Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mimi nina maeneo manne tu ya kuchangia, kama dakika moja moja tu Mungu akinijalia.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kwanza ni kwamba, ninamshukuru sana Waziri wa Mifugo, Ndugu yangu Mheshimiwa Ulega, pamoja na Naibu Waziri, Ndugu yangu Mheshimiwa Mnyeti. Hawa wote ni ndugu zangu wa karibu sana. Nawashukuru wamekuja Sengerema na wameona changamoto zilizopo Sengerema. Sasa nikiwakumbusha changamoto zilizopo Sengerema haitakuwa sawa kwa sababu, wanazijua. Sasa nitategemea leo hapa wamenipangiaje, kama Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Ndugu yangu Shemdoe naye ni miongoni mwa watu wanaoyajua matatizo ya Sengerema. Tuna Soko letu la Samaki la Nyampurukano, hili ni soko la samaki wabichi. Samaki wale wanatumika sana katika maeneo mengi, Kahama, Misungwi, Kwimba, Nzega, Shinyanga na Tabora wanategemea samaki kutoka Nyampurukano. Sasa soko hili, kitaalam, sijui wao wanaliona liko katika hali gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tuna soko ambalo limebeba uchumi wa Sengerema, Soko la Nyakaliro. Soko la Nyakaliro limekusanya zaidi ya visiwa 17 ambavyo vinaleta samaki pale. Hili soko limekuwa na mvutano kati yetu sisi na Kirumba. Soko la Kirumba, wenzetu wanakuwa na wasiwasi, hawa watu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwamba, wakitoa leseni kwa Soko la Nyakaliro ambako kuna uwekezaji mkubwa, Wizara imepeleka pale pesa zaidi ya shilingi milioni 700, tunashangaa kwa nini hawafungui hilo soko? Kwa hiyo, leo tunategemea majibu ya Mheshimiwa Waziri yaje hapa kwamba, tunafungua lini Soko la Samaki na Dagaa la Nyakaliro? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tuna Soko la pili la Dagaa la Kijiweni. Tumekwenda pale katika hili soko mara mbili na Mheshimiwa Ulega na hata Mheshimiwa Mnyeti amekwenda pale. Kuna ujenzi wa kimagumashi ambao uko pale unaendelea, lakini sitaki kusema sana hapa. Mheshimiwa Waziri anajua kwa sababu, huyo mkandarasi wanajua walikompata. Sasa sisi tunachotaka ni kazi yetu iishe na ule mradi pale ukamilike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna sehemu ya uanikaji wa samaki wadogo (dagaa). Tumeomba vifaa vya kuanikia wakadai kwamba, tayari kuna wawekezaji, tumepata wataalam kutoka Uganda ambao watakuja kutuwekea namna ya kuanika dagaa pale Chifufu. Wananchi wa Chifufu sasa hivi wako kwenye TV wanasubiri kuona mwalo wao wa dagaa utatengenezwa lini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tuna Mwalo wa Furu wa Bungonya, kote huko tumekwenda na Mheshimiwa Waziri. Sasa tunakuomba jambo hilo pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni, nataka kuzungumzia suala la mifugo. Sisi tuna Kituo kinaitwa Kishinda. Serikali ilijenga kituo kile kupitia Mheshimiwa Hayati Lowassa, wakati ule akiwa ni Waziri wa Mifugo. Kituo kile kilikuwa kinaletewa mitamba pamoja na madume ya mfano yanayokuja kukaa pale. Kwa sababu, yale madume yalikuwa na kilo 500 tulitegemea kwamba, ule mradi ungekuwa ni mradi mkubwa kwa kuwa, ulikuwa ni wa majaribio. Serikali imeutelekeza, watu wa Wizara ya Mifugo wameutelekeza. Sasa tunaomba maelekezo ya Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, tuna mabwawa, ameyatembelea haya malambo Ndugu yangu Mheshimiwa Ulega wakati alipokuwa Naibu Waziri leo amekuwa Waziri Alhamdulillah dua zetu. Katika watu wanaomwombea dua ni pamoja na mimi sijui anakuwaje? Sasa akanisahau mimi mpaka nikaingia kwenye matatizo jimboni kwa ajili ya haya malambo, mtani wangu inakuwaje ndugu yangu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni Mamlaka ya Uvuvi, hii Mamlaka ya Uvuvi kama Mheshimiwa Waziri kweli udugu wangu atakomea hapa na wewe kama hatakuja na majibu hii Mamlaka ya Uvuvi na Mifugo inaanza lini? Anaona wenzetu kule wamekuja na RUWASA, wamekuja na TARURA, leo wanakwenda vizuri, anafeli wapi? Nilimsikia Mheshimiwa Rais anamwita mwanangu Ulega, nikamsikia siku moja tena anamwita Mheshimiwa Mnyeti mwanangu, hawa wanakuwa ni watoto wa kambo kwa mama maana yake sielewi au wanamwogopa wakifika kule hawamwelezi kwamba sisi tunahitaji Mamlaka ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu Bunge leo liazimie kuhusiana na suala hili. Wavuvi wanakuwa wanapata matatizo makubwa. Tuna uvuvi kule unaitwa luwa luwa na hawa Wakongo sasa hivi wamevamia Ziwa Victoria. Tunahitaji waje waone hawa BMU wanakuja kuwapa mafunzo gani waapishwe wale viapo. Tutengeneze BMU yenye nguvu ambayo itafanya kazi na halmashauri pamoja na Serikali za Vijiji ili tukomeshe uvuvi haramu ili Ziwa hili la Victoria liwe ziwa la kunywa maji ya kunywa, kweli inawezekana na siyo limebeba uchumi?

Mheshimiwa Naibu Spika, wanavyoanza kuchokonoa leo wanaanza kufunga Kigoma, najua wanaelekea kufunga Ziwa Victoria. Sasa hapa itakuwa hatari kubwa Mheshimiwa Mnyeti ndugu yangu...

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana maana yake nitakwenda mbali zaidi. Mimi namwombea kwa Mungu na nasubiri majibu halali atakayonipa Waziri hapa leo Wanasengerema wanayasubiri. Ahsante sana. (Makofi)