Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sengerema
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana lakini leo kidogo naomba nianze kwa Dua kumwombea sana Mheshimiwa Rais; “Bismillah Rahman Rahim Rabbanna ahfilana wallii ikhwanina ladzina sabaquna bil iman, walatajiru fil ikurubina illa Al ladhina amanu rabbanna innaka raufur Rahim.” Mwenyezi Mungu umjalie sana Mama yetu Samia Suluhu Hassan. Kwa nini nimeanza na dua hii, ni kwamba kelele zilikuwa nyingi sana siku zinavyozidi kwenda kelele zinapungua katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka juzi na mwaka jana barabara zilitengenezwa kwa kiwango cha hali ya juu tokea nchi hii imepata uhuru na tulikuja hapa sisi mwaka juzi kwa kuchukua mgawanyo kwamba TANROADS wapate pesa zao na TARURA wapate pesa zao. Kule TARURA walibakiza 30% zilizokuwepo za mwanzo halafu TANROADS wakawa wana pesa zao kule 70% kwenye pesa za Mfuko wa Road Fund. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ndugu zangu kwa ilivyokuwa mafuriko yametokea ya kila namna, mara sijui kuna Hidaya, sijui kuna Farida. Kwa hiyo ikatokea hali ya sintofahamu katika nchi hii. Haijawahi kutokea mvua ya namna hii na mvua hii mimi nimepita katika maeneo kule nilikuwa nimetembelea maeneo ya Tabora sehemu za Tura kule, Maguliati sijui Loya watu wanasema kwamba tena hawana habari kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani nyinyi huku mnavyohangaika na barabara wale hawana habari wanasema tena wanazungumza kwa Kisukuma kwa huyu Mama alikuwa wapi mvua za namna hii tunapata mpunga wa ajabu mwaka huu. Sasa yaani wao wanaombea mvua izidi sisi huku tunatafuta barabara Wabunge Bungeni yaani hawana habari na nyinyi. Kwa hiyo kuna watu yaani hii mvua wao wanaitaka wanataka huyu mama aendelee kuomba alikoenda kuomba mvua hii yaani ni maajabu makubwa sana, halafu humu ndani Wabunge tunahangaika sasa na barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ndugu zangu nataka nianze kuchangia, Bismillah. Kwanza nataka nikutoe hofu Mheshimiwa Waziri Bashungwa ni kwamba kwa mimi hivi ambavyo Mwenyezi Mungu akijalia mwaka huu Mwezi wa Kumi na Mbili nakwenda kupokea daraja. Tukiwa hai tunakwenda kupokea Daraja la Kigongo – Busisi kilometa 3.3. Ndugu yangu shilingi bilioni 730, kwanza naangalia unaingia kwenye historia ya dhahabu Mjomba wangu Bashungwa wanapokea daraja hili na Mama anakabidhi daraja hili ambalo lina uwezo wa kukaa miaka 100 zaidi ya Marais kumi watakuja kuliangalia daraja hili, mpigieni makofi Mheshimiwa Rais kwa kazi anayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge ambao hamjafika Sengerema nawaombeni mkaribie mje kuona huu muujiza uliotokea Sengerema kule. Kwanza najiuliza sana wakati Mheshimiwa Dkt. Magufuli anawaza habari hii ya kujenga daraja ndani ya ziwa mimi niliona kama hadithi, amefariki Mheshimiwa Dkt. Magufuli daraja lina 24%. Leo tunavyozungumza daraja lina 89% bado 11% tu daraja likamilike. Tunatengeneza muujiza mwingine ndani ya Tanzania. Ndugu zanguni kelele mpaka sasa hivi watu wananiuliza Mheshimiwa Tabasam mbona umekaa kimya kwani unafikiri haya yanayofanyika Sengerema hamuyaoni? Nitakuwa mtu gani mimi ambaye sina shukrani? Mtu gani ambaye sina shukrani? haiwezekani. (Makofi/ Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza ni kwamba daraja lile sasa hivi wanaanza kuunda barabara ya lami upande wa Misungwi kuja pale Sarajani na upande wa Sengerema kwenda Darajani. Tunachosubiri hapa Mheshimiwa Bashungwa kwenye design yako hii ambayo inaendelea pale tunakuomba daraja hili lilindwe kwa mizani. Hatuona mpango wa ujenzi wa mizani, magari yanayoingia darajani tusije tukaharibu daraja letu sisi. Huu ni urithi tunapata sisi wana Sengerema ambao wakina Tabasam tutakuwa hatupo lakini tutakuwa kwenye historia kwamba Mheshimiwa Tabasam alikuwa Mbunge daraja limekwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ninachomshukuru Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yako ya Wizara ni kwamba design ya lami lile daraja linakuja kupokelewa na lami yingine kutokea Busisi kwenda Ngoma kwenda Nyang’hwale tayari mkandarasi yuko kule anaendelea na usanifu na Wana-Sengerema jamani nawaombeni mmpe ushirikiano. Pia kuna lami ya kutokea Sengerema kwenda Ngoma kuna lami ya kutokea Kamanga inaendelea kilometa tatu na kilometa saba zingine Mheshimiwa Waziri umetupa tunakushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninachotaka kusema vivuko vyetu vyote vinavyoendelea kujengwa nilikuwa na Mheshimiwa Naibu Waziri tumekwenda na wewe kwenye kikao Mheshimiwa Waziri pamoja na Katibu Mkuu na timu yake Mkandarasi Songoro tayari jamani tunaombeni Serikali imekubali kumlipa pesa Waziri wa Fedha kanihakikishia kwamba analipwa pesa zake mwezi huu kabla haujaisha na bado siku mbili. Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri tunakupitishia bajeti yako tumlipe Kandarasi Songoro vivuko vyetu viweze kufanya kazi. Nakushukuru kwa design ya vivuko hivi vivuko viko salama upande wa ndugu yangu Mheshimiwa Eric Shigongo tayari kivuko kiko salama kule hivi tunavyozungumza Mheshimiwa Waziri tutakwenda kukabidhi kivuko hicho lakini kuna Kivuko cha Buyagu Mbalika sasa hivi kiko 60% na magati sasa hivi yameshaanza kutengenezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Gati la Buyagu - Mbalika tayari mkandarasi ameshapatikana na ameshasaini mkataba. Kuna gati lingine la ndugu yangu Mheshimiwa Mabula pale Luchelele, kuna gati linatengenezwa Luchelele pamoja na Ilunda, kwa hiyo tuko vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni barabara yetu sisi ya Sengerema - Nyehunge tuko kwako na Mheshimiwa Eric Shigongo tumezungumza na Katibu Mkuu pamoja na Mtendaji wa TANROADS mnamchukua mkandarasi wa pili CCIC kwenda kutengeneza barabara tunawapongezeni sana, kwa sababu huyu bwana ndiye anayejenga daraja na vifaa vyake viko pale na kokoto anazo palepale. Kwa hiyo hii barabara itakwisha kwa muda wake, hatuna wasiwasi kabisa na jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakupongeza sana kwa barabara zetu zilizopanda hadhi Sengerema kwenda Chifufu kilometa 43 tayari mkandarasi ameshapatikana kuna shilingi milioni 500, Nyitundu kwenda Nyamatongo Karumo shilingi milioni 500 iko pale na mkandarasi yuko site. Barabara nyingine inayopita kwa mama yako mzazi kutoka Ikoni kuja Sima moja kwa moja kwenda mpaka Buyagu kwenye ferry na yenyewe tunakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo uko vizuri Mheshimiwa Waziri hawa wanaozungumza kwamba wanataka kukamata shilingi wanataka kwenda kukuonea tu lakini ninachotaka kukuambia atakayekamata shilingi Mungu anamwona. Ahsante sana kwa kunisikiliza. Ahsanteni sana Waheshimiwa Wabunge tupitishe bajeti hii bila mgomo wa aina yoyote, mtatutia simanzi sisi akina Mheshimiwa Tabasam ambao tunaona miradi inaendelea hali ni ngumu sana Mama yetu tumwombee kwa Mungu.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naomba kuunga mkono hoja.