Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Alexander Pastory Mnyeti

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Misungwi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia afya njema na hadi leo tuko hapa tunaendelea kulitumikia Taifa. Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi nikimsaidia kaka yangu Mheshimiwa Ulega. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii pia kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa ushirikiano mkubwa sana ambao amekuwa akinipatia. Yeye kwa kweli ni mwenyeji sana kwenye Wizara hii, amekaa zaidi ya miaka saba. Amekuwa msaada mkubwa sana katika hali ya kunielekeza na kunifundisha. Mimi sasa nina miezi tisa, bado naendelea kujifunza. Kwa kweli nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Abdallah Ulega kwa namna ya kipekee sana. Nataka niwahakikishie kwamba boss wangu ni mtu mwenye roho safi. Unajua wako mabosi wengine roho inakuwa mbaya sana, roho ngumu, mtu anakuwa na roho ngumu, boss unakuta amenuna kila siku, sababu inayomfanya anune haieleweki, ukimuuliza hasemi, haeleweki anataka nini, maisha ni magumu wizarani, lakini nataka niwahakikishie sisi Wizara ya Mifugo tuko pamoja na tunafanya kazi pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napokea maelekezo kutoka kwa boss wangu na kwa kweli nimejifunza vitu vingi sana kwa boss. Kulingana na umri wake, upendo alionao na roho safi aliyonayo naendelea kujifunza kusema ukweli na namhakikishia kwamba nitaendelea kumshauri vizuri, nitaendelea kujua kimo changu kinaishia wapi na maelekezo yake nitayafanya usiku na mchana ili kuhakikisha kwamba gurudumu hili tunalifikisha mahali linapotakiwa kufika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta hii ya Mifugo ni sekta mtambuka. Sote tunafahamu kwamba sekta hii inapaswa kuwa na mchango mkubwa sana katika ujenzi wa uchumi katika Taifa letu. Kazi ninayoifanya kwa sasa ni kupitia na kurejea documents mbalimbali ambazo zimetufanya tunase hapa tuliponasia. Ninachokifanya kwa sasa ni kumshauri Mheshimiwa Waziri, kwamba sasa kwa sababu tulinasia hapa tuanzie hapa ili kunusuru Sekta hii ya Mifugo na Uvuvi ili iwe na impact kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua mambo mengine mengi atakuja kuyasema Mheshimiwa Waziri, mimi nizungumzie mambo machache sana ambayo nimeyaona jioni hii ya leo niweze kuyazungumzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ni kuhusiana na migogoro inayoendelea baina ya watumiaji wa ardhi. Migogoro hii imekuwa ikiripotiwa kutoka maeneo mbalimbali. Watani zangu wa Mikoa ya Kusini wamekuwa wakilalamika sana juu ya wingi wa mifugo inayoingia katika maeneo yao. Mbaya zaidi mifugo hii imekuwa ikiingia mpaka inaharibu miundombinu ya kilimo kwenye mashamba ya wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme jambo moja hapa, kwa maelekezo ya Mheshimiwa Waziri; kwamba tushauri sana katika vijiji vyetu kuhakikisha kwamba tunapanga mipango ya matumizi bora ya ardhi; na mipango hiyo ya matumizi bora ya ardhi ni lazima iheshimiwe na kila mtu anayeishi katika eneo hilo. Mfugaji ajue kwamba shamba hili ni la mkulima na hivyo hapaswi kuingiza mifugo kwenye shamba hilo na mkulima naye ajue kwamba eneo hili ni la wafugaji na kwa hivyo hapaswi kwenda kulima katika maeneo hayo. Serikali za Vijiji, Serikali za Mitaa na kule halmashauri ndani ya zile wilaya wahakikishe kwamba wakishapanga hiyo mipango bora ya matumizi ya ardhi na sisi huku wizarani, Wizara ya Kilimo na sisi Wizara ya Mifugo na Uvuvi tupate documents za mipango hiyo. Mfugaji anapoingiza ng’ombe zake kwenye shamba la mtu tukienda kwenye ramani tukakuta amefanya kwa makusudi, sisi Wizara ya Mifugo na Uvuvi tuko tayari kushirikiana na wasimamizi wa sheria ili achukuliwe hatua za kisheria, tena za kumuumiza ili asirudie kosa hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kuwa wizara ya kulalamika kila siku, kwamba sisi tunakuwa sehemu ya kutetea wafugaji wasiofuata sheria. Wafugaji ni lazima wafuate sheria na sisi tutawapenda sana wafugaji. Hapa wako wengine wananisikia, kwamba ni lazima na ni lazima mfugaji yeyote awapo ndani ya nchi hii azingatie sheria, aheshimu mashamba ya watu na aheshimu makazi ya watu. Si kila sehemu tutapeleka ng’ombe, kila sehemu tutapeleka mbuzi ama kila sehemu tutapeleka kondoo, haiwezekeni. Pamoja na kwamba mimi na Mheshimiwa Waziri ni mawaziri wa ng’ombe, ni mawaziri wa kondoo na ni Mawaziri wa mbuzi, lakini hatuko tayari kuwa na ng’ombe wasiofuata sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikasema hili nilisisitize na namwona Mheshimiwa Mbunge wa Ngorongoro ananiangalia vizuri, nadhani amenielewa vizuri; kwamba ni lazima wafugaji wafuate sheria. Tukikaa bila sheria iko siku tutakutana na ng’ombe wameingia Bungeni hapa. Hili nalisisitiza kwa sababu limekuwa likilalamikiwa na limelalamikiwa na Waheshimiwa Wabunge wengi sana. Tunapokea simu nyingi sana, Wakuu wa Wilaya wanapiga simu nyingi sana wakielezea habari ya hawa ng’ombe, kila kitu ng’ombe, kila kona ng’ombe. Ni kweli tunakubali kwamba sisi ni mawaziri wa ng’ombe lakini ng’ombe wanaofuata sheria. Haufuati sheria haki ya Mungu lazima tukubaliane kwamba sheria inakuhusu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili nimelisema sana kwa sababu limekuwa likipigiwa kelele sana na ni lazima kila mtu afuate sheria katika mazingira hayo. Kwa hiyo tunaendelea kusisitiza, Serikali za Vijiji na Serikali za Halmashauri za Wilaya zote zinapaswa kuhakikisha kwamba maeneo yote yenye wafugaji wanapanga mpango bora wa matumizi ili kuepusha hii migogoro ambayo huingiliana katika maeneo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni kuhusiana na vizimba. Imesemwa hapa na Waheshimiwa Wabunge kwamba vizimba kule Ziwa Tanganyika ni vichache, ni kweli, tumepeleka vizimba 29, lakini vizimba hivi vimekwenda kulingana na maombi tuliyoyapokea. Vizimba vipo vya kutosha na kwa hiyo tupo tayari kuendelea kupokea maombi. Tumepokea maombi mengine ya Ziwa Nyasa, Ziwa Rukwa na maeneo mengine. Mheshimiwa Rais ametoa vizimba vya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa maombi ya awali tuliyoyapokea ndiyo hayo 29, maombi mengine tunaendelea kupokea. Jinsi tunavyoendelea kupokea maombi ndivyo tutakavyowaletea vizimba. Nataka niwahakikishie kwamba Mheshimiwa Waziri ametoa maelekezo pia, kwamba vizimba hivyo vitakuja kadri ya maombi yanavyokuja wizarani na sisi tuko tayari kuendelea kuleta vizimba mpaka wavuvi wa Ziwa Tanganyika watakapotosheka wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika maombi hayo ni lazima kuna utaratibu kwa sababu hii ni mikopo. Huwezi kufika tu mahali ukaanza kugawa mikopo kama njugu mawe, kwamba sasa sandakalawe, chukua, lazima kuwe na utaratibu wa maombi ambayo mtu anaandika. Lazima atupe ka-concept kake, kwamba una concept gani katika hili baada ya kuwa tumeshampa elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ni lazima mikopo hii iende kwa utaratibu na ni lazima tufuate utaratibu kwa sababu inakopeshwa na benki. Pamoja na kwamba anapitia kwa fedha za Serikali kutoka wizarani kwetu, lakini kuna utaratibu ambao umewekwa ili kumjua yule anayekwenda kukopeshwa ni nani, anafanyia wapi na kwa faida gani na atapata faida gani. Hii itasaidia sana kumfuatilia ili aweze kupata tija katika shughuli hii anayoifanya. Kwa hiyo naendelea kuwasisitiza wavuvi wale wote ambao wana hamu ya kujua zaidi kuhusu vizimba hivi kwamba Wizara ya Mifugo na Uvuvi iko tayari kuendelea kutoa vizimba hivi na iko tayari kuendelea kuwakopesha boti katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusiana na elimu. Hii pia imesemwa sana. Ni ukweli kwamba elimu haina mwisho, ni kweli; na katika hili la vizimba tumekwishatoa elimu kwa kiwango kikubwa sana na kwa kuwa elimu haina mwisho, basi tutaendelea kutoa elimu hii kwa kiwango kingine kikubwa zaidi. Kwa kweli tumejitahidi sana na watalaam wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wamekuwa wakienda mpaka vijijini kabisa kule ili kuwaelimisha wavuvi wetu juu ya namna gani vizimba vinatakiwa kuwa na juu ya namna gani boti hizi zinatakiwa kuwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, amesema Mheshimiwa Anjelina Mabula pale, kwamba boti zingine ambazo zimetolewa horsepower yake ni kubwa. Wao wenyewe wavuvi ndio waliochagua, kwa sababu sisi hatuwezi kumkopesha mtu, lazima tukubaliane, kwamba unataka horsepower ngapi nataka horsepower kumi, nataka horsepower 20. Wao wenyewe kulingana na uzoefu wa lile ziwa lenyewe ndio wanachangua wanataka horsepower ngapi ili isukume mtumbwi wa mita ngapi. Kwa hiyo kama kuna changamoto yoyote pia ya mtu mmoja mmoja aliyekopa boti hizo tuko tayari kukaa chini na kurekebisha tuone njia nzuri zaidi ya kumsaidia huyo mvuvi ili aweze kupiga hatua zaidi. Tunaendelea kupokea maombi ya namna hiyo katika picha hiyo katika mazingira ya maziwa yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, kwamba tunaendelea kutoa elimu na wataalam wetu wataendelea kutoa elimu na hata sasa tunapozungumza wengine wapo katika vijiji vyetu huko wanaendelea kutoa elimu. Waheshimiwa Wabunge tumejitahidi sana kukutana nao na wenyewe tukawapa elimu. Nina uhakika Waheshimiwa Wabunge wanaotoka katika Ziwa Tanganyika kama ni diploma au certificate ya uvuvi sasa tayari wanayo kwa sababu tumekutana nao mara kwa mara, tukawafundisha na tukawaelimisha njia nzuri ya kufuga samaki kwa njia ya vizimba na kwa kutumia hizi boti. Kwa kweli kama ni cheti tayari wanacho na sisi pale Wizarani tuna profesa wa uvuvi, Profesa Ulega, kwa kweli kama alivyosema Mheshimiwa Dkt. Chaya pale, kwamba kama ni kubobea kwenye suala la uvuvi Mheshimiwa Ulega amebobea, huna chenga ya kumpiga, amebobea sana. Digrii ya kwanza ni ya uvuvi na digrii ya pili ni ya uvuvi. Pale wizarani tuna maprofesa na wao wakileta ile elimu na wenyewe wameshajichanganya, sasa ni Profesa Ulega; tunaendelea vizuri kwa kweli kwa taaluma hiyo hiyo kubadilishana mawazo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu linahusu usimamizi wa miundombinu ya mifugo. Wizara imekuwa ikijenga majosho na malambo. Wizara inapomaliza kujenga majosho na malambo inayakabidhi kwenye halmashauri husika; kama ni halmashauri ya kijiji ama ni halmashauri ya wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, uzoefu unaonyesha kwamba tunapokuwa tumemaliza kujenga majosho na malambo tunapowakabidhi wenzetu na wenyewe wanayatelekeza. Majosho yanamaliza miezi mitatu yakishaharibika hata ile service ya hayo majosho hakuna anayehangaika nayo. Malambo yakijaa kidogo tu anayetakiwa kwenda kutoa hata zile tope hayupo; halmashauri wameyatelekeza Serikali za Vijiji wameyatelekeza, kila mtu ameyatelekeza. Kwa hiyo tukasema kwamba hapa lazima tuwe na chombo kitakachosimamia miundombinu hii ili kunusuru miundombinu hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta service yake pengine hata ni laki moja au shilingi 50,000, lakini hakuna anayehangaika nayo. Hii ni kwa sababu hakuna usimamizi madhubuti. Sisi tunapojenga tunakabidhi kule ili waweze kusimamia, lakini hakuna anayesimamia. Ndiyo maana tukaja na mpango; kwamba Bunge likisharuhusu habari hii lazima sasa tuwe na chombo kinachosimamia miundombinu hii ili kiweze kuratibu miundombinu hii na hivyo iweze kuleta tija kwa wafugaji wetu walio katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ni kuhusiana na ufungaji wa ziwa. Pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri atakuja kulisemea vizuri zaidi, lakini na mimi nigusie kidogo. Kwa wanaotoka maeneo ya Kanda ya Ziwa, wanaotoka maeneo ya Ziwa Tanganyika na maeneo mengine ya maziwa kama Nyasa na Rukwa na maeneo mengine; ukweli ni kwamba samaki wamekwisha ziwani, huo ndio ukweli. Hata hilo Ziwa Victoria. Leo samaki unayemnunua Victoria ana bei ghali kuliko samaki unayemnunua Dar es Salaam; kwa nini? Kwa sababu Dar es Salaam tayari wana mabwawa, wanafuga kwa njia ya mabwawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Victoria kule Mwanza maeneo yote anayoyasema mzee wangu Mheshimiwa Tabasamu ukiuliza bei ya samaki si ile bei ambayo sisi tumekua tukiiona na ukubwa wa samaki wanaopatikana katika maeneo hayo ni samaki wadogo, lakini ni bei ya juu. Kwa nini? Kwa sababu samaki wamepungua ziwani. Ziko sababu nyingi za samaki kupungua ziwani ambazo nikianza kuzielezea hapa nitachukua muda mwingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa faida ya muda, niombe sana Wanatanganyika wote waelewe kwamba pamoja na kwamba huu ni mkataba wa kimataifa, lakini samaki wamekwisha na tunakwenda kwa lengo jema sana la kuhakikisha kwamba tunanusuru samaki hawa. Kuna utafiti umefanyika, hatufungi ziwa kiholela tu, kwamba tumeamka tumekurupuka tumefunga ziwa, hapana, utafiti umefanyika na imeonekana kabisa kwamba hapa bila kufunga ziwa tunaendelea kupoteza mazalia madogomadogo ambayo baadaye yangekuja kuleta tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Kigoma na mikoa mingine ambao wamelielewa zoezi hili. Tunakwenda kulifunga kuanzia tarehe 15 Mei mpaka tarehe 25 Agosti. Yangekuwa ni matakwa yangu lile ziwa ilipaswa lifungwe hata mwaka mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukifanya utafiti nchi zote zenye maziwa kama haya huwa zinafunga na kuna nchi huwa zinafunga mpaka miaka kumi. Baada ya hapo mazao yanayopatikana kwenye kufunga huko kama ni samaki huwa ni kuzoa kwa mikono. Fanya utafiti, nenda China, ambako wao wanafunga mpaka miaka kumi; lakini baada ya hiyo miaka kumi wanakuja kuvua kwa mikono, samaki ni wengi mpaka sebuleni, wamejaa, samaki ni wengi. Yaani nataka nikwambie kwamba sisi tumechelewa. Ziwa Tanganyika hili lilipaswa lifungwe kuanzia miaka mitatu minne na kuendelea ili kuwe na tija kwa wafanyabiashara wetu na walaji wa samaki wanaoishi katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ni kuhusu Mamlaka ya Uvuvi. Hii nayo imesemwa sana na Mheshimiwa Waziri atakuja kulisemea zaidi na kwa kweli Waheshimiwa Wabunge wengi wameonyesha kuunga mkono jambo hili. Ni jambo lenye tija na ni jambo la maana sana kwa sababu ndilo linalokwenda kuwa mwarobaini wa wavuvi haramu na uvuvi usioeleweka katika maeneo yetu ya ziwa. Kwa hiyo niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge, tunawashukuru sana kwa jinsi ambavyo wanaendelea kutusapoti katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)