Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naunga mkono hoja iliyopo mezani ya Wizara ya Ujenzi.

Mheshimiwa Spika, nitakuwa na mambo machache, jambo la kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anazozifanya, ninampongeza Waziri wetu Mheshimiwa Innocent Bashungwa, nampongeza Katibu Mkuu wa Wizara, Watendaji na Naibu Waziri pia kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya kwenye Wizara hii. Mzigo akiubeba mwenzako ni rahisi kuona ni mwepesi lakini kazi ambayo wanaifanya wenzetu wa Wizara ya Ujenzi ni kazi kubwa sana na sisi wananchi wa Makete tunaitambua.

Mheshimiwa Spika, toka jana nasikiliza michango mingi hapa ndani, Waheshimiwa Wabunge wanatambua efforts za Mheshimiwa Waziri kwenye ujenzi na kupambana na mambo ya barabara kwenye nchi yetu, kwa hiyo, mimi Mheshimiwa Waziri nakupongeza sana, kwanza ni mtu ambaye ni msikivu na pili ni darasa kwa sisi vijana tunajifunza jinsi gani ambavyo inatakiwa tu-behave na jinsi gani ya kufanya kazi za watu. Kubwa zaidi ni jinsi ambavyo una-attend kwenye matukio kwa wakati, mimi niseme wazi ulikuja Makete mdogo wako nilipokwambia kwamba Makete kuna changamoto ya barabara kutoka Makete kwenda Mbeya, ulifika site na wananchi wa Makete wamenituma, Mwenyekiti wangu wa Chama, Katibu DC na Mkurugenzi wamenituma kukushukuru sana kwa kufika Makete, kufika kwako Makete kumekuwa ni muarobaini kwa barabara ile angalau wananchi sasa wameona jitihada.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu wa Makete tulikuwa tukisimama kwenye hili Bunge siku zote ni barabara kutoka Makete kuelekea Mbeya ilikuwa ndiyo kaulimbiu yetu. Pili, hata kwenye uchaguzi yeyote anayetafuta nafasi yoyote kwa Jimbo la Makete alikuwa anatumia barabara ya kutoka Makete kwenda Mbeya. Leo nasimama hapa siyo kwa sababu nyingine yoyote ni kuishukuru Serikali kwa sababu mkandarasi yuko site anaendelea na kufanya kazi. Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yangu iliyopita wakati Mheshimiwa Mbarawa ni Waziri nilisema: “Hatutachanguliwa kwa uzuri wa suti au uzuri wa tai tunazozivaa lakini tutachaguliwa kama miradi ya maendeleo inaenda kwa wananchi”.

Mheshimiwa Spika, leo hii wananchi wa Makete wanasema ahsante sana kwa sababu wanamuona mkandarasi yuko site anaendelea na kazi. Jambo moja pekee ambalo wananchi wa Makete wanaliomba ni mkandarasi alipwe fedha, amefika site lakini speed yake siyo kubwa sana kwa sababu kuna changamoto ya fedha, hajalipwa. Mnasema advance payment, mkandarasi wetu hajapewa fedha kwa sababu ya changamoto ambazo mnazipitia. Nakuomba Mheshimiwa Waziri chukueni hatua ya kumlipa mkandarasi huyu kwa sababu ulipokuja kule uliona kuna vifaa vingine pia ameshindwa ku-mobilize kutokana na uhaba wa fedha. Sasa nakuomba ili wananchi wa Makete tunapoelekea huko mbele tuwe na nguvu kubwa zaidi ya kuiunga mkono Serikali ni kuona mkandarasi huyu anaendelea, ni kilomita 36 ambazo amezianza.

Mheshimiwa Spika, barabara hii ya kutoka Makete kwenda Mbeya ni barabara ya kiuchumi, ndiyo oxygen ya Wilaya yetu. Kama ni oxygen ya Wilaya yetu kuna lot mbili bado, imetangazwa hiyo lot ya kwanza katika kilometa 96 za barabara yote, lot moja tu ya kilometa 36 imetangazwa bado lot mbili. Mheshimiwa Waziri tunakuomba kama kuna mchakato unatakiwa uanze ni kutangaza lot mbili, lot ya kwanza kutoka Makete kupita Bulongwa kwenda hadi pale Ipelele na nyingine ya kutoka Kikondo kufika Mbeya ni kilomita chache chache ambazo zimebaki, tunakuomba sana Mheshimiwa Waziri ulichukulie hatua barabara hii sisi ndiyo oxygen.

Mheshimiwa Spika, kutoka Makete kwenda Njombe ni mbali kuliko kutoka Makete kwenda Mbeya kwa Mheshimiwa Dkt. Tulia, ni sehemu ya karibu zaidi na sisi tumeiuchagua ile kwa sababu pia shughuli kubwa za kibiashara na kiuchumi tunazifanyia pale. Kwa hiyo, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, barabara hii ndiyo oxygen ya Wilaya yetu ya Makete.

Mheshimiwa Spika, niliporudi Makete wananchi wanasema kwa jinsi ambavyo barabara zimeharibika nchini matarajio yao ni kuona Wizara ya Fedha wanaiangalia Wizara ya Ujenzi kwa jicho la karibu sana. Mheshimiwa Waziri kwa fedha ulizotengewa kwenye bajeti hii nikuambie wazi tutaendelea kukulaumu. Tutakulaumu kwa sababu fedha hizi ni kidogo sana, haziwezi kukusaidia.

Mheshimiwa Spika, tunaiomba Wizara ya Fedha waiangalie Wizara ya Ujenzi kwa jicho la karibu, miundombinu ya barabara, wananchi ukitaja TARURA ni nadra sana kukuelewa kuhusu TARURA, lakini ni nadra sana kukuelewa kuhusu TANROADS na barabara nyingine. Kwa hiyo, nakuomba Mheshimiwa Waziri na naliomba Bunge tuongeze fedha kwenye Wizara ya Ujenzi. Kama kuna source zozote tunaweza tukazichukua sehemu Mheshimiwa Waziri wa Fedha nakuomba kama kuna jinsi ya kum-support Innocent Bashungwa Waziri wa Ujenzi, kupata fedha za kutosha ili aweze kujenga barabara na kurekebisa barabara zilizoharibika ni vema tukamuongezea fedha kwenye bajeti yake. (makofi)

Mheshimiwa Spika, huwezi kuzungumza uchumi wa nchi kama hujazungumzia barabara, huwezi kuzungumzia afya za watu kama hujazungumzia barabara, huwezi kuzungumzia kilimo cha nchi kama hujazungumzia barabara, huwezi kuzungumzia biashara za ndani na za nje kama hujazungumzia Barabara, barabara ndiyo uti wa mgongo wa Taifa lolote lile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tumepitia katika kadhia ya barabara kuharibika sana, nakuomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, tunajua unafanya kazi nzuri sana lakini Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Bashugwa aongezewe fedha ili Wizara hii iweze kuleta tija na kufanya marekebisho. Tutakuwa tumejenga vituo vya afya vingi sana lakini wagonjwa hawatafika kwenye vituo vya afya kutokana na changamoto za Barabara, tunaweza tukawa na changamoto za vifaa kupanda bei kutokaana na barabara kuwa mbovu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina kila sababu ya kuendelea kuwashawishi pia Wabunge wenzangu tuweke joint kumsaidia Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi ili aweze kupata fedha za kuongezewa ili barabara ziweze kujengwa kwenye nchi hii.

Mheshimiwa Spika, sina mambo mengi lakini sisi kama wananchi wa Makete tunapongeza sana tunae Mkurugenzi wa TANROADS mzuri sana Mkoa wa Njombe, Mama yetu Shallua, anafanya kazi nzuri sana, anatuunga mkono Wabunge na anatushirikisha kwenye changamoto zote na anafika kwa wakati, kwa kweli nisipompa maua yake nitakuwa sijamtendea haki. Meneja wa TANROADS Mkoa wa Njombe anatu-support sana na pale ambapo kuna changamoto anatusaidia.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa mezani kwako kuna barabara ya kutoka Lupila kuelekea Kipengele. Mheshimiwa Waziri ulipokuwa TAMISEMI ulifika Makete ile barabara tuliileta mezani kwako uipandishe kwenda TANROADS, wana-Lupila na wananchi wa Makete wanakuomba barabara ile ipelekwe TANROADS angalau iwe kwa kiwango cha changarawe Mheshimiwa Waziri ili iweze kupitika.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana, kengele ya pili imeshagongwa.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, ahsante sana. (Makofi)