Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambayo ipo mezani. Nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya katika kusimamia maendeleo ya nchi yetu. Sekta zote tumekuwa tukiona anafanya kazi kubwa na hata kwenye Sekta hii ya Mifugo na Uvuvi tumeona kazi kubwa inafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili nichukue nafasi hii kumpongeza kaka yangu Mheshimiwa Alhaji Abdallah Ulega kwa kazi kubwa anayoifanya na wenzake Naibu Waziri ndugu yangu Mheshimiwa Alexander Mnyeti pamoja na Katibu Mkuu Professor Shemdoe na wataalamu wote kwa kazi kubwa wanayofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta hii ni Sekta muhimu katika uchumi wa nchi yetu lakini chakula kama ambavyo tumekuwa tukielezwa na leo wanasema ni siku ya protini ambayo ipo kwenye viwanja vya Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeambiwa takwimu hapa na tumesikiliza vizuri Hotuba ya Mheshimiwa Waziri, kwamba tunao ng’ombe wengi sana wapatao milioni 37.6 lakini pia tuna mbuzi pamoja na kondoo wa kutosha. Maana yake tukitumia vizuri rasilimali hii tunaweza kubadilisha kabisa uchumi wa nchi yetu na tutaongeza pato la Taifa kupitia kuchangia kwenye GDP, ni mipango tu ikiwekwa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimesema nampongeza Mheshimiwa Waziri. Tangu umeingia katika Wizara hii ukiwa Naibu Waziri, tuliona mchango wako lakini sasa ni Waziri kamili, nina amini kabisa tutatumia rasilimali hii vizuri, tutajipanga vizuri kulingana na mipango ambayo umetuambia.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumpongeze Mheshimiwa Rais, ametuongezea bajeti kutoka shilingi bilioni 169 mpaka sasa ni shilingi bilioni 460, ni zaidi ya 63% imeongezeka bajeti. Maana yake ni kwamba ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba yale ambayo ni matamanio ya Wizara hii kwenye utafiti, kuwekeza rasilimali watu na mipango mbalimbali, ikifanyiwa kazi vizuri itaongeza uchumi kwa kiasi kikubwa katika Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi. Kwa hiyo nilitaka tu nitoe mchango wangu kwenye maeneo machache ili niweze kuona namna ambavyo tutafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze kwenye lile suala la kuweka bandari ya Uvuvi pale Kilwa Masoko. Sisi tulifika kama Kamati, ni uwekezaji mkubwa sana zaidi ya shilingi bilioni 286 inaenda kuwekwa pale. Tutakuwa na uwezo wa kupaki meli tatu za mita 100 ambazo zitakuwa na uwezo wa kupakia Samaki na kuzipeleka kule kunakotakiwa. Maana yake ni kwamba tunaenda kuongeza uchumi mkubwa katika Sekta ya Uvuvi pia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nataka nieleze maeneo machache ambayo nadhani yaweze kuwa kama mchango wangu. Eneo la kwanza nataka niombe kwamba, tumesikia hapa migogoro mingi ya wakulima na wafugaji. Hii ni kwa sababu huenda hatujatenga maeneo halisi ya wafugaji. Ndiyo maana leo wafugaji wanalalamika nchi nzima katika maeneo mbalimbali. Niombe sana Mheshimiwa Waziri kaa na Wizara zingine zinazohusiana na Wizara hii ziweze kusaidia wakulima na wafugaji waondokane na migogoro hii. Mfugaji wa nchi hii asionekane ni yatima kwa sababu kuwa na mifugo mingi kama walivyosikia wengine siyo laana ni sehemu ya rasilimali kila mmoja anajivunia kile alichonacho.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni kuomba migogoro hii iweze kutatuliwa kwa amani ili wananchi wote waweze kufurahia mifugo yao. Kwenye eneo la wataalamu Mheshimiwa Waziri, unaweza ukawa na mipango mizuri kwenye level ya Wizara lakini kule chini kwenye halmashauri hatuna wataalamu wa mifugo, hatuna wataalamu wa uvuvi. Leo hii tunalia kule kwa sababu watendaji wa kata na wa vijiji ndiyo wanafanya kazi kwa niaba ya Wizara yako, niombe sana tuongeze wataalamu ili waende wakafanye transformation ya ile mifugo katika maeneo yetu. Kwa hiyo nilitaka niombe sana tuongeze wataalamu katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ujenzi wa majosho, kwenye eneo hili Mheshimiwa Waziri una deni na mimi. Nilikuomba majosho manne, umenipatia josho moja katika Kata ya Ntuntu. Kuna josho muhimu lipo katika Kata ya Siuyu, lile josho linatakiwa liondolewe katika maeneo ya Kanisa. Niombe sana lile josho unijengee ili wananchi wale waendelee kupata huduma za kuogesha mifugo yao na kuweza kusaidia mifugo iendelee kunenepa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, niombe sana mifugo katika maeneo ya Isuna, Mang’onyi...
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Mtaturu...
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Naibu Spika, Unyahati pamoja na Siuyu nao wanahitaji majosho...
NAIBU SPIKA: Ahsante sana, Mheshimiwa Mtaturu...
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Naibu Spika, ili waweze kuboresha mifugo yao. Ahsante sana naunga mkono hoja, nakutakia kila la heri Mheshimiwa Waziri, ahsante sana. (Makofi)