Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Agnes Elias Hokororo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja iliyopo mezani. Awali ya yote naomba nitumie fursa hii kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutekeleza miradi ya kimkakati ya kitaifa kwenye Wizara hii. Kipekee, kwa kazi inayoendelea na hakuna kilichosimama kwa barabara ya Mnivata – Tandahimba – Newala – Masasi, kilometa 160. Mkandarasi yuko kazini na ujenzi unaanza, tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Sisi tutamlipa kwa imani tuliyonayo kwake na kura zitatosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuanza kumpongeza, tofauti na tulivyo wengi, nimpongeze sana Balozi Dkt. Aisha Amour, Katibu Mkuu, kwa kazi nzuri na yeye ni mwana-Mtwara anajua changamoto za huko. Nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri. Naishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi pia kwa zile kilometa 35 za Mangamba – Madimba – Msimbati, taratibu za kupata mkandarasi zinaendelea, tunaishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru pia Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa zile kilometa 200.51 za Mtwara – Mingoyo – Masasi. Tunaambiwa taratibu za manunuzi zinaendelea na hii ilikuwa bajeti ya 2023/2024. Tuna uhakika kabisa hata kama zimebaki siku chache lakini taratibu zinaendelea, tuna imani kwamba hii barabara itajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa naomba nishauri; kwa sasa hii barabara ndiyo inapita malori yote yanayotoka Liganga na Mchuchuma kwa hiyo mzigo ni mkubwa. Tunaomba itakapojengwa ijengwe kwa kiwango cha juu ili isije ikawa kama ile barabara ya Dar es Salaam – Lindi – Mtwara ambayo imekwisha kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu kwa sasa hatuna mategemeo ya kupata treni ile ya Kusini kwa sababu bajeti imepita na haipo, kwa hiyo tunategemea hii barabara kwa mambo yote. Kwa hiyo, tunaomba sana hilo lizingatiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo naomba kushauri kwenye maeneo mawili, la kwanza; barabara ya Dar es Salaam – Lindi – Mtwara tunajua haikujengwa kwa kiwango cha juu na ndiyo maana imepondeka pondeka. Kila baada ya mita 100 kuna kiraka na hii barabara kwa sasa hali yake ni mbaya. Tunajua awamu iliyopita Hayati Mheshimiwa Magufuli aliagiza itengenezwe lakini kwa bahati mbaya mpaka sasa hivi haijatengenezwa. Tunaomba sana, Kimbunga Hidaya kimekwenda tu kuongezea madhara lakini tunafahamu barabara hii iko hoi. Sisi kule hatuna meli kwa hiyo tunategemea barabara hii peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sasa inafanya gharama za maisha kwa wananchi wa Lindi, Mtwara na maeneo hayo hata Pwani yawe magumu kwa sababu hata mizigo ya mabegi inatozwa kwenye mabasi, sembuse mizigo ile inayokwenda madukani. Kwa hiyo, tunaomba hii barabara ijengwe kwa kiwango cha lami maana sidhani kama itakuwa ni ukarabati kwa sababu imeharibika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili; ni huyu anayeitwa EPC+F. Hapa ndani tumeuliza maswali ya msingi na maswali ya nyongeza zaidi ya 15, tukipata majibu kwamba ujenzi unakwenda kuanza lakini cha kusikitisha ni kwamba kwenye bajeti hii hakuna japo tuliambiwa ujenzi utaanza na utiaji saini ulifanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nashauri, sasa tunapojenga barabara mimi nilikuwa nadhani kuna mambo matatu ya kuzingatia. Jambo la kwanza ni sababu za kiuchumi, pili ni sababu za kiusalama na tatu ni za sababu za kijamii. Kwa hiyo, Wizara iweke vipaumbele na izingatie. Kwa nini tumeingiza mikoa 13 kwenye EPC+F, tumeingiza majimbo 32 kwenye EPC+F, Wabunge wameenda kujinadi kule hizi barabara zitajengwa na imeshindikana?

Mheshimiwa Spika, sasa kama imeshindikana tutafute utaratibu mwingine. Jambo la kwanza ni kuboresha mfuko wa barabara kwa kutafuta vyanzo vingine ili ikafanye hiyo kazi kwa sababu sasa hivi uwezo wake ni shilingi bilioni 600 lakini mahitaji ni shilingi trilioni mbili; haiwezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa bajeti ya mwaka huu shilingi trilioni 1.7 tunaona shilingi bilioni 900 inakwenda kulipa madeni, shilingi bilioni 700 plus inayobaki haiwezi kukamilisha zile shilingi trilioni 2 zinazotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili; huu utaratibu umeshindikana, hii module imeshindikana basi tutafute labda PPP, pengine inawezesha. Hatusemi wananchi watachangia lakini Serikali ichangie, itafute mwekezaji halafu Serikali itaona kama ni huduma basi Serikali itakuwa imebeba mzigo na wananchi watakuwa wamepata hiyo barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano kule kwetu, Barabara ya Masasi – Nachingwea – Liwale, hizo 175, hali ni mbaya, hali ni mbaya, hali ni mbaya. Kwa hizi mvua za El Nino, madaraja yaliondolewa, Daraja la Mto Lukuledi liliondolewa, lakini kule Liwale Mheshimiwa Bashungwa amekwenda na amejionea, hivyo kweli anaweza akasema hali ni nzuri ama hali ni ya kuridhisha? Kwa hiyo, ni muhimu kufanya jambo, hata akatupa matumaini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kule zamani kulikuwa na utaratibu, maeneo ambayo yalikuwa hayapitiki kabisa tumekuta kuna zege, watu wamejenga, lakini kama si zege akajenga madaraja, tukaanza kidogo kidogo. Ninavyoona kwa sasa EPC+F kwa utaratibu wa bajeti uliokuwa nayo hautaweza na wala hauwezekani, hiki ni kizungumkuti. Serikali itafute utaratibu mwingine wa PPP wa kujenga barabara zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la mwisho ni kuhusu ulipaji wa fidia. Naomba maeneo yote hayo yalipwe fidia ili wananchi wawe na amani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja na ahsante. (Makofi)