Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Aeshi Khalfan Hilaly

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumbawanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. AESHI K. HILALY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia…

NAIBU SPIKA: Ajiandae Mheshimiwa Kunambi.

MHE. AESHI K. HILALY: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa sana anayoifanya, pia niipongeze Serikali yote kwa ujumla kwa kweli wanafanya kazi wanajituma na mafanikio na maendeleo tunayaona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kuwapongeza sana wanajimbo, Jimbo la Nkasi Kaskazini, Kata ya Kagwe kwa ushindi mkubwa tulioupata kwa kukomboa Kata ile ya Kagwe ambayo iliongozwa kwa takribani miaka 27 ikiwa upinzani, lakini mwisho wa siku tumeikomboa na imerudi ndani ya mikono ya CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi pia kuwapa pole Wakazi wote wa Mwambao wa Lake Tanganyika kwa mafuriko waliyoyapata na mimi kama Mbunge na Wabunge wote wa Mkoa wa Rukwa tukimaliza Bunge tutakwenda kuwapa pole. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nishauri Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Kumekuwa na changamoto ya ufungaji wa Ziwa Tanganyika kwa miezi mitatu au minne. Naomba nishauri au nitoe mawazo ambayo naamini Waziri atayachukua na atakwenda kuyafanyia kazi. Ziwa la Tanganyika huwa linajifunga lenyewe kwa hiyo hatuna sababu ya kulifunga kwa ulazima. Ninaamini hata sasa hivi lile ziwa limejifunga yaani hakuna shughuli yoyote ya uvuvi inayoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kupata mazao ya uvuvi nilitaka nishauri kwamba, tuweke maeneo ya uzalishaji wa samaki. Nitatoa mfano kule Lake Tanganyika kuna maeneo yale ya Mahale National Park. Pale Mahale pembeni yake mwa ziwa wamezungusha ring fence ambayo ni marufuku kwa mtu yeyote kuvua. Nini faida yake?

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yake yamekuwa yakizalisha samaki wengi na dagaa wengi sana. Sasa wanaonufaika ni wale ambao wako jirani Sibwesa na kule Mgambo. Mwisho wa siku wavuvi wengi wanatoka maeneo mengine kwenda kufuata uvuvi wapi? Kule ambako ni maeneo ya karibu na Mahale National Park.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Waziri kwa nini usichukue mfano huo huo, mkachagua maeneo mengine matano mfano mkaweka maeneo ya Kipili, kule Kasanga, pale katikati Ninde kwa ajili ya uzalishaji wa samaki na dagaa. Yale maeneo mkayawekea sheria kwamba ni marufuku kwa mvuvi yeyote kwenda kuvua maeneo yale. Mwisho wa siku hata gharama ya ulinzi itakuwa ni ndogo kuliko sasa hivi ambako mkifunga ziwa lile kulinda wavuvi wasiende kuvua gharama kubwa kuliko ambavyo tungeweza kutengeneza maeneo ya kuzalisha samaki yakawa ni maalum na tukaweka vifaa vya ulinzi na hatimaye tukatunga sheria kwamba, yeyote atakayekwenda kuvua pale basi akamatwe na achukuliwe hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukilifunga ziwa lote kwa ujumla wananchi wale hawana maeneo mengine zaidi ya kukimbilia kwenda kwenye uvuvi. Kwa mfano, leo hii Mheshimiwa Waziri baada ya mafuriko mashamba yote ya mpunga yamemevamiwa, mashamba ya mahindi yameharibika. Sasa mvuvi anategeme nini au mwananchi wa Kirando, Kipili, Karema na Kabwe wanategemea uvuvi, ukilifunga ziwa lile umewaua wananchi wale. Ukilifunga ziwa lile wanafunzi hawatapata elimu kwa sababu wazazi wao hawatapata pesa kwa kwenda kuwalipia ada.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka nimshauri Mheshimiwa Waziri kuliko kulifunga ziwa; nakutolea mfano mwingine mdogo tu, Eneo la Kipili lile kuna mzungu pale katikati ana hoteli pale inaitwa Lake Shore. Yeye ameweza kudhibiti wavuvi wasiende kuvua maeneo yale. Pale pana samaki na dagaa wengi wa ajabu. Mwisho wa siku wenye maeneo karibu na pale Kipili wanapata wale samaki na dagaa kwa sababu gani? Wameweka sheria ndogo tu ya kuzuia lile eneo wasiweze kuvua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri ombi langu kwako sasa twende tukatafute maeneo maalum, tutenge kama ambavyo Mahale National Park walivyotenga eneo lile, walivyozungusha yale maboya na mwisho wa siku tuweke sheria. Dagaa na samaki watazaliwa pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwako ni kwamba, sasa tuende tukatafute maeneo maalum tutenge kama ambavyo Mahale National Park walivyotenga eneo lile, walivyozungusha yale maboya na mwisho wa siku tuweke sheria, uvuvi wa dagaa zitapatikana pale na samaki zitazaliwa pale na mwisho wa siku, kwa sababau samaki zikiwa nyingi na dagaa zikiwa nyingi zitasambaa kwenda maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu nataka kuishauri Wizara, nimekuwa nikishauriana na wewe muda mrefu, toka mwaka juzi ninakushauri jambo hili unaniitikia, unalifurahia lakini halifanyiwi kazi. Sasa, nakuomba, sisi Wabunge tunaotoka Kigoma, Rukwa na Katavi tukae chini na Wizara tushauriane na mwisho wa siku tukubaliane na vilevile tuyafanyie kazi. Maana yake hatuna sababu ya kuja hapa Bungeni watu tunachangia, tunapigiwa makofi, Waziri tunakusifia lakini utekelezaji haupo. Tulikuja hapa mwaka jana tukasema hayo hayo, mwaka huu tunasema hayo hayo, mwakani tunasema hayo hayo, utekelezaji haupo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri mimi naomba, nilikuwa nataka kusemea jambo hilo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili kabisa ninawashukuru kwamba umesoma bajeti yako nzuri kwamba utaleta boti, utaleta vifaa vya uvuvi, japokuwa sisi kule Lake Tanganyika mara nyingi tunakuwa ni wa mwisho, sasa safari hii fedha hizo zikija jitahidi sana na upande wa Lake Tanganyika vijana wale na wavuvi wale na wenyewe wapate vifaa vya uvuvi, wapate mikopo waweze kujiendeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ilikuwa ni hiyo ya kuishauri Serikali sina hoja nyingine, ninaonga mkono bajeti, ahsante. (Makofi)