Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia Wizara ya Ujenzi. Kwanza naomba nimtangulize Mwenyezi Mungu katika mchango wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa sana ambayo ameendelea kuifanya katika nchi hii hongera sana Mama tuko nyuma yako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wetu wa ujenzi Innocent Bashungwa kwa kweli kama jina lako lilivyo Innocent uko vizuri na kila mtu amesema kazi nzuri unazozifanya endelea kumtanguliza Mungu pia katika kazi yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Naibu Waziri wa ujenzi Engineer Kasekenya, kwa kweli unafanya kazi nzuri sana na unatujibu maswali yetu vizuri sana kila siku hapa ahsante sana. Pia niendelee kumpongeza Katibu Mkuu wetu Engineer Balozi Aisha hongera sana unatuwakilisha vizuri sana wanawake na uko jikoni katika Wizara hii ya Ujenzi na watendaji wote pia ninawapongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitakuwa sijamtendea haki nisipompongeza Engineer Wetu wa Mkoa wa TANROADS Iringa, Engineer Msangi hana baya, anafanya kazi nzuri sana na ana ushirikiano mzuri sana endelea kushirikiana na sisi Wabunge wote hongera sana kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Serikali iwapatie Wizara hii pesa ya kutosha kama ambavyo Wabunge wengi wamesema pesa hii waliyotoa haitoshi ongezeni ili barabara zetu ziweze kujengwa kwa kiwango lakini pia ili wakandarasi wetu pia waweze kulipwa. Pia ili wanaodai fidia waweze kulipwa kwa sababu barabara ni uchumi wapeni pesa ya kutosha Wizara ya Ujenzi ifanye kazi katika barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na Barabara ya Dodoma - Mtera - Nyang’oro mpaka Iringa hii barabara haijajengwa kwa kiwango, hii barabara ina makorogesheni mengi sana mimi naomba Serikali iangalie Mheshimiwa Waziri hebu pita; twende tu hata kesho baada ya hii Wizara ukaangalie hii barabara ilivyokuwa mbaya, magari makubwa yanapita kwenye hii barabara lakini viraka ni vingi sana ukikwepa unaingia kwenye korogesheni. Kwa hiyo naomba hebu iangalieni hii barabara ni ya kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ukienda kwenye kona zile za Nyang’oro maporomoko wakati wa mvua kila wakati Meneja wetu analala pale. Naomba tena Mkoa wa Iringa wapewe pesa ya kutosha ukarabati kwa sababu pia inakuwa ina makorogesheni lakini pia maporomoko ifanyiwe upembuzi yakinifu ili tuone tunasaidiaje ile barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Mgololo - Mafinga mkataba ulisainiwa toka mwaka 2022/2023 hii barabara majimbo yote matatu ya Mufindi yanapitiwa, lakini hii barabara ni ya kiuchumi. Malori yanakuwa yako pale muda mrefu nini lini sasa itajengwa? Tunawaombeni utakapojibu hebu utujibu hii barabara lini itaanza ujenzi kwa sababu ni barabara ambayo ni ya kiuchumi na Marais wote wametoa ahadi katika hii barabara. Pia barabara ya Nyororo - Mtwango tunashukuru imeanza kujengwa lakini tunaomba sasa muifikishe mpaka Igowole.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napongeza kwa upanuzi wa Barabara ya Kitonga. Mlima Kitonga tumeuliza sana maswali pale na barabara ile ilikuwa inakwamisha sana magari. Ninawaombeni jamani mmeanza kujenga njia ile moja mngefanya hata mbili ili msiendelee kurudia mara kwa mara kwa sababu ile barabara ni barabara inakwamisha mno magari na magari makubwa kuna ajali kila wakati. Tunawaombeni muongeza pesa ya kutosha ili angalau tuweke hata barabara nne katika ule Mlima Kitonga. Vilevile endeleeni kufanya upembuzi yakinifu kwa ile barabara mbadala ili tukipata matatizo. Lile eneo toka Mahenge – Udekwa - Wotalisoli, Mlafu inatokea Ilula itaweza kutusaidia hapo baadae.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Barabara ile ya Ipogolo - Kilolo. Hii barabara tunakupongeza Mheshimiwa Waziri ulikuja ukasaini na hii barabara pia inapitiwa na majimbo matatu lakini tunakuomba kama nilivyokuomba siku ile kile kipande ambacho hakijawekewa lami kingewekewa kwa sababu ndiyo kinakwamisha magari mengi, kile kinachotoka Kilolo pale kibaoni mpaka Kidabaga kiwekewe lami ili hii lami inaweza ikaungana na ya pale Ng’ang’ange kwenda mpaka kule Boma la Ng’ombe. Pia kuna hii barabara ikitokea pale Kidabaga iende Idete ndio kwenye shida sana watu wanapata shida wanakwama tunaomba sana Mheshimiwa Waziri ukija tena nenda kaitembelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, pia kuna barabara muhimu sana pale Kilolo, inatoka Kilolo kwenda Kising’a inakwenda Mkalanga, Wotalisoli, Mlafu mpaka Ilula, wananchi wanapata shida kwenda mjini wakati hii barabara ikiwa inapitika japo msiweke lami lakini ipitike watu waende Makao Makuu ya Kilolo waende kwenye Ofisi za Kilolo wanapata shida kupita mjini, ninawaombeni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hii bypass ya Barabara ya Tumaini. Ninakuomba magari makubwa kupita katikati ya mji ni mateso makubwa itatokea ajali kubwa lakini wafanyabiashara wanafanya biashara kwa shida mno magari yanafungwa wanalipishwa pesa lakini pia wafanyabiashara hawafanyi biashara zao vizuri kuna siku ajali itatokea pale Iringa Mjini jamani nawaombeni hii barabara ya bypass iishe sasa, iishe Mheshimiwa Waziri uje utuambie tunapata mateso makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Kiwanja cha Iringa. Hiki kiwanja kimeanza kujengwa siku nyingi sana, sasa ni lini kitaisha? Tunamshukuru Mheshimiwa Rais alikuja kwenye hiki kiwanja akazindua tukajua sasa kitakwisha lakini bado mpaka leo zaidi ya miaka mitano sita, saba bado lakini kinachoniuma mimi kuna Shule ile ya Nduli shule ya msingi watoto wanateseka miaka saba sasa hivi wanateseka Diwani wa pale ameugua mpaka afya ya akili kwa sababu haikarabatiwi. Ile shule inatakiwa ihamishwe watoto ufaulu wao umekuwa ni mbaya mno kwa sababu wanaishi kwenye mateso, vyoo havikarabatiwi, shule haikarabatiwi, walimu wanapata shida makelele mengi. Ninakuomba Mheshimiwa Waziri hii shule iondoke iende ikajengwe kunakotakiwa kwa sababu tayari ilitakiwa ihamishwe toka 2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie Barabara ya Msembe inayokwenda Ruaha National Park. Hii barabara pia muda mrefu sana sana tumekuwa tukiomba ikarabatiwe hii itatuongezea uchumi sisi wananchi wa Mkoa wa Iringa lakini na Taifa zima tunakuomba ni muda mrefu sana sana lakini mwisho wakandarasi walipwe pesa zao ninakuomba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niunge mkono hoja hii ya ujenzi, ahsante sana. (Makofi)