Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa fursa hii. Baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu Kitabu chetu kitukufu cha Quran, kwenye Surat Dhuha Aya ya 11 inatuambia, “wa amma bi ni’mati Rabbika fahaddith.” Maana yake neema za Mola wetu tuzitangaze na neema zenyewe za Mwenyezi Mungu ndizo hizi ambazo sisi wanadamu tunazitenda na kuzifanya. Kwa hiyo, kabla sijajikita kwenye ushauri, naomba nitangulize kutoa pongezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kama wenzangu walivyotangulia, kwa utashi wake wa kisiasa. Pia, hajaishia tu kwenye utashi ila amekwenda kwenye vitendo. Kwanza, kwa kuongeza bajeti ya Wizara yetu na kwa ujumla kwa Wizara hizi zote ambazo zinasimamia sekta ya uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua umuhimu wa Sekta hizi. Kwanza kwa kuzalisha ajira kwenye nchi yetu lakini kwenye kuchangia kipato cha uchumi wetu na kuingiza fedha za kigeni katika nchi yetu. Hata hivyo, kikubwa sisi ni wawakilishi wa wananchi, kwenda kunyanyua maisha ya mmoja mmoja katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Mheshimiwa Waziri Ulega, hongera sana; kazi unaifanya na tunaiona. Leo hii tunaongelea ajira mpya kupitia BBT life ni ubunifu wako na unaendelea kuufanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jana tulikuwa pale Kongwa kwenye uzinduzi wa Kituo atamizi ambacho kinakwenda kunyanyua vijana wetu na kuwafundisha ufugaji wa kisasa wa mbuzi ili waweze kuuza ndani ya nchi na nje ya nchi. Hayo ndiyo mambo; tulikuwa tunataka Serikali kwenye sekta hizi za uzalishaji wawafikie wakulima, wafugaji na wavuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo wavuvi wanapewa boti na Serikali, leo wavuvi wanapewa nyenzo na Serikali. Kwa kweli kwa hilo acha tukupe maua yako, tukutie moyo kijana wetu uendelee kuchapa kazi. Sekta hii unaijua kiundani na kwa kweli uliyafanyia kazi mawazo mazuri ya Waheshimiwa Wabunge ambapo lengo wanataka kukusaidia ili na wewe uache alama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii kwa kweli Serikali kwenye bajeti tunapitisha fedha kwa ajili ya kuchanja mifugo yetu bure. Sisi hiki ndicho tulichokuwa tunakitaka. Kwa kweli nikutie moyo, chapakazi na usonge mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wameongelea kuhusu mamlaka. Namwomba Mheshimiwa Waziri aelewe na aielewe Kamati. Inawezekana mengine tukikaa kwenye Kamati tunamweleza yeye, tukiongea hapa Bungeni, tunaongea na Serikali yote. Kama Waziri amekwishafanya kwa nafasi yake, Serikali kwa sehemu nyingine inatakiwa iongezee nguvu, ndiyo maana tunaliongelea hapa kwa nia njema.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba, unaweza ukaanzisha duka kwa mtaji mzuri, biashara nzuri, ukawa pale una meneja, muuzaji na mhasibu mzuri katika eneo zuri. Ukikosa usimamizi ulio madhubuti, huwezi kutengeneza faida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Uvuvi ni Sekta muhimu katika uchumi. Leo tunaona makubwa yanayofanyika kwenye Wizara ya Kilimo lakini yatachukua muda kuyaona. Hata hivyo tujiulize, samaki ni rasilimali kama vile ilivyokuwa miti na misitu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, samaki hahitaji chanjo, kule kwenye bahari na ziwani samaki hahitaji chakula; anajilisha mwenyewe na anajitibu mwenyewe. Sisi tunakwenda na tukimvua na kumla anatusaidia afya. Unaweza kuwa na walakini kwenye nyama nyekundu lakini kwenye samaki madaktari kila siku wanatuambia tule. Kwa hiyo, tunapopaza sauti kwamba uvuvi tunataka uongezewe wigo kwenye kuusimamia tuna maana yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii anayesimamia mustakabali na maendeleo ya uvuvi na wavuvi hammiliki mvuvi. Mvuvi leo hii anamilikiwa na halmashauri. Afisa uvuvi yuko chini ya Mkurugenzi. Kipimo cha Mkurugenzi ni ukusanyaji wa mapato, kipimo cha Mkurugenzi ni yale mapato yake ameyatumia vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kumhoji Mkurugenzi kama amemnyanyua mvuvi au uvuvi ndani ya Halmashauri yake. Kwa hiyo, yeye anamchukulia mvuvi kama chanzo cha mapato. Ndiyo maana leo tunaona haya mambo tunaongea kwamba jamani tozo, sijui nini, kwa sababu yule anayemmiliki mvuvi hamuwazi yule mvuvi kukua.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana tumekazia kama Bunge kama Kamati ni lazima Mheshimiwa Waziri apate mamlaka ya uvuvi. Vilevile, mimi nimewaza mbali, mwanzoni huko nyuma Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ilikuwa Wizara moja lakini Bunge hili hili liliwaza na tumeona sasa hivi tuna Wizara ya Kilimo na tuna Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Naomba Hansard iweke hiyo kumbukumbu yangu. Iko siku tutahitaji hii Wizara ya Uvuvi ibaki yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisome nchi kumi Afrika ambazo zinaongoza kwa kuuza samaki na mazao yake duniani. Tunaanza na Morocco, Namibia, South Africa, Mauritius, Senegal, Tunisia, Seychelles, Mauritania, Madagascar, Uganda ni ya 10, Tanzania hatupo. Tujifananishe na Uganda tu ambayo ina Ziwa Victoria ambalo na sisi tunalo na sisi ndiyo tuna sehemu kubwa ya Ziwa Victoria. Sisi tuna Nyasa, Tanganyika na tuna Bahari, kwa nini hatumo humu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yote huyu hana usimamizi ambao ana umiliki kwa 100%. Mheshimiwa Mwijage ameongea mambo ya msingi namna gani tunaweza, leo hii pamoja na usimamizi mbovu lakini tayari Sekta ya Uvuvi inachangia GDP kwa asilimia 1.8. Je, tukiwa na mamlaka hii Wizara ikijitegemea tutafika wapi katika kuingiza kipato kwa nchi yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, suala la kuwa na mamlaka kamili ya kutunza hizi rasilimali zetu zinazotokana na uvuvi hilo jambo haliepukiki. Mheshimiwa Ulega, wewe ni mtaalamu wa Uchumi wa bluu. Umekaa pale na umesoma pale UDSM, Degree yako na Masters umesomea huko. Acha legacy kwenye hii Wizara, historia ya hii nchi ikukumbuke. Ili mwanzo uwe mzuri ni lazima Mheshimiwa Waziri asimamie hii mamlaka itimie na ianze kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunatunza misitu kwa nini tusitunze mazao haya ambayo yanakuja kutuongezea mapato na Tanzania itapaa tena kwa haraka? Wala hatuhitaji tena kusubiri sijui miezi miwili, ni sisi kuwawezesha wavuvi wetu wakawa na mazingira mazuri. Kwa sababu vitu vingine ni vya kujiuliza. Ukienda kwa wadau wote ambao wanazunguka Ziwa Victoria, wavuvi wanasema uvuvi haramu hawahutaki, ukienda Serikali inasema uvuvi haramu haiutaki, ukienda kwa sisi wawakilishi wa wananchi uvuvi haramu hatuutaki. Kila mtu anauchukia lakini bado unaendelea; shida iko wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ndiyo maana tunasisitiza usimamizi uwe thabiti. Hii yote ni katika kuanzishwa kwa mamlaka yetu hii ya uvuvi ambayo matokeo yake tutakuja kuyaona kwa haraka na sisi tuweze kuwa katika ramani kwa hizi rasilimali. Hizi neema ambazo Mwenyezi Mungu ametupatia sisi kama Nchi ya Tanzania ili tuweze kuleta maendeleo kwa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kusema kwamba naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)