Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Eng. Mwanaisha Ng'anzi Ulenge

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi ya kuchangia. Awali ya yote nimshukuru Mungu muumba ardhi na nchi kwa kuniwezesha kusimama mahali hapa muda na wakati kama huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nami nichukue fursa hii kumpongeza Rais wetu mpendwa mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha Taifa letu linaendelea kupata maendeleo. Kazi kubwa alizozifanya ni pamoja na kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuunganika na nchi za jirani kwa kuwa na mtandao mkubwa kwa takribani 200,000; tunao mtandao huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile niipongeze sana Wizara pamoja na watendaji wake wote chini ya uongozi wa dada yangu Engineer Aisha kwa kazi kubwa wanayofanya kuhakikisha kama Taifa tunaungana mkoa kwa mkoa, wilaya kwa wilaya na mataifa ya jirani. Kipekee kabisa nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri rafiki yangu na kaka Mheshimiwa yangu Bashungwa na Naibu wake. Kiukweli kabisa bila kupepesa maneno na sisi wanasiasa wakati mwingine tunapaswa kuwa realistic, tuwe wakweli wa nafsi setu. Kwenye suala zima la miradi yetu hii leo tunayoipigia kelele sana, kutokufanyika kwa wakati, kutokumalizika kwa wakati na wakandarasi kutokulipwa kwa kweli Mheshimiwa Bashungwa is innocent. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi kama Kamati tulimwita Waziri wa Fedha, Waziri wa Fedha alikuja kwenye Kamati yetu na akatueleza changamoto zilizopo zinazopelekea fedha zisiende kwenye ujenzi na kiuhalisia kama Taifa tutafikia wakati vilevile unaweza ukasema hata huyo Waziri wa Fedha unayesema unaweza usimlaumu lakini ni katika kuhakikisha bado kama Taifa tunapigana na tunaendelea kukua kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee naomba niseme kwamba kama Taifa tumekuwa na wakandarasi nchini ambao wakandarasi wetu hao takribani 16,020 ndio ambao wametuwezesha miaka yote kuwa na mtandao huu wa barabara ambao tunao. Wakandarasi hawa nafikiri leo nyinyi wenyewe Waheshimiwa Wabunge mmekuwa mashahidi, mara nyingi mmekuwa mkilaumu kwamba wakandarasi wanafanya kazi kwa fedha nyingi, lakini sababu kubwa hata wewe ukiwa mfanyabiashara lazima faida uiweke kidogo kubwa ukisubiria zile fedha zako muda wote ambao utakuwa hujalipwa. Ile profit margin lazima utaiongeza kidogo. Kwa hiyo, suala la wakandarasi wetu kuwa ghali linasababishwa pia na ukosefu wa fedha zinazotakiwa kulipwa kwenye miradi kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo leo mmekuwa mashahidi mmewatetea wakandarasi kwamba hawalipwi na hatimaye tunazalisha riba kubwa. Vilevile, siyo wakandarasi tu hata wahandisi washauri na wenyewe kadiri mradi unavyoongezeka muda vilevile fedha inaongezeka. Kwa hiyo, hii ni changamoto ya kucheleweshewa miradi kama Taifa ni wakati sahihi namna ya kuangalia tutavyokwenda vizuri na kuweza kujipanga vizuri.

Mheshimiwa Spika, pia niendelee kusema kiuhalisia Mheshimiwa Bashungwa is innocent, hakuna sababu ya kushika shilingi yake ndugu zangu wala hakuna sababu ya kutokupitisha bajeti hii. Wote ni Watanzania na wote ni wananchi lazima tuwe realistic tunafahamu hali halisi, wala Mama Samia na yeye unaweza ukasema vilevile is innocent. Lazima tukubali tumekuwa na miradi mikubwa mingi ambayo imefika wakati lazima imalizike, ni point of no return. Kwa hiyo, tukubaline na uhalisia, tujipange kama Taifa tuweze kusonga mbele. Ukiangalia pia hata aliyeondoka hatuwezi kusema hakuwa sahihi kwa sababu tunafahamu umuhimu wa miundombinu yetu kwa maendeleo ya Taifa letu. Kwa hiyo, ndugu zangu sisi politicians wakati mwingine we have to be realistic kwa manufaa mapana ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba nampongeza kaka yangu Mheshimiwa Mwakibete amezungumza vizuri sana ni wakati sahihi vilevile tuone namna ya kuwa na Benki za Wakandarasi nchini kama vile China Construction Bank zipo, kwa sababu ukiangalia mkandarasi mmoja anaweza akawa na ile annual turnover (ule mzunguko wa mwaka) wa takribani kama bilioni mbili au tatu. Ukichukua hiyo 40% tu ya wakandarasi waliokuwepo wakiwa wanapita kwenye benki fulani moja, maana yake hiyo benki ina uwezo wa kujizungusha vizuri.

Mheshimiwa Spika, kama Taifa tuone namna ya kutengeneza utaratibu huu kwa manufaa mapana, siyo kwa wakandarasi bali kwa Taifa letu, kwa sababu wanaajiri vijana wengi na vijana wengi wanaotoka vyuoni wanapata ajira kupitia wakandarasi. Ni huu umuhimu wa private sector katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia tangu mwaka 2013 – 2023, zaidi ya shilingi trilioni 61.6 zimetumika katika miradi ya ujenzi ndani ya miaka 10 lakini tumekuwa na hizo kilometa za lami tulizokuwa nazo. Kwa hiyo, ni wazi kwamba kupitia sekta ya ujenzi ni sekta ambayo kama Taifa tukiwekeza vizuri tunaweza kupiga hatua kwa sababu mzunguko wake ni mkubwa na bado kama Taifa tunahitaji kupanua miundombinu yetu kwa mustakabali mpana wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Tanzania tumekuwa na shida ya Wahandishi wa Udongo (Geotechnical Engineers) na kwa kuwa Wizara hii ndiyo Wizara Mama ya Wahandisi na Bodi ya Wahandisi iko chini ya Wizara hii, ninaiomba sana Serikali ione namna ya kuhakikisha wanafanya jitihada za maksudi kuhakiksha tunaongeza Wahandisi wa Udongo (Geotechnical Engineers). (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninafikiri utakuwa umeona kule Kigoma barabara ilivyokuwa imekatika na kule Pwani barabara ilivyokuwa imekatika, kama tutakuwa na Geo Technical Engineers wa kutosha nchini lile tatizo mimi nina uhakika lingeweza kuepukika, kwa sababu teknolojia zipo za kuhakikisha tunaboresha layer ya chini ya udongo, ile sub-grade layer ili kuhakikisha wakati wote inakuwa na nguvu inayohitajika kuhakikisha hayatokei matatizo kama yale katika barabara zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona Bagamoyo – Msata ilipojengwa, changamoto kama ile iliwahi kutokea, cracks kwenye barabara zile na ipo nja sahihi ambayo ilitumika kuboresha kuboresha barabara ya Bagamoyo – Msata na mpaka leo tunaiona ipo.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, ninashukuru. Ninamaliza kwa kusema kwamba, tuone haja ya kuhakikisha tunaongeza nguvu, Wahandisi wengi wa Udongo wanatoka nchi za nje, wanaofanya kazi Tanzania, wanalipwa shilingi milioni 10 kwenye miradi, Watanzania tunaweza pia. (Makofi)

SPIKA: Haya ahsante sana.

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo ninaunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)