Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Asia Abdulkarim Halamga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika bajeti ya Wizara hii muhimu kabisa Wizara ya Ujenzi katika nchi yetu kwa mwaka 2024/2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kutoa pongezi za dhati kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha kwamba yale matatizo makubwa ambayo tumeyapata kwenye nchi yetu kulingana na majanga ya El Nino kutokea mwezi wa tisa mwaka 2022, tumeweza kukabiliana nayo na ile shida kubwa imeondoka kwenye nchi yetu, jambo ambalo hatukuweza kulitarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee kabisa tunaendelea kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. kile kipindi cha maafa kwetu sisi tunaotoka Wilaya ya Hanang’ ilitolewa zaidi ya bilioni 1.5 kwa ajili ya kuja kuokoa mji wetu na kwa namna hii nichukue nafasi hii kukushukuru sana Mheshimiwa Innocent Bashungwa Mbunge wa Jimbo la Karagwe, hakika wananchi wako hawakukosea kukuchagua na ninataka kuwahakikishia wananchi wako kuwa, wasikosee tena wafanye kama walivyofanya mwaka 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, amekuwa ni mwema kwa watu wa Hanang’, umekuwa ni mwema kwa Watanzania, mafuriko katika nchi yetu yametokea katika mikoa mbalimbali lakini kila sehemu tumekuona kwa bodaboda, Mama ntilie, umehakikisha kwa jitihada zako za kibinadamu pamoja na kumuomba Mungu kuhakikisha kwamba unasimamia vizuri zile fedha za dharura ambazo, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezitoa. Lakini bila kusahau Naibu wako Waziri, Baba yangu Kasekenya, Katibu wako Mkuu ndugu yetu Aisha, Mwana Mama shupavu kabisa ambaye ameanza kutenda haki na amefanya kazi kubwa sana bila kuwaangusha wanawake na bila kuwasahau Naibu Katibu Mkuu wako na timu yako nzima ya Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipekee nichukue nafasi hii kumshukuru sana na kumpongeza Meneja wetu wa Mkoa, hakika katika kipindi kile cha majanga siyo tu Hanang’ ndani ya Mkoa mzima tulipata changamoto hizo za El Nino lakini Meneja wetu Doto Masele hakika ni mchapakazi, mtu bingwa, tunakushukuru sana. Tunajua ni sehemu ya kazi yako na majukumu yako lakini sisi watu wa Manyara tuna kila sababu ya kukushukuru kwa sababu umefanya zaidi ya unavyotakiwa kufanya katika wajibu wako wa siku zote wa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali kwa kuendelea kutenga fedha katika bajeti na kutuletea Mkoa wa Manyara ili kuhakikisha kwamba Mkoa wetu unafikika na unaweza kupitika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali, kuna kila sababu na haja ya kuongeza fedha Mkoa wa Manyara. Tumetengewa kiasi cha shilingi bilioni 11 ambayo ni sawa na aslimia 13 tu ndani ya Mkoa wetu wa Manyara katika utatuzi wa changamoto za barabara, haitoshi, haitoshi, haitoshi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuiomba sana Serikali kwa sababu Mkoa wetu wa Manyara una jumla ya mtandao wa barabara za changarawe pamoja na lami 1657. Hata hivyo, ukizingatia lami ambayo inapita kwenye Mkoa wetu katika mtandao wa barabara ni kilometa 207. Lakini barabara halisi, lami ambayo iko ndani ya Mooa wa Manyara ni kilometa 52 peke yake na hasa ukizingatia Mkoa wetu wa Manyara ni Mkoa wa tatu kwa ukubwa katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuendelee kukuomba sana Mheshimiwa Waziri watu wa Manyara tunakuheshimu na tunakupenda. Toka ukiwa TAMISEMI umekuwa ni sehemu ya kuja Manyara na unaijua sana jiografia, kilometa hizi 52 kwa kweli hazitoshi ndani ya Mkoa wetu. Tukushukuru kwa juzi ulivyokuja na kutupitishia Kilometa saba za kutoka Dareda Center kwenda Dareda Mission ambazo zinasababisha mkoa wetu kuwa na kilometa 59 za lami. Tunakushukuru sana kwa hili lakini tukuombe sana bado mna kazi kubwa ya kuangalia Mkoa wa Manyara hasa ukizingatia jiografia yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuiombe sana sasa Serikali kwa kuangalia barabara hizi za ndani ya mkoa. Tuombe ifunguliwe barabara ya Singe – Galapo - Kiteto mpaka Simanjiro ili kutengeneza mkoa wetu kuweza kuongezewa kiwango hiki kikubwa cha Barabara tuone hii asilimia 59 ya lami inakwenda kuongezeka kulingana na jiografia ya Mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuombe barabara ya Basotu kwenda Mbulu, hii ikifunguliwa mtakuwa mmetusaidia sana, lakini tuishukuru Serikali kwa kutupatia fedha barabara ya Nangwa kuja Gisambalang kutokea Kondoa, hakika tunauona huu ni mchango mkubwa na tunaomba sasa ule ujenzi uanze ili ile dhima ya Mheshimiwa Rais ya kuendelea kuufungua Mkoa wa Manyara tuendelee kuiona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee tuiombe sana Serikali, Mradi wa EPC+F ni Mradi ambao ulikuwa mkubwa wenye matumaini makubwa katika mkoa wetu na mikoa mingine ndani ya nchi yetu ya Tanzania. Barabara ile ingeweza kufungua kati ya Mkoa wa Manyara na Tanga, Mkoa wa Manyara na Morogoro na ingeweza kufungua Dodoma, Arusha pamoja na Singida. Pia, ingeweza kutufungulia barabara za ndani Kiteto, Simanjiro mpaka kuja kutokezea Kondoa. Hakika hii barabara ilikuwa na tija sana na ule mradi uliuwa una mpango mzuri, tuombe Serikali ikazie na ione namna bora ambayo itakuja sasa ili ile nia na dhamira njema ya Serikali iweze kufika mwisho na wananchi waweze kupata barabara hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee kabisa nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri na timu yako kwa namna ambavyo mmeendelea kuwabeba wakandarasi wanawake na hatimaye kwenye bajeti hii tunaona mtawapa zaidi ya kilometa 20 za lami. Huu ni uwekezaji mkubwa kwa wakina mama na ninawaomba sana wakina mama watakaopata hizo fursa wahakikishe wanafanya kikamilifu ili kuendelea kuweka dhamira njema ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumuinua mwanamke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwapongeze wizara kwa sababu mmekuja na mikakati mizuri kwa upande wa vijana ukiangalia ukurasa wa 60 wa hotuba ya bajeti yako, page nzima umeongelea vijana. Tunaiona mikakati ya kufanya mikutano zaidi ya mitano ya kukutana na wanafunzi wa shule za msingi pamoja na sekondari ili kuweza kuwahamasisha kusoma masomo ya sayansi. Huu ni uwekezaji mkubwa lakini bado tumeona mmeendelea kuwa na mpango wa kuwasaidia vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja kwa sababu ya muda ningeendelea kuchangia lakini Mheshimiwa Waziri pamoja timu yako hongera sana. (Makofi)