina soko zaidi (hayo mazao ambayo hayatumii kemikali) na pia wananchi wa humu ndani sasa hivi hayo mazao wanayatafuta kwa sababu ya kulinda afya zao. Kilimo kile kiendelee, lakini na kilimo hiki kingine kiendelee kikiwemo kilimo hai na kilimo hifadhi. Tutenge kabisa bajeti ya kuendeleza kilimo hai na kilimo hifadhi kwa faida yetu yetu, wananchi na ardhi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo kwenye kilimo twende tuongeze uzalishaji wa humu ndani kwa viuatilifu vya mazao mbalimbali kuepusha wananchi wetu na wakulima wetu kuletewa viuatilifu feki au ambavyo havina ubora au vimezidi viwango ambavyo vinahatarisha maisha ya mwananchi katika hayo mazao yanayozalishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijielekeze sasa hivi kwenye sekta ya uvuvi. Naipongeza Serikali kuingia kwenye uvuvi wa bahari kuu, tunajenga gati yetu kule Kilwa ya bandari ya uvuvi lakini Serikali iendelee na ule mchakato wa kununua meli za uvuvi pamoja na kuhakikishika Shirika la TAFICO linaanza kazi, kwa sababu hili Shirika litakapopewa fedha za kutosha tukakamilisha miundombinu yote likaanza kazi pale pesa zipo, pesa zipo sana kwenye uvuvi. Shirika hili lisipewe pesa kwa awamu awamu, tutafute fedha za kutosha tuachane na hili Shirika liendelee kufanya kazi tupate mapato tuwekeze kwenye miradi mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta ya mifugo napenda kuvipongeza viwanda vya ndani na hasa kiwanda kilichoanzisha utengenezaji wa maziwa ya unga. Hapa tutaokoa fedha nyingi za kigeni kuagiza maziwa ya unga. Kumbe maziwa ya unga ni uwekezaji mkubwa, imetumika karibu shilingi bilioni 22 kwenye kuweka mitambo tu ya uzalishaji wa maziwa ya unga. Tukilinde kiwanda hiki na tuhamasishe na wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie hizi kodi mbalimbali ambazo zitakuja kurejesha nyuma uwekezaji huu. Nawashauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Waziri wa Uwekezaji mwende kule kwenye kiwanda msipite nje mkaone ndani hali ilivyo mtashangaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye maziwa tumesamehewa yaani wafugaji wamesamehewa mambo mengi yanayohusu mifugo na maziwa. Tunaishukuru Serikali kwa kuondosha baadhi ya tozo na baadhi ya kodi. Hata hivyo naishauri Serikali kwenye hii sekta ya maziwa basi yasamehewe maziwa yote kwa maana ya maziwa ya unga na cheese, kwa sababu maziwa ya unga siyo anasa tunataka kuepukana na lishe duni na utapia mlo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, tukiweza kutoa kodi kule, maziwa ya unga yatanunuliwa kwa wingi kwa sababu kuna baadhi ya wananchi wetu hawana hayo majokofu ya kuhifadhia haya maziwa ya kawaida kwa hivyo watakaponunua maziwa ya unga atajenga afya yake na watoto wake lakini ikiwa bei iko juu yatashindikana kununuliwa. Nashauri iangaliwe sana hapo kwenye kodi hizo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi nataka nijielekeze kwenye mpango, nimeona ukurasa wa 59 kuna kipengele kinasema tutaimarisha, kukuza na kubidhaisha Kiswahili Kitaifa, kikanda na kimataifa. Mwenyezi Mungu katupa neema, sasa hivi wenzetu wanahangaika kuhakikisha hili soko wanalikamata, sasa sisi Tanzania wenye hii mali tutakuja kunyang’anywa na kwa sabbu kuna nchi wenzetu tayari sasa hivi wanafunzi wao wamewalazimisha lazima wawe na dictionary ya Kiswahili na lugha yao nyingine kama Kifaransa au Kingereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwenye hii mipango tuseme sasa ndani ya mwaka mmoja tutawawezesha na kuwaandaa wakalimani wangapi? kama ni mia tatu kama ni mia mbili. Tuna mpango gani wa kuongeza walimu wa Kiswahili kama ni mia nane kama ni mia tisa, tuwe na takwimu kwa sababu tusipokuwa na uhakika wa kuwekeza kwenye hili soko, soko hili tutanyang’anywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema tu kuna nchi moja ya mbali ya Asia tayari wao wamejitangaza wana walimu wa Kiswahili na tayari wameshapata soko na wanasomesha huko duniani. Sisi tumekaa Kiswahili cha kwetu, Kiswahili cha kwetu. Wanachapisha vitabu, wanachapisha dictionary, wakienda kuchapisha nchi jirani ikawepo ile ilama wanaona ndiyo kule Kiswahili.kilikotoka (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuhakikishe tunawekeza mitambo ya kutosha hapa nchini tuchapishe machapisho yetu, dictionaries zetu na vitabu vyetu hapa ndani ya nchi ili kutangaza jina letu kama hii ni mali ya Tanzania. Pia tutafute, hivi Kiswahili ni hatimiliki ni ya nchi gani? Kwa sababu tusipojua hatimiliki ni ya nchi gani tutakuja kunyang’anywa. Nimeshasema hili tayari watu wameanza kusema Kiswahili ni cha nchi fulani kwa sababu anaona yale machapisho, wanaona vile vitabu, wanaona vimechapishwa nchi fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tupambanie, hii ni rasilimali, hizi ni ajira. Ndani ya Tanzania tunafanya mikutano yetu ya kimataifa lakini ukiweka kusikiliza mkalimani anatoka nchi jirani. Ile lafudhi na yale matamshi ni ya nchi jirani. Kweli tumeshindwa hapa kukidhi vigezo vya kuwa na wakalimani wa kutosheleza ndani ya mikutano yetu hata ya ndani ya nchi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo sisi tunaliona ni jepesi lakini wenzetu wanalichukulia kwa uzito mkubwa na wanakuja Tanzania sasa hivi kwa wingi kuja kuona utamaduni wa Mswahili na hiyo Lugha ya Kiswahili. Tusiipoteze hii fursa, ukalimani ni muhimu duniani, ualimu ni muhimu duniani. Tutengeneze mazingira ya vijana wetu na kwanza, mfano vijana wetu wenye ulemavu hii ni nafasi nzuri kwao kwa ajira kwa sababu haitumii nguvu kubwa ni kuwaelemisha tukawaongezea uwezo wa lugha mbalimbali na tukawapa mafunzo ya ukalimani, watafanya hii kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo msisitizo wangu kwenye lugha ya Taifa ya Kiswahili. Tuipigie debe lakini kwa kuiwekea mikakati maalumu na mizito ili kuhakikisha lugha hii na utajiri huu hatuporwi na mataifa mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho namalizia kwa kuipongeza Serikali kwa kuiweka nchi yetu kuwa salama na yenye utulivu amani ya nchi inaendelea nawapongeza viongozi wote kwa kazi kubwa wanayoifanya kutuletea wananchi maendeleo. Nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)