Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Nashon William Bidyanguze

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Ujenzi, ambayo ni Wizara kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Bashungwa, kwa kazi nzuri anayoendelea kufanya kwenye Wizara hii, lakini pia akishirikiana na Naibu Waziri. Pia, nimpongeze Katibu Mkuu wa Wizara pamoja na timu yote kwa kazi wanayoendelea kuifanya na tukijua kabisa barabara ni sawa na mishipa ya damu katika mwili wa binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Rais, kwa kazi nzuri anayoendelea kufanya kupeleka fedha kwenye Wizara hii ambayo kwa kweli tumepata shida sana kwa mwaka huu ambapo tulipata majanga mengi ya kuharibikiwa kwa barabara nyingi pamoja na madaraja. Mama ameendelea kupeleka fedha kwa ajili kuokoa na kuwezesha wananchi waweze kupita katika maeneo hayo ambayo yameharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwalike Mheshimiwa Waziri aje Kigoma. Tunayo Barabara ya Mpeta – Uvinza, hii barabara ndiyo kipande ambacho kimebaki kwa Mkoa wa Kigoma kuunganishwa na mikoa mingine hasa Mkoa wa Tabora. Ndiyo kipande ambacho kimebaki na kina kilometa 51.5. Mheshimiwa Waziri kipande hiki kiliwekewa fedha na mkandarasi yupo na anaendelea kufanya kazi na kwa kweli ana muda mrefu sana na wananchi mpaka wamefika mahali wamechoka sasa ninaomba uje uone kazi inayoendelea kufanywa. Naona kidogo kwa sasa ameanza kuweka lami lakini alikuwa amekwama kabisa hakuna kinachoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ukija utuambie Wabunge wa Mkoa wa Kigoma na sisi tushiriki kwenye ziara yako ili tuweze kuona namna ambavyo tutawasaidia wananchi kufungua hicho kipande ili tuondokane sasa na vumbi ukitoka Dar es Salaam, ukitoka Dodoma pita Tabora unafika Kigoma kwa kiwango cha lami lakini hicho kipande kwa kweli kinasumbua sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Mkoa wa Kigoma ipo barabara ambayo inaitwa Simbo – Kalya ambayo ipo Uvinza. Hii barabara ni kweli inakwenda Kalya, lakini ukweli ni kwamba hii barabara kuna kipande kule mbele ambacho ni cha TARURA ambacho kinaunganisha kwenye Mkoa wa Katavi na namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri niliwahi kumwomba aje aione hiyo Barabara. Hii barabara aliipita na akavuka kwenda mkoa mwingine. Nilikuwa napenda Mheshimiwa Waziri hii barabara pia ifunguliwe, isiitwe tu Simbo – Kalya hapana. Katika Mkoa wa Kigoma tuna barabara tatu ambazo zinatoka kwenye mikoa mingine kuingia Mkoa wa Kigoma, lakini hiyo ni ya nne. Tunapoendelea kuwa na barabara nyingi za kutoka ndani ya mkoa kwenda mikoa mingine ni faida pale ambapo barabara moja inaweza ika-broke (ikavunjika) maana yake hapo sasa tunatumia njia nyingine mbadala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii huwa ina shida sana hasa kwenye mwinuko. Nashukuru Naibu Waziri alipokuja alitoa maelekezo ya kuwekewa zege katika baadhi ya maeneo ya miinuko yaani mwananchi anashuka Basi la Saratoga na vijana wale wa Saratoga kwa kweli wamejitolea sana kuhakikisha kwamba wanahudumia eneo lile ambalo lina watu wengi. Eneo lile lina watu wengi karibuni 200,000 kwa sababu wapiga kura wangu ni karibu 450,000. Kule ndiyo kuna upande wa watu karibu 200,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wale vijana mpaka wanafika mahali wanajaribu kutengeza barabara wenyewe katika maeneo korofi. Sasa naomba katika maeneo haya korofi yawekewe zege, lakini barabara hiyo kwa sasa imefungwa kutokana na kwamba kivuko hakifanyi kazi kwamba maji yamejaa sana pale Ilagala. Mheshimiwa nikuombe, kwa kuwa tayari upembuzi yakinifu wa daraja lile umekamikika basi naomba utamke Serikali ina mpango gani katika kujenga daraja hilo? Kwa sababu wewe fikiria kwamba barabara ile sasa imekwama, imekwama kwa sababu kivuko hakifanyi kazi kutokana na maji kuwa mengi, upembuzi yakinifu umeshakamilika kwenye Daraja la Mto Malagarasi Chini, sasa mpango wa Serikali ni upi katika kuhakikisha kwamba hilo Daraja sasa linakwenda kujengwa? Nitapenda Mheshimiwa Waziri ukija kuhitimisha uzungumze chochote na utakapokuwa unakuja Mkoa wa Kigoma naomba nikupeleke hapo Ilagala uweze kuona hiyo adha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimeenda juzi Jumapili iliyopita ile kwa kweli wananchi wanasikitika sana kuona kwamba usafiri sasa katika barabara ile haupo watu wamesimama, maboti yalishaoza na meli hazifanyi kazi. Kwa hiyo watu 200,000 wamekaa hawatembei, wamesimama hakuna kinachofanyika. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri, kwa hilo niwe nimeliwekea msisitizo mkubwa, lakini nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa jinsi anavyoendelea kutuletea fedha nyingi katika Jimbo la Kigoma Kusini kwa maana ya Wilaya ya Uvinza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli napongeza sana kwa juhudi ambazo zinaendelea kwenye eneo la afya na elimu. Kwa kweli kuna haja ya hiyo barabara, kwa maana ikitengenezwa tukiweka daraja naomba nikuhakikishie kwamba kwa kweli itakuwa imeenda vizuri na tutakuwa tumewashika vizuri sana hawa wananchi kwa maana ya kwamba tumewashika kwenye eneo ambalo kwa kweli wanalihitaji. Ukienda pale Ilagala na wewe utakuwa shahidi yangu siku nitakayokupeleka watakwambia kilio chao ni daraja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, basi naomba niunge mkono hoja, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)