Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Nicodemas Henry Maganga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbogwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi mchana wa leo kuweza kuchangia mchango wangu katika Wizara hii ya Ujenzi, yenye bajeti ya trilioni 1.7 ambayo inaenda kuleta mabadiliko kwenye nchi yetu ya Tanzania. Nakushukuru Mheshimiwa Waziri kwa kuteuliwa kuwa Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi lakini ninakuomba Kaka yangu au mdogo wangu, wewe unatokea Kanda ya Ziwa, unayaelewa maeneo yote tunayotokea huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanda ya Ziwa tunayo changamoto barabara zetu ni mbaya sana, nyingi ni za vumbi, magari yanakata chassis kwa ajili ya ubovu wa barabara. Ninaiangalia hii bajeti ni kama ni kidogo sana, kama kuna uwezekano umuombe Mheshimiwa Rais iweze kuongezwa ili kusudu tuweze kutengeneza barabara zetu ziweze kuwa za viwango na zinazopitika kwa kila wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa siwezi kujua kilichoko ndani yake kwenye upande wa fedha, ndiyo maana niko na Mheshimiwa Waziri wa Fedha hapa, nimemsogeza karibu kujaribu kumuuliza tunatokaje huu mwaka wa uchaguzi kuelekea mwaka 2025, lakini amenihakikishia mambo yatakuwa mazuri na tutazidi kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na maeneo ambayo ni hatarishi. Mheshimiwa Waziri kwenye Wilaya ya Mbogwe ambayo ni Mkoa wa Kimadini, tumejaliwa kuwa na madini, mifugo pamoja na mazao mengine. Tunalo Daraja Mwabomba ambalo kila mwaka huwa linasumbua, ambalo naomba ulitengee hata kilometa moja ya lami ili kusudi likitengenezwa vizuri liwe linapitika kila wakati mvua zinaponyesha. Hii ni barabara muhimu sana, huwa inawapa shida sana wananchi na hii barabara ni ya TANROADS, tumeungana na Mheshimiwa Cherehani kwa upande wa Shinyanga na Geita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo daraja lingine la Budoda, Waheshimiwa Wabunge mtakumbuka mliniona nimebebwa na wananchi wa Budoda vijana wa kule, naiomba Serikali iweze kutenga hata nusu kilometa ili kusudi tukaondokane na huu usumbufu wa kila mwaka, kila mvua ikinyesha barabara inakatika wananchi wanateseka, kwa sababu tuna miaka 61 ya uhuru sasa hivi tunaiongoza nchi hii, ni vema tuwe na mtazamo wa haraka kuweza kusaidia wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna daraja la Ilangale ambalo Wilaya hii imeungwanishwa na Wilaya ya Bukombe kwa Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Ikalanga pamoja na Ilangale na penyewe kila mvua zikinyesha hili daraja linakatika. Mheshimiwa Waziri pia naomba unitengee nusu kilometa tu, hii barabara tumeiweka kwenye mapendekezo iingie kwenye TANROADS ili kusudi tuweze kuondokana na usumbufu, kwa kuwa labda pesa za kutengeneza lami hakuna, ndiyo maana naomba nusu nusu tu. Naibu Waziri Mheshimiwa Kasekenya unazifahamu hizi sehemu kwa kuwa wewe umewahi kufanya kazi kwenye hiyo Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna Mto Nyikonga, namshukuru Mheshimiwa Rais kupitia mradi wa RISE, tunaenda kutengeneza lami kutoka Nyikonga kuja Lulembela pamoja na Kashelo. Nakuomba Kaka yangu Mheshimiwa Kasekenya huu mpano uharakishwe haraka kama mlivyoniahidi mwezi wa nane, kwa sababu upembuzi yakinifu kila kitu kimeshaisha, sasa utekelezaji wake ukaanze haraka kwa sababu Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameniambia pesa zipo tayari na mikataba imeshafungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mapendekezo ya barabara tatu, Mheshimiwa Waziri naomba unisikilize sana, Mkoa wa kimadini wa Mbogwe ambao unazalisha dhahabu kwa wingi ukiitoa Geita na Chunya, huwa tunapata mali nyingi sana lakini magari yanayotumika yanabeba zaidi ya tons 30. Kwa sheria zetu kwenye barabara hizi za TARURA, hizi gari haziruhusiwi kutembea chini ya tons 10 kushuka chini. Kwa kuwa, wafanyabiashara wa Mbogwe wanayo malori yanabeba tons 35, sasa Barabara hii ya Kanegele - Mpakali - Mbizi, kuelekea Segese, naomba ipandishwe kuingia upande wa TANROADS ili wafanyabiashara hawa wasiwe wanagombana na watumishi wa TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mara hizi barabara zinapitiwa na haya maroli makubwa, wakati mwingine watumishi wa TANROADS wanapomaliza ubinadamu wanaingia kwenye zile sheria wanagombana, sasa haipo sababu ya kugombana wakati hii nchi moja, Tanzania moja na sisi ni viongozi wananchi wametuamini kuweza kuwasaidia maisha yao waweze kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ipo barabara ya Mwalo – Iyogelo kuja Iponya – Masumbwe hii tumepakana na Wilaya ya Bukombe na yenyewe naomba iingizwe TANROADS ili hawa wafanyabiashara wa marudio wanaobeba zaidi ya tons 30 waweze kuruhusiwa wawe wanapitisha magari yao, mpaka sasa huwa wanapitisha magari lakini ni kinyume cha sheria na huwa wanakamatwa, wanapigwa faini lakini mizigo iliyoko Iyogelo kuipitisha kwenda Masumbwe, haiwezekani bila kupitisha magari hayo ya zaidi ya toni 30, kwa sheria za TARURA, hayo magari yanazuiliwa kupita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo barabara nyingine ya Bwerwa – Mwendamwizo, inatokea Bukoli, Mheshimiwa Kasekenya unaifahamu. Ukitoka Masumbwe kwenda Rugunga mpaka Makao Mkuu ya Wilaya ya Mbogwe, kuna kijiji kinaitwa hapo Bukoli ambacho tumeungana na Magesa, naomba hii barabara na yenyewe ni muhimu sana, wenye maroli wanaitumia lakini sasa hivi kwa vile iko kwenye kiwango cha TARURA, wenye magari makubwa wanazuiliwa kupita. Kwa hiyo, naomba na yenyewe ichukuliwe ili kusudi ikae kisheria ili watu hawa waweze kufanya biashara zao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa zamani, yule aliyekuwepo kabla yako, mwaka jana alinifanyia surprise kitu kizuri sana, pale Mjini Masumbwe alinipa kilometa moja ya lami na wewe nakuomba ukiwa bado Waziri uniachie kumbukumbu ili niweze kukukumbuka kwamba uliwahi kuwa Waziri wa Ujenzi, unisaidie ili kusudi pale Mjini Masumbwe ipo barabara muhimu sana inayotoka lami kwa Moris pale kuelekea Shule ya Kasandalala. Mheshimiwa Waziri naomba hiyo kilometa moja kwa nguvu zako na uwezo wako uliopewa na Mwenyezi Mungu kwenye Wizara yako ya Ujenzi uweze kunisaidia ili kusudi na yenyewe iweze kuunganishwa na hii tuliyopewa na Mheshimiwa Mbarawa ili kusudi wananchi wale waweze kuishi pale Masumbwe Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo Makao Makuu ya Wilaya ambayo yako Mbogwe, ninaiombea sana hiyo Wilaya iweze kupata kilometa mbili za lami kwa sababu pale ndiyo Makao Makuu, vilevile, barabara ni mbaya sana na watumishi bado tunaishi nao mjini, Mvua zinaponyesha wanapata kazi sana kwenda kufanya kazi kwenye Makao Makuu ya Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, nina malalamiko ya wakandarasi. Wakandarasi wamekuwa wakipata kazi kweli lakini pesa zinachelewa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nakuomba ujaribu kulifuatilia sana hili suala. Hasa wakandarasi wa ndani, wanapopata hizi kazi wana rise certificate wanapata usumbufu mkubwa kuweza kupata malipo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyoelewa wakandarasi wa ndani hawana mitaji, wanategemea pesa kutoka Serikali ili kusudi waendelee kufanya kazi vizuri. Nimezungumza na Mheshimiwa Waziri wa Fedha hapa na wewe utamfikishi, wakandarasi wa ndani wapewe kipaumbele ili kusudi wanapopewa hizi kazi za ujenzi waweze kufanya vizuri na waweze kuendeleza Taifa letu, tuweze kupata matajiri wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine hapa, ninaomba kwa vile hii barabara imeshapa lami kupitia Mradi wa Rise kutoka Lulembela; Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu huwa anapata shida sana kwenda pale kwake Bukombe. Serikali ione kila namna kuongezea lami hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu ni mtu mkubwa. Barabara anayopita haifanani na Unaibu Waziri Mkuu. Kwa hiyo, Serikali iangalie kila iwezavyo, iweze kuweka lami, ni kipande kadogo tu kama kilometa 38 ambazo zimebaki na hii barabara iliahidiwa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano, pale alipokuwa anapita tarehe 27 mwezi wa kwanza, kwamba itawekewa kiwango cha lami, kwa hiyo, Serikali isirudi nyuma iweze kuitengeneza hii barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, kwa kuwa wewe Jimbo lako liko Magharibi, tuko mpakani na wewe. Ninakuomba siku moja uweze kusimama Masumbwe tuweze kuziangalia hizi barabara ambazo nazipendekeza ili kusudi uweze kutoa ushauri wa kitaalam pamoja na wataalam wote, mameneja kwa maana ya Meneja wa Mkoa wa Geita na Mkoa wa Shinyanga ili tuende tukaiunganishe Mbogwe yetu iweze kufanana na Mkoa wa kimadini ambao unaingiza pesa nyingi sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante. Naomba hitimisha tafadhali.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nahitimisha kwa kusema, Mheshimiwa Waziri hii trilioni 1.7 naona ni kidogo, fanya mpango Serikali iweze kukuongezea kwa sababu maeneo yote yameharibika ili kusudi iweze kupatikana pesa ya kwenda kukarabati barabara za Tanzania ziweze kupitika. Ahsante sana. (Makofi)