Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlimba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mimi nianze kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, kwa kweli nasema tu kwa dhati, Mheshimiwa Rais amekuwa akituamini vijana kwa kiasi kikubwa sana, akiwa na imani kwamba kijana atakuwa na fikra mpya katika ulimwengu unaobadilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu imejaliwa kuwa na idadi kubwa ya mifugo, tunaambiwa Barani Afrika ni nchi ya pili ukiachana na Ethiopia, lakini ukitazama tija ya mifugo hii kwa Watanzania unaambiwa hapa inachangia kwenye Pato la Taifa kwa asilimia saba, kitu ambacho ninadhani ni sehemu ndogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mifugo kuwa mingi siyo laana, mifugo kuwa mingi ni uchumi kwa Taifa letu lakini sasa mifugo imegeuka kuwa migogoro kwa wananchi. Leo hii utasikia migogoro baina ya mfugaji na mkulima, leo hii utasikia migogoro ya wafugaji na mamlaka za uhifadhi, kundi hili la wafugaji limeachwa kama mtoto yatima, wafugaji wameachwa wanajiendesha wenyewe, hatuwezi kufika! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwambia Kaka yangu Mheshimiwa Ulega you are my brother, wewe bado ni kijana tunaamini utafanya mabadiliko makubwa na msaidizi wako. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimelifanyia tafiti ndogo tu kwa wafugaji, wafugaji wanaambiwa punguzeni idadi ya mifugo, haiwezekani! Kwa sababu wafugaji wanasema hivi, mifugo yangu ni sawa na wewe kuwa na akaunti ya benki na mnada ndiyo ATM yangu. Sasa, ukiniambia nipunguze mifugo, ah! Mheshimiwa Mbunge kwa nini wewe benki yako usipunguze fedha kwenye akaunti yako? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mkulima anasema, mimi mkulima thamani yangu ni mazao yangu, mfugaji thamani yake ni mifugo, sasa wote hawa kila mmoja anapaswa kumheshimu mwenzake lakini kundi hili la wafugaji limeachwa wanajiratibu wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano pale Jimboni kwangu, mwaka jana Kata ya Mofu kulikuwa na mapigano kati ya wafugaji na wakulima na wananchi wawili wakapoteza maisha. Ukienda leo hii ninavyozungumza, kuna mgogoro pale Kata ya Utengule eneo la Ndefi, watu wa hifadhi TAWA na watu wa kile kitalu chetu pale wanagombana. Sasa, nikafanya tafiti kwa mfano Ireland mkulima na mfugaji ni marafiki, walifanyaje tu Ireland ninakupa tu elimu Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, walichokifanya Ireland waliwaambia wakulima kwa kuwa wafugaji, mfugaji hahitaji ardhi niwaambie ukweli, Mfugaji anahitaji malisho na mnielewe tu hapo. Mfugaji haitaji ardhi anahitaji nini, malisho. Sasa, elimu ninayokupa Mheshimiwa Waziri ni kwamba wakulima wapewe elimu kwamba, okay, ninyi mnaokaa karibu na wafugaji mashamba yenu limeni nyasi ni biashara, huyu mfugaji utamkodisha hapa. Inawezekana ikawa biashara baina ya mkulima na wafugaji, uka-harmonize. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, tunazo ranchi mbalimbali, tunayo ranchi ya Mkata na ranchi ya Kongwa. Kwa nini tusiwaambie wafugaji waje pale? Lakini kuna teknolojia wataalam wanasema kila ng’ombe mmoja anakula eneo la hekta moja ni sawa na 2.5 acres. Eneo la heka mbili na nusu kila ng’ombe mmoja anapaswa kula kwenye eneo la heka mbili na nusu lakini kuna teknolojia wenzetu wachina wamegundua ya kupanda majani, kwenye 2.5 acres unaweza ukalisha ng’ombe 50 mpaka 70, Mheshimiwa Waziri wewe ni shahidi, pale Kongwa mmeanza, sasa kwa nini usi-disseminate? Kwa nini isiende kwa hao wafugaji? (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Geter, Mheshimiwa Mbunge ana dakika moja tu iliyobakia.
TAARIFA
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, sawa ninampa taarifa tu, ni mwenzangu katika kuongea lakini ninampa taarifa kwamba, mashamba ya wakulima pia yana mahitaji kwamba sisi tunahitaji chakula kwa maana ya kuishi na nyasi ni chakula kwa maana ya chakula cha ng’ombe, sasa tukilima mashamba yote nyasi maana yake watu hawataishi isipokuwa wachague maeneo mazuri kwenye maeneo yetu mazuri hayo. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Sasa wewe..
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, sipokei hiyo taarifa! Sina maana tuache kulima mazao ya chakula, ninasema kuna maeneo mnawapa elimu wafugaji wachache ambao wanadhani wanaweza kufanya hiyo biashara.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kunambi muda wako umekwisha.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshiiwa Naibu Spika, ninaomba nimalizie kwa kusema, dakika moja amechukua muda wangu, nakuomba!
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu wa Maliasili sasa wameacha kulinda majangili wamekuwa wachungaji wa ng’ombe, tutafika kweli? Tuwaache wafanye kazi yao, Mheshimiwa Waziri kazi ya mifugo ni ya kwako. (Makofi)