Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuzungumza kidogo kwenye hii hoja ya Waziri wa Uvuvi na Mifugo. Bahati nzuri nimesikiliza vizuri bajeti yake na nimeisoma. Kusema ukweli imekaa vizuri. Naendelea tu kuwapongeza na kuwapa moyo kwamba waendelee na kazi yao pasipokuwa na shaka yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie tu kwenye maeneo mawili; eneo la kwanza ni eneo la uvuvi. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuweka fedha nyingi. Wameweza kutusaidia kuongeza ajira kwa kuleta vizimba hasa katika Ziwa Victoria na hususan katika Mkoa wangu wa Mara na Mji wangu wa Musoma vilevile wameweza kufaidika na msaada huo. Niwaombe tu, kwa sababu wameahidi wataendelea kutoa vizimba zaidi, nimwambie tu Mheshimiwa Waziri, watu wangu wapo tayari na vikundi vyao vipo tayari na wanasubiri kwa hamu sana ili waendelee kupata ajira kutokana na hii fursa ambayo Serikali ya Mama Dkt. Samia imeamua kuitoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu tu mambo mawili yanapaswa yafanyike au kuna changamoto mbili ambazo zinatusumbua. Kwanza kwenye upande wa uvuvi kwa kutumia vizimba. Shida kubwa ambayo tunaipata ya kwanza ni tatizo la chakula. Tatizo la chakula kwa maana kuwa chakula ambacho kinatolewa au kinachouzwa sio chakula sahihi cha kukuza wale samaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kwa utaratibu kile chakula samaki wanapaswa wale ndani ya miezi sita na wao wameshakuwa na umri wa kuuzwa ambao sio chini ya gramu 500, lakini kwa bahati mbaya sana kwa sababu chakula kinachouzwa sio sahihi unakuta kila mara samaki wanafugwa mpaka miezi 10 lakini wanaishia gramu 300. Kwa hiyo, wanasababisha gharama ziwe kubwa kwa mfugaji na mwisho wanaona kama sio biashara ya kufanya, lakini tukipata chakula sahihi chenye content sahihi ni rahisi sana watu wengi wakaingia kwenye biashara hiyo na biashara hiyo ikaendelea kuwapatia kipato.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ana kazi ya ziada ya kuhakikisha kwamba wataalam wake kwanza wanakagua vile vyakula vinavyouzwa kulingana na zile content ambazo zimeandikwa na kuona kama ni sahihi. Vilevile kututafutia formula halisi itakayoweza kutusaidia kuhakikisha kwamba tunapata chakula ambacho ni bora na chakula cha kuwasaidia watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo wakati mwingine ufugaji ule wa njia ya vizimba maana yake ni kwamba ikitokea aina yoyote ya pollution kwenye maji kwa maana ya sumu ya aina yoyote ile tafsiri yake ni kwamba wale samaki wote ambao umeweka kwenye ile cage moja either ni 40,000 au 30,000, matokeo yake wale samaki wanakufa. Hata mwaka jana nakumbuka kule kwetu watu wengi samaki wao walikufa na ilisemekana kwamba kuna sumu ilimwagwa kutoka huko juu, lakini hata wale wavuvi haramu nao imekuwa ni tatizo kubwa maana kila ikitokea tu kwamba wamevua kwa uvuvi haramu inatuathiri na inasababisha hata wale samaki ambao wanafugwa kwa bahati mbaya wanakufa na hii inakuwa ni hasara kubwa kwa yule ambaye ni mtegaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wa bure hapo na hili Mheshimiwa Waziri nakumbuka kwenye bajeti iliyopita aliahidi. Tulisema ili tuweze kudhibiti vizuri uvuvi haramu, lakini ili tuweze kuhakikisha kwamba uvuvi unakuwa mzuri tuhakikishe kwamba tunakuwa na mamlaka ya uvuvi ambayo hiyo mamlaka itatusaidia kuhakikisha hiyo shida ya uvuvi haramu inaisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kwa sababu muda wangu umekwisha, nampa Mheshimiwa Waziri hii nakala ya vile viwanda vya nyama, vimebaki viwanda viwili ndiyo vimeruhusiwa ambacho ni Kiwanda cha Bagamoyo na Kiwanda cha Mpakaniā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Manyinyi, mengine utaandika.

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, hilo nalo atalifanyia kazi. Nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)