Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUNIRA MUSTAFA KHATIBU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kupata fursa hii ya kuchangia katika bajeti ya Wizara ya Ujenzi.
Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu kwa kazi kubwa wanayoifanya kwenye Wizara. Nampongeza pia Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya.
Mheshimiwa Spika, katika uchangiaji wangu naomba kujikita katika eneo moja tu ambalo kwa utafiti na ufuatiliaji wangu nimeona kuna changamoto kubwa. Eneo ambalo nataka kuchangia ni kuhusu Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA).
Mheshimiwa Spika, Wakala huyu anakabiliwa na changamoto kadhaa zinazoweza kuathiri ufanisi wake na utoaji wa huduma bora na hapa nimeainisha baadhi ya changamoto kuu ambazo TEMESA inakumbana nazo ambayo ni kama ifuatavyo:-
(i) Upungufu wa rasilimalifedha; TEMESA inakabiliwa na upungufu wa fedha za kuendesha shughuli za kila siku, kufanya matengenezo ya vifaa na kuboresha miundombinu. Hali hii imekuwa ikiathiri utendaji kazi wa taasisi na kuleta malalamiko kwa wadau ambao ni taasisi za Serikali. Ikumbukwe kuwa ukosefu wa bajeti ya kutosha kutoka Serikalini unakwamisha utekelezaji wa miradi mikubwa na muhimu. Hivyo, ninaitaka Wizara kuangalia namna kuongeza fedha katika taasisi hii.
(ii) Vifaa na vitendea kazi vya kisasa; wakala huu pamoja na umuhimu kwa Serikali bado anakabiliwa na ukosefu wa vifaa vya kisasa na vya kutosha kwa ajili ya matengenezo na ufundi. Hali hii kwa ujumla wake inarudisha nyuma ndoto na mipango ya taasisi.
(iii) Rasilimali watu; upungufu wa wataalamu wenye ujuzi na uzoefu unaohitajika kwa huduma bora. Changamoto nyingine inaendelea kuumiza taasisi hii ni ukosefu wa wataalamu wenye ujuzi na maarifa kulingana na mahitaji ya sasa. Hali hii imefanya baadhi matengenezo ya magari na mitambo kuchukua muda mrefu kwa sababu ya kutegemea makampuni binafsi hasa katika utambuzi wa matatizo ya magari na kutatua. Ili taasisi hii iweze kujitegemea na kutekeleza majukumu yake ipasavyo Serikali inapaswa kuhakikisha inaajiri wataalamu ambao wana sifa na uwezo.
(iv) Mikopo na madeni; utafiti niliofanya unaonesha kuwa TEMESA inakumbana na changamoto za kudhibiti mikopo na madeni ambayo inaweza kuathiri uwezo wake wa kujiendesha. TEMESA inadai taasisi za umma kiasi kikubwa cha fedha zilizotokana na matengenezo ya magari na mitambo. Kucheleweshwa kwa fedha hizi kunaathiri mwenendo wa taasisi kutekeleza majukumu yake.
(v) Utaratibu mbovu wa kazi na urasimu unaochelewesha utoaji wa huduma kwa wakati; Wakala anakabiliwa na changamoto ya matumizi ya kisasa ya mifumo ya kiteknolojia katika kufanya kazi zake. Matumizi duni ya teknolojia mpya na za kisasa katika kutoa huduma za ufundi na umeme imefanya kazi nyingi za Wakala kuchukua muda mrefu kukamilika na kuleta malalamiko kwa wadau. Kutokana na hali hiyo, yapo malalamiko juu ya ubora wa huduma zinazotolewa ikiwa ni pamoja na muda wa kukamilisha matengenezo na kiwango cha matengenezo hayo.
(vi) Wakala kukosa mikakati ya kibiashara; taarifa za Wakala zinaonesha wazi kwa namna gani Wakala amekosa mikakati ya kibiashara ili kuhimili ushindani na kuongeza mapato yake. Hali hii imefanya Wakala kujiendesha kwa hasara ikilinganishwa na washindani wake katika soko.
(vii) Miundombinu na mazingira duni ya kazi; Kamati ya Bunge ya Miundombinu imetembelea na kukagua baadhi ya miundombinu ya Wakala na kubainisha mazingira yasiyoridhisha kama vile karakana za matengenezo na ofisi ambayo inaweza kuathiri ubora wa kazi. Aidha, mazingira ya kazi kwa watumishi ni duni kiasi cha kuathiri afya na usalama wa wafanyakazi. Kutokana na chagamoto hizi nashauri hatua zifuatazo kuchukuliwa na Wizara:-
(a) Kuhakikisha bajeti ya kutosha kwa ajili ya shughuli na uwekezaji wa vifaa na teknolojia mpya;
(b) Mafunzo na maendeleo; kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa wafanyakazi na kuboresha mazingira ya kazi;
(c) Ufanisi wa usimamizi; kuimarisha mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji wa utendaji wa wakala; na
(d) Kuboresha mawasiliano na ushirikiano na wadau mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, TEMESA inahitaji mikakati madhubuti na jitihada za pamoja ili kukabiliana na changamoto hizi na kuboresha utoaji wa huduma zake kwa ufanisi zaidi.
Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja hii.