Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Jumanne Kibera Kishimba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kahama Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye huu Mpango wa Bajeti ya mwaka 2024/2025. Kwanza nimpongeze Waziri wa Fedha na Timu yake, Waziri wa Mipango na wasaidizi wake kwa bajeti hii ambayo nafikiri tunakwendanayo vizuri. Kikubwa zaidi nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kutuongoza wakati huu wa matatizo makubwa ya uchumi duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye hoja. Mimi Jimbo langu au Mji wangu wa Kahama ndiyo umeongoza Tanzania kwa Mapato lakini pia ndiyo unaongoza kwa barabara mbovu. Sasa nikuombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Waziri wa Mipango hebu nipangie vizuri kama unaweza kunipa mkoa wa kibarabara utakuwa umenisaidia sana. Kwa sababu wewe unakusanya pesa nyingi unafurahia unanipa zawadi ya ushindi wa mapato lakini unanichonganisha na wananchi wangu, kwa sababu wewe umekusanya pesa kwa njia ya mtandao hupiti barabarani kwa sababu mtandao haupiti barabarani, mtandao unaruka juu, ungekuwa unapita barabarani na wewe ungeona lakini sasa hivi mtandao haupiti barabarani. Naomba, naomba sana sana unisaidie sana kwenye suala la barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vitabu vya Mungu, Biblia, Quran hata mila za wenyeji ni vitabu vimetengenezwa ili binadamu waishi na vimetengenezwa kwa kuzingatia vitu vingi sana, lakini sisi hapa tunaleta sheria ya kumwadhibu mtu ambaye hakutenda kosa kulipa faini ya shilingi milioni 15 au kwenda gerezani au vyote viwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, anayekaa kwenye biashara siyo tajiri anayekaa kwenye biashara ni mfanyakazi. Sasa mfanyakazi hakutoa risiti unasema utamfunga tajiri, si matajiri wote utawamalizia gerezani? Lakini huyu mnunuzi anachukuaje mali ambayo haina risiti, kwa nini na yeye asikamatwe? Kwa sababu mali haina risiti, wewe umetoa hela hukupewa risiti unatokaje dukani? Maana yake ukikutwa na ile mali basi ni mali ya wizi, kama mali haina risiti ni mali ya wizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo matajiri wana-branch ngapi Tanzania? Haya kina Azam, kina Bakheresa kina nani wote mtawamalizia gerezani, kwa sababu analewa na gari yake iko Ngara nyingine iko Tabora, mfanyakazi hakurudi maana yake shilingi milioni 15 itamu-encourage kila mtu kwenda kumshambulia huyu tajiri. Sasa mimi naweza kuwa gerezani kwa kosa hili, shughuli zangu za biashara zinaendelea kwa hiyo mashtaka yatakuwa yananifuata gerezani. Nitakuwa naongezewa tu miaka tu kule kule gerezani, kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake Serikali ni kama mchungaji wa mifugo, haiwezekani mchunga mifugo akawa na hasira dhidi ya mifugo yake. Mwananchi ni kama mifugo ya Serikali, sasa mfugaji gani huwa ana hasira? Mchungaji hanaga hasira. Huwezi ukawa na hasira ukifikia kiasi cha kusema kwamba mimi sasa nataka niwauwe hawa ng’ombe sasa utachunga nini? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya biashara, ndiyo maana wewe unasema hakuna mapato ni kweli hakuna pesa. Leo maduka yote yamejaa plastiki, wachina wamechukua zile hela zimeishaenda. Nyumbani wote humu ndani Waheshimiwa Wabunge ukipata shida unaweza kuuza nini ndani? Wote tunamiliki plastiki hatumiliki chochote, hela zimeenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya bei ya mahindi leo shilingi 30,000 utauza gunia ngapi ili wewe Serikali upate hela? Kwa hiyo, hali ya biashara ni ngumu, fikiria sana hili suala. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu wewe mwenyewe una timu ya mpira je, mtu akichenga pale bila kutoa tiketi kwenye mpira ukamatwe wewe? Maana yake huyu ni mwizi kakuchenga wewe, haiwezekani. Mheshimiwa Bashe ana bucha, ana mabucha mawili, bucha yake sasa hivi Dar es Salaam mtu katoka kuchukua nyama bila risiti, kweli utakuja umkamate Mheshimiwa Bashe humu Bungeni... (Makofi/Kicheko)

MBUNGE FULANI: Na Nzega.

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, itawezekani kweli? Na Nzega anayo. Sasa itawezekana kweli? Lazima tufikirie kwamba huyu anayechukua ile nyama bila risiti ndiyo mwenye kosa. Huyu tajiri anashirikije kwenye huo wizi? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuliangalie kwa mapana sana. Kila siku mimi nasema humu matajiri wachache mno ndio wazima, wengi wanashinda na vidonge wanameza vidonge kutwa nzima kwa matatizo makubwa mno. Alikuwepo hapo Meneja wa CRDB, mngemuuliza aeleze statement ya matatizo waliyonayo wafanyabiasha wa mikopo ni makubwa mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona niliseme kwa sababu umesema naongoza lakini simu ninazopata kule kwa wafanyabiashara wangu kwamba tumeongoza mapato. Halafu tarehe moja mnaanza tukukamata kwa risiti maana yake watu hawa watafanyiwa uhuni na collaboration itakuwa kubwa mno ya utapeli. Hali ya utapeli ni mbaya sana sasa hivi, itakuwa ni tatizo…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa faini ya trafiki…

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, faini ya trafiki ni shilingi 30,000 watu hawalipi, wanampa trafiki shilingi 3,000 wanaendelea hawalipi. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha lifikirie sana kwa mapana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la afya, mara mara najaribu kuliongelea sana, najua nikiwambia dawa hautakubali kuwapa wananchi bure lakini tuna sheria nyingi sana za kikoloni kwenye suala la afya. Leo tuna madaktari zaidi ya 7,000, 8,000 waliomaliza hawana ajira. Waliostaafu wapo zaidi ya 7,000, 8,000 medical assistant wapo, wafamasia wapo kwa nini watu hawa wasipatiwe na wao leseni kama za mganga wa kienyeji kwa shilingi 30,000 kufanya shughuli zao? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanye shughuli zao, wengine wamebakiza miaka nane kustaafu na kazi hawajapata na ninyi mnawadai je, mtawadai wakiwa wamestaafu? Waruhusuni watibu watu. Hali ya hospitali Waheshimiwa Wabunge tunaifahamu ilivyo, tuna zahanati zetu zinatibu watu mpaka sasa tano asubuhi, kuanzia ile asubuhi mpaka jioni si ziko tupu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, daktari aweke bango pale kwamba mimi natibu kwa bei hii, ukija hata na mbuzi nitapokea au kama huna hela ukipona utakuja ufanye kibarua kwangu, tatizo litakuwa nini? Wananchi watasubiri huyu saa tano, wataacha hii ya kwenu, bwana ninyi malizeni ya kwenu ya Serikali mimi nasubiri ya huyu ili nikipona nitaenda kufanya kibarua. Kwani mimi nikifanya kibarua kwa matibabu kuna kosa gani? Kwa vile Serikali hatoi dawa bure, waruhusu hawa madaktari maana yake wewe ndiye uliyewapa digrii waje pale hospitali, waweke mabango kwamba, mimi natibu kwa gharama hii nafanya hivi, wafanyie kwenye zahanati zetu tumezijenga wenyewe, lakini baada ya saa nne au tano hazina watu ule muda wote. Wafanyie hapo kama wanaweza kutulipa sisi vijijini, si ndiyo tulijenga sisi, watulipe hiyo hela kama ni kodi ili kupunguza msongamano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kuliongea kwa mapana sana, maeneo ya kwetu yale ambayo yana watu wengi watu, hali yao ya umaskini ni mbaya sana. Hatu-control bei ya dawa na matibabu, watafanya nini hawa watu? Ondoeni sheria hizi mbaya za kikoloni. Tuna dawa nyingi sana zipo Kenya na Uganda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna chloroquine nitatoa mfano, Kenya na Uganda wanatumia chloroquine lakini Tanzania imekataliwa, sasa mimi najiuliza ina maana wale mbu wa Uganda walijua hapa ni Mtukura waka-stop hapo wakakataa kuja huku? Walijuaje kwamba hapa ni Uganda? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini basi wasingekuja chloroquine ikafanya kazi ikafika mpaka Nzega au Kahama ndiyo tukasema sasa imekataa, kweli inawezekana? Wote tunaamini kabisa chakula salama duniani ni cha buffet kwa sababu watu wote mnaona. Sasa kama wanatumia wakenya na waganda wewe unakataaje chloroquine isifanye kazi? Kwenye corona imetujsaidia, jaribuni kufikiria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri tunatoka hapa kwenda India kutibiwa, je, huwa tunaenda na dawa zetu? si tunatumia dawa za India? Kuna ubaya gani tukanunua dawa za bei rahisi kutoka India hawa maskini wakatumia, matajiri wakatumia za bei ghali, nilitaka tu kuliongelea hilo kwa mapana sana ili kuwapunguzia maisha ni magumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango huo nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, lakini lifikirie kwa makini sana suala la milioni 15.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango huo nakushukuru, ahsante sana. (Makofi)