Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Antipas Zeno Mgungusi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi, mimi nina mambo mawili tu. Jambo la kwanza changamoto yetu ya Barabara ya Malinyi na pili ni suala la kuunganisha Wilaya ya Malinyi na Jimbo la Mlimba kwa Kivuko cha Kikove kwa maana ya kutumia pantoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuendelea na mengine yote nitoe shukurani kwa Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla kuweza kuhangika kufanya recovery ya mafuriko. Barabara nyingi nchini zimeathirika tunafahamu, ikiwemo Malinyi tumeathirika sana. Niseme tu, kufikia leo jioni barabara kubwa ya TANROADS kutoka Njiapanda au niseme Malinyi – Ifakara – Malinyi Mjini itapitika kwa maana ya hali ya udharura wakandarasi wapo pale wanarudisha hali kwa matengenezo ya muda mfupi wakati tunasubiri bajeti kubwa ya madaraja na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kipande kilichobaki kutoka Njiapanda – Ngoheranga kule Kilosa kwa Mpepo njia ya Songea nacho wakitoka hapa Malinyi Mjini (Madumba) wataelekea kule nadhani ndani ya siku tano au sita kazi itaanza na baadaye kutakuwa salama. Kwa hiyo niwaambie tu Wana-Malinyi wenzangu waungane nami kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa ajili ya jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri nimekuwa nawasiliana naye mara nyingi wakati wote kipindi cha mafuriko yeye na Naibu Waziri, Mheshimiwa Kasekenya amefika Malinyi zaidi ya mara tatu. Katibu Mkuu naye Mhandisi Aisha nimekuwa nawasiliana naye na kumsumbua mara nyingi ingawaje hajaweza kuja lakini amekuwa akitoa maelekezo mara kadhaa na Engineer wetu Meneja wa Mkoa Bwana Kiyamba na timu yake wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana. Kwa hiyo kiukweli kama Wana-Malinyi tunafarijika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali kuhusu changamoto yetu ya Malinyi nilikuwa nazungumza kipande cha kutoka Ifakara – Malinyi tunakuwa tunateseka masika wote mnafahamu na nimekuwa nikisema mara kadhaa, hili ni jambo la kwanza. Kwa hiyo naamini kuna kitu kitafanyika, lakini hata ukiacha hivyo ule mpango mkubwa wa barabara yetu ya kutoka Dar es Salaam – Mikumi – Ifakara – Malinyi – Kilosa kwa Mpepo – Namtumbo ipo kwenye mtindo wa EPC+F kwa maana ya ujenzi wa mtindo wa mkopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka mitatu iliyopita niliomba walau; najua Serikali inaweza ikabanwa uhitaji ni mkubwa nchi nzima. Niliomba walau kilometa 50 tujenge barabara hiyo ya Malinyi kwa vipande vipande pengine ndani ya miaka mitatu au minne tungeweza kuwa tumemaliza, lakini iliwapendeza Wizara ya Fedha na Ujenzi kuihamishia barabara hiyo kwenye huu Mfumo wa EPC+F kwa maana ya kujengwa yote kutoka Ifakara – Namtumbo – Ruvuma - Lumecha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nadhani mnafahamu mwaka jana tulisaini mkataba mwezi wa sita na tunasubiria wakandarasi wafike site. Sijajua uvunguni kuna nini hasa lakini shida ya wazi inaonekana kama mkandarasi anatudai down payment. Basi niombe Wizara kama ni hilo, basi alipwe tuweze kufanya hilo jambo liweze kwenda. Sisi barabara yetu hiyo ambayo tunaizungumzia mara nyingi ina umuhimu mkubwa sana. Kwanza kutuokoa Wana-Malinyi na changamoto ya masika. Sisi nadhani ndiyo watu pekee wakati wa masika hatuwezi kufika Halmashauri ya Mji, hatuwezi kufika mjini. Ndiyo hali ilivyo ya Malinyi na mara kadhaa nimekuwa hapa nikizungumzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia umuhimu wa pili wa barabara hii mnafahamu Serikali na Chama ni mpango wetu kuunganisha barabara za mikoa na mikoa kwa kiwango cha lami nchi nzima, lakini sisi bado. Kwa hiyo maeneo ya Morogoro na Ruvuma hatujaunganika, hii ndiyo barabara pekee na tumeisemea mara kadhaa najua Serikali mnafahamu ndiyo maana mnaiweka kwenye mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa wafanyabiashara na wananchi wa kawaida hasa kwa watani zangu Wangoni kule Ruvuma nao wanataka kupita Malinyi wafike kwao kiurahisi. Leo kwenda Ruvuma kwa maana ya Songea kupitia Masai kutoka Dar es Salaam kilometa karibia 1800. Kutoka Dar es Salaam kupitia Njombe kwenda Songea kilometa 950 lakini kutoka Dar es Salaam kwenda Songea kupitia Malinyi kilometa 785. Kwa hiyo unaweza kuona barabara hiyo ni fupi sana sana. Zaidi ya kilometa 200 zinaenda kuokolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Watu wa Malinyi uchumi utakuwa umechagizwa kwa kiwango kikubwa lakini hata ndugu zetu wale wa Ruvuma nao watakwenda kunufaika. Sisi ni wazalishaji wakubwa wa mpunga mnafahamu Bonde la Kilombero lote. Tunafahamu barabara yetu ya pale Ifakara, kupita Mlimba kwenda Njombe inaendelea na yenyewe tuombe tu Serikali wa-speed up na baadaye tukimaliza Malinyi kutoka pale Ifakara kupitia Mahenge kwenda Liwale nazo zote tunazihitaji ili kulifungua Bonde la Kilombero.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tuna mpunga mwingi tunazalisha kabla ya mafuriko lakini bei zake mnafahamu ya mazao, bei zipo chini sana kutokana na kwamba hatuna alternative roads. Malinyi hatuwezi kufika, hatuna sehemu ya kupitisha watu kwa meli wala kwa treni, barabara pekee ndiyo hii. Kwa hiyo naomba nitoe changamoto Serikalini, Mheshimiwa Waziri mlichukuwe Watu wa Malinyi tuweze kusaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ilikuwa ni ahadi yangu mimi kama mgombea Ubunge wa CCM na CCM yangu kwenye uchaguzi wa 2020. Tuliwaahidi Wana-Malinyi na Wana-Mlimba tutaunganisha Mlimba na Malinyi kupitia Kivuko cha Kikove kwa maana tutaweka pantoni pale kivukoni jambo liweze kwenda. TEMESA wameanza kujenga hilo eneo lakini bahati mbaya mpaka sasa kipo 50% tu na mradi unasua sua na mafuriko sasa hivi yameenda kuharibu zaidi mambo hayaendelei, lakini hata kabla ya hapo kulikuwa na uzembe wa mkandarasi sijui kama Serikali pengine hamkuwa mnamlipa lakini mwaka wa tatu mradi ambao ulipaswa utumie miezi sita bado haujaisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri nikupe changamoto deal na watu wako wa TEMESA kama hamjawapa fedha naomba muwasaidie. Hata dharura ambayo imetokea hatuwezi kufika Ifakara – Mlimba watu wangepita shortcut kule nyuma, tunavuka pale Ngoheranga tunaingia Ngalimila tupo Mlimba tayari. Leo kutoka Malinyi tunaingiliana na Mlimba unatembea kilometa zaidi ya 300 mpaka ufike Ifakara Mjini uende Mlimba kutoka Malinyi lakini tukimaliza kile kivuko pale Kikove maana yake tutatumia siyo zaidi ya kilometa 40 Malinyi – Mlimba kwa maana Ngoheranga, lakini leo kilometa 300 tunazunguka. Kwa hiyo mheshimiwa Waziri ninakupa hii challenge naomba utusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri umeniahidi, ulikwama kuja Malinyi wakati mafuriko yalipokuwa makubwa maana sehemu nyingi Taifa lilikuwa linakuhitaji, tumelipokea hatulalamiki lakini naamini baada ya bajeti hii kama ulivyoniahidi tutakwenda wote Malinyi ukaone maeneo yote ambayo ninayazungumza. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri utusaidie hili jambo liweze kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkandarasi mpya ambaye anapewa kazi kwenye kivuko, naomba mmuhimize atusaidie, kwa sababu wa kwanza naona amefukuzwa kwa sababu alikuwa mzembe, basi naomba huyu wa pili apewe muda. Matamanio yangu mimi, wananchi wa Malinyi na Mlimba, tunatamani hata Christmas ya mwaka huu tuweze kuvuka pale kwa mara ya kwanza tangu dunia imeumbwa, tuweze kuwa tumeunganika Mlimba na Malinyi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi lakini ndugu yangu Mheshimiwa Bashungwa naomba unisaidie katika haya, sitaki Bunge la Septemba tuje tuanze kugombana tena humu ndani, nakutunzia heshima na ninakuamini ninakuomba utusaidie watu wa Malinyi, Mlimba, Ulanga na Kilombero, ahsante. (Makofi)