Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilwa Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Nianze tu kwa kuwakumbusha kwamba, ambayo leo tunaiita Wilaya ya Kilwa ni dola ambayo ilikuwepo tangu karne moja. Wakati wa Dola ya Azania iliyokuwa inaundwa na miji mikubwa ya Rufiji na Kilwa kwa wakati huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kilwa hii ndiyo dola ambayo ilitengamaa karne ya 11 mpaka ya 15 ikiwa imeweza kujitengenezea fedha zake yenyewe. Mwanahistoria maarufu kutoka Morocco, Ibn Battuta baada ya kuzuru Kilwa anaandika akisema kwamba, “Nimetembea katika Pwani ya Afrika Mashariki na Kati, sijapata kuona Mji uliojengeka wenye dola kamili, wenye ustawi na ustaarabu kama Kilwa.” (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, historia inatupeleka katika kupanda na kushuka kwa masuala mbalimbali ikiwemo miji hii. Kilwa hii ilipanda ikashuka. Karne ya 18 Dola ya Kilwa ikashuka na kuanguka. Imeendelea kuwa hivyo na ndiyo Kilwa iliyosahaulika mpaka karne hii ya 20.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kwa wasomaji wa Biblia, turejee Kitabu cha Isaya ile Sura ya Sita mstari wa nane andiko linasema, “Kisha nikasikia sauti ya Bwana akisema nimtume nani? Naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu? Ndipo niliposema mimi hapa nitume mimi”. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muktadha wa Tanzania, wana Kilwa tulikuwa na kilio cha kusema ni nani atakayerudisha hadhi ya Kilwa kabla ya mwisho wa robo ya karne ya 21? Mama Samia anasema mimi hapa, mimi nitafanya kazi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuja kutujengea Bandari ya Uvuvi Kilwa yenye gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 266 ongeza shilingi bilioni 10; hakuna kama Mama Samia. Kwa wanaosoma Quran rejea Sura ya 27 Surat Naml, Aya ya 40. Nabii Suleiman alikuwa amepatwa na dharura. Dharura hii ndiyo dharura iliyotukuta wana Kilwa. “Audhu billahi minash shaitwan rajiim, Qalla-lladhi indahu ilimun mina-l-kitabi, anaa atiyka bihi qabla an yartadda ilayka twarfuka.” Dharura iliyomkuta Nabii Suleiman akatafuta wenye maarifa makubwa ya kufanya jambo la dharura la kuleta Kiti cha enzi cha Malikia Sheba wakati huo Bilqis. Akatokea mwenye elimu kubwa akasema mimi ndiye ambaye nitaleta kiti hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kupepesa jicho, wana Kilwa tunauliza; ni nani atakayerudisha hadhi ya Kilwa kabla robo ya kwanza ya karne ya 21 haijaisha? Mama Samia anasema, mimi hapa nitafanya kazi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Bandari hii ya Uvuvi ambayao itakuja kuchechemua viwanda vya kusindika samaki na mazao ya bahari pale Kilwa, inakuja kuchechemua miundombinu mingine ya kimataifa ikiwemo uwanja wa ndege wa kimataifa, masoko ya samaki pale Kilwa, vituo vya kuhifadhia samaki, karakana ya kujenga meli ya uvuvi ambayo Mheshimiwa Waziri ametaja katika hotuba yake. Hiyo ndiyo kazi ambayo sisi wana Kilwa tunakuja kuiona kuiona Kilwa ya karne ya 13. Hiyo ndiyo kazi ya Mama Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mama Samia amemaliza kazi yake kwetu sisi wana Kilwa, deni limebaki kwetu sisi. Vilevile, sisi wana Kilwa tunasema kabla maeneo mengine hawajamuheshimisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, sisi Wanakilwa mwaka 2025 tutakuwa wa kwanza halafu wengine watafuata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuna mashaka na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameiheshimisha Kilwa. Bandari ya uvuvi inakuja kuleta mabadiliko makubwa, mapinduzi makubwa ya kiuchumi, mapinduzi makubwa ya ustaarabu na mahusiano mengine ya kimataifa ikiwemo utalii. Sisi Wanakilwa tunachomuahidi Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mwaka 2025 tutaanza sisi halafu wengine watafuata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, naomba uniruhusu niwasilishe maombi ya wadau wa Sekta ya Uvuvi kwa Mheshimiwa Waziri. Nikianza na Kilwa Kivinje na Kilwa Somanga wanauliza, ile ahadi ambayo sisi Waheshimiwa Wabunge tulipitisha hapa ya kujengewa masoko Somanga na Kivinje inatekelezwa lini? Nitaomba Waziri anapokuja hapa Wanakilwa wapate majibu haya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima wa mwani nao wana hoja yao. Tunashukuru Waziri ametualikia hapa wadau wa mwani kutoka Kilwa na Mafia, tumewatembelea. Pia, wao wanasema kwamba wanaomba Serikali iwatafutie masoko. Kwa sababu hapa Tanzania upande wa Bara kumekuwa na mnunuzi mmoja tu ambaye ame-monopolize soko la ununuzi wa mwani. Wanaomba wapanuliwe wigo, wanunuzi wawe wengi zaidi ili kuwe na ushindani na waweze kupata bei nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho wanaloomba wadau wa mwani ni mashine za kuchakata. Mheshimwa Waziri akipata nafasi atembelee wanamwani hawa, wana ombi mahsusi la kuomba mashine za kuchakata mazao yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, na nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge watakapopata fursa, basi watembelee wajasiriamali hawa wanaochakata products mbalimbali za mwani hapa hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, kwenye hizi boti za uvuvi ambazo Mheshimiwa Waziri atanunua kutokana na bajeti ambayo si muda mrefu tutaipitisha, zaidi ya mia nne hamsini, tunaomba wale ambao walikosa mara ya kwanza wapewe kipaumbele katika awamu hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wa kipekee na mahsusi kabisa ni kwamba, katika vikundi ambavyo tumeviwezesha kuomba mikopo hii ya boti za uvuvi niombe kwa unyenyekevu mkubwa, pale Kilwa kuna Kikundi cha BMU Magengeni, afanye kama case study hivi, awakopeshe BMU Magengeni boti moja kati ya boti 450 anazokwenda kugawa katika huu mwambao wa Pwani halafu aone matokeo yake. Wao wanasema kwamba wataitumia boti hii kwa ajili ya uzalishaji, doria na kama dharura pale maafa au majanga yanapotokea baharini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)