Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru na mimi kwa kunipatia muda niweze kusema machache kwenye Wizara hii. Mimi ninaomba nianze kwenye ukurasa wa 35, barabara za EPC + F.
Mheshimiwa Spika, kuna barabara ziko nyingi hapa lakini ninaomba niisemee barabara hii ya kutoka Olboroti – Mrijo mpaka Kwamtoro, kuunganisha na Singida. Maelezo ya Mheshimiwa Waziri hapa anatuambia Serikali inaendelea na mazungumzo na wafadhili ili kupata fedha za utekelezaji wa miradi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nimeingia Bungeni hapa mwaka 2015. Bajeti ya kwanza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi niliichangia mwaka 2016. Tangu mwaka 2016 ninachangia bajeti hii, ninauliza maswali ya msingi. Ahadi ni kila leo kwamba barabara hii itajengwa, barabara hii itajengwa. Mwaka jana tukaambiwa barabara hii sasa inakwenda kujengwa kutoka kwenye Serikali Kuu kwenye mapato yetu, tunaenda kupata fedha za kwenda kuijenga hii barabara yote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwaka 2022 walituambia wanaanza kujenga kipande kipande kuanzia Kibirashi. Tukaambiwa safari hii barabara hii inaenda kujengwa yote kwa mfumo wa EPC. Kibaya zaidi mwaka jana tumesaini mikataba kwa ajili ya ujenzi wa hizi Barabara, lakini leo kwenye andiko la Waziri anatuambia kwamba wao bado wako kwenye mchakato. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa mimi ninajiuliza, haya mazungumzo mpaka tunafikia kusaini mikataba, ina maana tulianza kusaini mikataba kabla ya mazungumzo? Ni kweli Serikali tulikuwa hatujui nini tunachokifanya? Kwa sababu mpaka tunafikia hatua ya kusaini, tumeshakubaliana na hawa watu tumejua gharama ni kiasi gani, watafanyaje kazi, kusaini ni kitendo cha mwisho kwamba umesharidhia kila kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa, leo inakuaje Serikali mnarudi kinyumenyume mnatuambia kwamba mko kwenye mazungumzo, tena mapya? Kama hamjengi hizi barabara tuambieni. Wilaya ya Chemba tuna kama 26, ni Kata tatu tu ndiyo zinazopitiwa na lami, Kata 23 hazina lami! Wilaya ile ndiyo inayolima leo, wakulima wake wanasota wanahenya kwa kuuza mazao yao kwa bei ya chini kwa sababu hawana barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo wakinamama wanajifungulia barabarani kwa sababu hawana barabara ya kuwafikisha hospitalini. Watu wanakufa kwenye madaraja, maporomoko huko, mitaro iko ya ajabu kwa sababu hakuna Barabara, watoto wanafia kwenye maji wakivuka vivuko. Mheshimiwa Bashungwa umeenda ukafika na ukatupatia ahadi ukatuambia unapeleka hela kwa ajili ya kujenga lile daraja la Kelema, leo unakuja kutuambia story hapa! Kwani mnatuchukuliaje? Yaani mnatuonaje kwa mfano? Kwamba kuna watu special sana katika Taifa hili na wengine hatustahili kabisa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yaani watu wa Wilaya ya Chemba leo kuanzia mwezi wa 12 mpaka mwezi wa tano wao wanahangaika na maporomoko ya maji, wanakesha barabarani magari yamekwama. Kiangazi hiki leo wanahangaika tena na hii mitaro, ni kupanda na kushuka, rasta za kutosha, wakifika wanasafiri wanakotoka, hata wakija tu hapa Mjini mpaka wakifika hapa wamepauka kama nyani. Ni kwa nini mnatuchukulia sisi watu wa Wilaya ile kwa namna hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Kunti Majala, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Godwin Mollel.
TAARIFA
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ninataka tu kumwambia dada yangu ambaye anachangia vizuri na ninamwelewa sana lakini ninataka kumhakikishia kwamba hakuna mtu mwenye utu na mchapakazi na humble kama Waziri wa Ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwaambie tu, hapa juzi mmetuuliza swali la kipindupindu, the corner stone ya kusababisha ni pamoja na mafuriko, majanga ya El Nino na leo hakuna kipindupindu na magonjwa, ni kwa sababu saa zote Mheshimiwa Bashungwa yuko site na anahakikisha nchi inafunguka. Mimi ninachokuomba tumvumilie, mimi nina hakika hayo unayoyasema yatafanyika kwa aina ya mtu tulienae hapo mbele. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Kunti Majala, unaipokea taarifa hiyo?
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, siipokei taarifa. Wema, u-innocent wake na jina lake ni kwake yeye Mheshimiwa Dkt. Mollel, siyo kwa wananchi wa Wilaya ya Chemba na Mkoa wa Dodoma. Watoto wanaokufa, juzi mvua za mwezi wa pili, kwenye Daraja la Songolo watoto watatu wamesombwa na maji, wewe unaniambia kwamba yeye ni mtu mwema? Ingekuwa ni mtoto wako Mheshimiwa Mollel kafa pale, kwa nini mnachukulia hivi vitu simple kiasi hicho? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yaani ni kwa sababu gani haya mambo yanatendeka kwa watu wengine, kwa nini? Mheshimiwa Waziri umefika umeona na ulishuhudia, wamama wa Wilaya ya Chemba Kata ya Mondo, Kijiji cha Kelemasimba walipiga magoti na kukushika kichwa na kukuvisha ushanga, wakakuomba uwasaidie daraja lile linalowauwa wakina mama na watoto wao wanakwenda shule, mpaka leo hujafanya jambo! Ukija hapa wameniambia wanatamani kusikia, ni lini fedha ulizoziahidi zinakwenda kujenga lile daraja? Lakini wananchi wa Chemba wameniomba nije nikukumbushe kwamba, ulizungumzia pia suala zima la barabara hii ya kutoka Kibirachi, wanataka kujua barabara hii inajengwa ama haijengwi ili wajue. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine, barabara hii pia imewarudisha nyuma wananchi wa Wilaya ya Chemba zaidi ya Kata 13 ambao wanapitiwa na mradi huu. Mliwawekea X leo ni mwaka wa 29 hamjawalipa fidia hamjafanya chochote na mmewazuia kuendeleza maeneo yao. Wako pale kimya hawana chochote wanachokifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wananchi wanaomba kujua leo kupitia sauti yangu, ni lini mnakwenda kuwalipa fidia? Kama hamuwalipi wamesema wanataka tamko la Serikali. Waambieni waendeleze maeneo yao ili waachane na hadithi hizi za kwenda kuwajengea barabara ambayo ni hadithi za abunuwasi. (Makofi)