Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii ya mifugo na mimi moja kwa moja niseme naunga mkono hoja kwa sababu sina shaka kabisa na utendaji kwa Mheshimiwa Waziri mahiri Mheshimiwa Ulega na Mheshimiwa Naibu wake lakini pamoja na watendaji wote wa Wizara hii angalau ndoto za wafugaji sasa nafikiri tunaenda kuzifikia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza kwa namna ya pekee Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuongeza bajeti ya mifugo bajeti iliyokuwepo mwaka jana ya shilingi bilioni 292.5 lakini sasa hivi ameenda kuridhia shilingi bilioni 460.33, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme tu pamoja na uwekezaji huu mkubwa unaofanyika katika mifugo bado hatujaweza kupata tija kabisa kwenye mapato ya ndani, kwenye fedha za kigeni lakini kwenye kaya za wafugaji wenyewe, kwa sababu ya aina hii ya ufugaji unaoendelea nchini kwetu ufugaji wa kuhama hama (pastoralist). Wafugaji wa Arusha, Manyara utawaona mpaka Kilindi, Morogoro, Chalinze mpaka huko kusini. Kwa nini? Kwa sababu wanahangaika kutafuta malisho na maji na kwa sababu hiyo ndiyo chanzo kikubwa kabisa ya migogoro kati ya wafugaji na wakulima, uharibifu wa mazingira na kuendelea kueneza magonjwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe kabisa kwamba Wizara ilishaanza kutambua maeneo ya malisho na nyanda za malisho kwenye mikoa kadhaa tulishapima hekta 3,189,000. Sasa niombe tu kwamba kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Matumizi Bora ya Ardhi wafugaji wangemilikishwa maeneo yao ya ufugaji ili kwamba kila mfugaji aweze kufuga kulingana na uwezo wa ardhi (grazing capacity). Hii itawafanya wafugaji waelewe kuvuna mifugo ili wabaki na mifugo yao michache wanayoweza kuifuga hii itasaidia sana na kupunguza kutembea tembea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mwarobaini ambayo Mheshimiwa Waziri amekuja nao wa kusambaza mbegu ya malisho nawapongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri. Sasa kuna Shamba la Ikunge kule Pwani ambalo kwa msimu uliopita imezalisha tani 127. Leo umewatangazia umma wa Watanzania na wafugaji kwamba mbegu hizo zitapatikana katika maduka yote ya mawakala, mbegu hizi bado ni kidogo wataanza kwenda kule kutafuta hizi mbegu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu kabisa Serikali iendelee kutenga fedha za kutosha katika Wizara hii, kuendelea kuzalisha mbegu za kutosha ziweze kupatikana kwa mawakala kama inavyouzwa mbegu za mahindi kwenye pakiti mbalimbali. Kwa vipando hizi cuttings kama majani ya tembo zipelekwe halmashauri na halmashauri watoe kwa wafugaji, wafugaji wanajua kupeana mbegu na mbegu hizi zitaenea.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mwingine ni kuhusu upungufu wa huduma za ugani. Ni kama tumewaacha wafugaji peke yao wanavyohangaika hasa kwenye kutibu mifugo, wanahangaika wanatumia uzoefu kitu ambacho ni hatari kabisa. Wanavyotumia uzoefu wanatumia dawa kali kwa dozi wanazojua wao na kwa isivyo bahati kabisa kama akiona mifugo haiponi, atachinja hiyo nyama ataleta buchani tutakula wote au kwa vyovyote vile atatibu na pengine maziwa yatakuja sokoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ku-promote vizimba kwenye uvuvi bado hatuna wataalamu wa kutosha kwenye uvuvi na hata hao wachache pengine hawawajibiki. Pamoja na miradi mingi ambayo Wizara inafanya na kuipeleka katika Serikali za Mitaa kama majosho na mengineyo bado inakosa usimamizi. Sasa naona tu suluhisho la huduma hizi za ugani ni kuanzisha hiyo mamlaka ambayo wenzangu wamekwisha kusema: Mamlaka ya Ufugaji na Mamlaka ya Uvuvi. Hizo zinaweza kuwa mwarobaini maana wataajiriwa para professional kote katika ngazi ya kijiji na katika ngazi ya kata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mwingine ni kuhusu utotoshaji wa mifugo, tumeweka uwekezaji mkubwa sana katika sekta hii ya mifugo kwa kweli inasikitisha kabisa tunavyoona mifugo mingi inatoroshwa nje ya nchi na Serikali inakosa mapato. Pamoja na kujenga minada kwenye mipaka kwa mfano mnada wa Horohoro umejengwa kwa shilingi milioni 563 lakini hebu tuone kule wanaotorosha ni Watanzania wenzetu kwa nini hatujajua changamoto, kwa nini wanatorosha hii mifugo na tunakosa mapato. Pengine kuna kila sababu ya Wizara kwenda kukaa na wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo kujua changamoto ni nini? Pengine kuna utitiri mwingi wa tozo na vitu vingine lakini kuimarisha mipaka huko kwenye minada ili tupunguze utoroshaji wa mifugo na Serikali yetu iweze kupata fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nasisitiza kuhusu zoezi la utambuzi wa mifugo ambapo safari hii Serikali itenge fedha za kutosha ili zoezi la utambuzi wa mifugo ifanyike na kufahamu mifugo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi na naunga mkono hoja. (Makofi)