Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema siku ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi watu wa Mtwara katika ule mgao wa zile boti za kisasa zimetufikia boti tano; tunaishukuru sana Serikali kwa hilo. Namwomba Mheshimiwa Waziri atume wataalam wake wakaangalie mchakato wa zile boti, kwani inaonekana kama zinasumbua vitu fulani havijakaa sawa sawa. Naomba tu hilo lifanyiwe kazi ili lile lengo ambalo limekusudiwa na Serikali basi liweze kutimia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia namuomba Mheshimiwa Waziri pale katika Manispaa yetu ya Mtwara Mikindani, waangalie kwa jicho la karibu pale ferry ambapo samaki wanauzwa, kununulia, kukaangwa, kutayarishwa na kila kitu. Tunaomba miundombinu ya pale ferry katika Manispaa ya Mtwara Mikindani paboreshwe. Kwa sababu wanawake wengi wanafanya biashara zao lakini mazingira yaliyopo pale siyo rafiki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye issue ya nishati bado mpaka leo kuni zinatumika pale kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, kwenye storage facilities (sehemu ya baridi ya kuhifadhia samaki) bado uwezo wake siyo mkubwa. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri wafanye kila linalowezekana ili kusudi sehemu ile iweze kuboreka.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna changamoto kubwa ya mbegu ya majongoo bahari. Mheshimiwa Waziri, mwaka jana nililisema na mwaka huu nalisema. Vijana, wanawake na watu wazima wamehamasika sana kufuga majongoo bahari kwa sababu soko lake ni la uhakika lakini upatikanaji wa mbegu bado unasuasua. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba walitilie mkazo suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo, Mheshimiwa Waziri tunasema mchango mdogo wa Sekta ya Uvuvi katika pato la Taifa. Sababu zinajulikana, ukisoma kwenye hiyo hiyo hotuba amesema uvuvi unachangia pato la Taifa kwa kiasi kidogo. Akasemaje? Kwa sababu kuna uwekezaji mdogo katika uvuvi wa Bahari Kuu na usindikaji wa mazao ya uvuvi kuna athiri mchango wa Sekta ya Uvuvi katika pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwenye mipango yake mingi imeeleza kuboresha uvuvi wa Bahari Kuu kwa kununua meli za uvuvi. Mara ya kwanza walisema watanunua meli nane. Zikaja wakasema watanunua tano, leo nazungumzia nne. Sasa nataka kujua, meli zinanunuliwa au hazinunuliwi? Yaani wanatuachaachaje sisi watu ambao tuko kwenye ukanda wa Bahari Kuu? Watueleze tu, from nane kwenda tano na sasa hivi tunaongelea nne. Wananunua au hawanunui? Waziri akija kuhitimisha hapo atueleze. Pia, naomba kama anaenda kununua, basi ya kwanza kabisa ipelekwe Mtwara kwa sababu kuna ukanda mrefu sana wa Bahari ya Hindi ili kusudi uvuvi utekelezeke kwa kiasi kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, boti za kisasa za doria. Sitaki kuamini na siamini, bahari yetu ina samaki wengi wakubwa. Tunachokosa sisi ni nyenzo za kuvulia hao samaki. Meli inunuliwe, maboya yanunuliwe lakini wanunue boti za doria za kisasa ili ziweze kufanya kazi ya kuchunga rasilimali ambayo ipo ili tuwezeshe Taifa letu kupata pato kubwa linalotokana na Sekta ya Uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, samaki hawajawahi kwisha baharini hata siku moja isipokuwa sisi tunashindwa kuwafikia kutokana na zana duni ambazo tunazitumia kwenda kuvulia. Kwa hiyo, bado nasisitiza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepata mshtuko kidogo. Bajeti ya maendeleo kutoka shilingi bilioni 194 mpaka shilingi bilioni 363 wakati iliyopita imetolewa mpaka sasa hivi hata 50% haijafika. Ongezeko hili kubwa kama litakwenda kutolewa, naona mabadiliko makubwa kwenye sekta hii. Kwa hiyo, ombi langu na hoja yangu ni kwamba, fedha hizi zilizotengwa zisiishie kwenye makaratasi. Ziishie kweli kutolewa zikatekeleze miradi ya maendeleo ambayo imekusudiwa kwa manufaa ya nchi yetu na manufaa ya wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache nakushukuru sana na namtakia heri kaka yangu Mheshimiwa Ulega. Waende wakayatekeleze haya yaliyopangwa na Serikali itoe pesa ili waweze kutekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)