Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nachingwea
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niungane na wenzangu awali ya yote kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Lindi na wilaya zake ni kati ya maeneo ambayo yameathirika sana na El Nino lakini pia kikaja Kimbunga Hidaya na nyakati zote Mheshimiwa Rais alituma wasaidizi wake akiwemo Mheshimiwa Waziri na kuja kwenye maeneo hayo husika. Pili, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi pamoja na Naibu Waziri Katibu Mkuu wa Wizara na wataalamu wote kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu Waziri ni msikivu lakini Waziri huyu anajali sana, Waziri huyu simu yake hata ukipiga saa nane ya usiku anapokea, anakusikiliza mnashauriana, mnatafuta ufumbuzi wa jambo ambalo linakukabili Mheshimiwa Waziri tunakupongeza sana lakini tunakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata pale aliposhindwa kuingia wakati ule Wilaya ya Nachingwea na Liwale vikiwa kisiwa Mheshimiwa Waziri kuna chochoro zingine alipita zilikuwa haziwezekani kupita kwa nafasi yake kama Waziri lakini alisema Mheshimiwa Mbunge nimekuja kufanya kazi hapa ya wananchi twende site tulipita kwenye maeneo hayo Mheshimiwa Waziri tunakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kabla ya hayo nilifikiri kwamba kwa sababu kulikuwa na mambo ambayo nilikuwa na kiu nayo nikasema sasa shilingi ya Waziri nitaondoka nayo kurudi nayo kule Nachingwea lakini Mheshimiwa Waziri kwa wema huu uliotufanyia lakini kwa namna ulivyotujali tukiwa na shida siondoki na shilingi yako kwenda nayo kule Nachingwea badala yake tutaendelea kuomba utusaidie hata yale mambo mengine ili yaweze kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo Barabara ya Masasi - Nachingwea mpaka Liwale kilometa 175. Barabara hii ilishawekwa kwenye mpango wa kujengwa kuanzia 2021/2022, 2022/2023 na baadaye ikaingizwa kwenye Mfumo wa EPC+F mwaka jana na tayari mkataba ulisainiwa tarehe 16 mwezi wa sita, 2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mambo ambayo yamechelewesha sana maendeleo kwenye Mikoa ya Kusini ni pamoja na mawasiliano na miundombinu ya barabara. Baada ya kusaini ule mkataba ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami Wananchi wa Mikoa wa kusini kwa maana ya Lindi lakini barabara hii inanufaisha majimbo manne Jimbo la Nachingwea, Jimbo la Ndanda, Jimbo la Masasi na Jimbo la Liwale. Tumekaa mkao wa kusubiri na huku tukiendelea kumwombea dua njema Mheshimiwa Rais kwa wema alioufanya kuelekea hata kusaini huo mkataba ni hatua kubwa na nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu wananchi sasa wamebaki hawaelewi chochote kinachoendelea kuhusu ujenzi wa barabara hii, sasa inakimbilia mwaka na Naibu Waziri hapa amejibu kwenye swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecil Mwambe kwamba mradi ule utatekelezeka kabla ya bajeti hii kuisha ambayo kimsingi tumebakiwa na mwezi mmoja kipindi cha bajeti hii kuisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hotuba yake aweze kutoa ufafanuzi ambao utawafanya wananchi wa majimbo yale manne kwa maana ya Nachingwea, Ndanda Masasi na Liwale waweze kujua nini kinaendelea. Tunajua nia njema ya Mheshimiwa Rais na nimeona kwenye hotuba yako hapa ya bajeti Mheshimiwa Waziri lakini mimi kama Mbunge najua wananchi wanatamani kujua zaidi Serikali yao ina nini kuhusu ujenzi wa barabara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko barabara nyingine ya kutoka Nanganga kwenda Nachingwea kilometa 43. Mheshimiwa Waziri wakati uko pale Nachingwea tulizungumza na hili mimi nikuombe sana tayari upembuzi yakinifu unaendelea basi baada ya kumaliza ili na sisi tuende mkoani tukiwa na uhakika wa usafiri utusaidie kuhakikisha hii barabara kwa kipande kile kilichobakia kiweze kujengwa na tuweze kufika mkoani vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili niishukuru sana Serikali kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka pale Nanganga, Ruangwa kuelekea Nachingwea. Tunaishukuru sana Serikali kazi hii kubwa ni nzuri na sisi kama Wana-Lindi na Wana-Nachingwea tunaendelea kuunga mkono juhudi hizi za Mheshimiwa Rais na tunapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko barabara nyingine ya kutoka Nachingwea - Kilimarondo mpaka kwenye Mto Rumesule pale. Kuna Mto Rumesule, Mto Rumesule unaunganisha kati ya Mkoa wa Lindi na Mkoa wa Ruvuma. Nikuombe Waziri hapa yaani kilometa 90 kutoka Nachingwea kwenda Kilimarondo zinamilikiwa na TANROADS halafu kuna kilometa 16 zinamilikiwa na TARURA upande wa Ruvuma wanamiliki TANROADS na hata lile daraja limeshafanyiwa usanifu waliofanya ni TANROADS sisi kwenye vikao vyetu vya mkoa tulishamaliza jambo hilo na tuombe jambo hilo ulichukue ili barabara yote iweze kuhudumiwa na TANROADS tuweze kupata sasa uhakika wa kuendelea kujengwa barabara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Kibiti - Lindi wenzangu wameizungumzia. Mheshimiwa Waziri kwa bahati nzuri umepita sana hiyo barabara. Hiyo barabara ina mashimo makubwa na sasa imekuwa ni adha na hiki Kimbunga Hidaya kimekuja kutuonesha maeneo mengine ambayo tayari yalishakuwa mabovu. Hii barabara tumeipigia kelele kwa muda mrefu sana mwone namna ambavyo Wizara mtaendelea kuona namna ya kukarabati hii barabara na Mheshimiwa Waziri kwa namna ilivyo kwa sasa kuna maeneo ambayo hayafai kuweka viraka tena yanafaa kubadilisha kabisa kwa sababu yameharibika. Sehemu ambayo ungeweza kutembea kilometa kwa muda fulani lakini utakwenda kwa mwendo mdogo kiasi ambacho shughuli zingine za wananchi zinasimama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, otherwise mimi niendelee kumtakia heri Mheshimiwa Waziri na timu yake kazi hii wanayoifanya Watanzania tunaiona lakini utakapokuja ku-windup bado niendelee kukuomba tena sema neno kuhusu Barabara ya Masasi - Nachingwea - Liwale ili wananchi wa maeneo hayo waweze kutulia mioyo yao ili wajue kabisa kwamba Mama, Dkt. Samia Suluhu Hassan yuko kazini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)