Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa fursa na mimi nichangie. Jambo la kwanza ninaunga mkono hoja ambayo imewekwa mezani. Jambo la pili, ninawapongeza Waheshimiwa Wabunge tunajadili bajeti ya Wizara ya Ujenzi katika kipindi ambacho barabara zimeharibiwa sana na mvua ambazo zimeendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninawapongeza Wabunge kwa kuwa wameitendea haki bajeti hii. Wamewatendea haki Watanzania kwa sababu wamejadili wameonesha uhitaji wa kuzirekebisha barabara hizo, ndiyo maana ninaipenda CCM kwa sababu inaleta viongozi wanaojali masilahi ya Watanzania na hiyo ndiyo sifa kubwa ya Chama hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali tumepokea hoja hizi ambazo Wabunge wamezisema na kwa ajili ya muda sitaenda kwenye hoja nyingi. Moja imeongelewa nyongeza ya bajeti, hata Serikali tunaiona bajeti hiyo na tunauona uhitaji huo. Uhitaji haupo tu kwenye nyongeza ya ukubwa wa bajeti, kuna uhitaji wa bajeti ambayo inahitaji marekebisho tu ya barabara ambazo zimeharibika. Tunalifanyia kazi hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi tunavyoongea tunatarajia tutakapokuja kwenye Bajeti Kuu tutatoa tamko kuhusu bajeti ya dharura mahsusi kuhusu kurejesha barabara zilizoharibika na tulivyokaa na wenzetu wa Wizara ya Ujenzi wametuambia, kwa upande wa ujenzi tu inahitajika takribani shilingi bilioni 700 mpaka shilingi trilioni moja, kwa upande wa barabara za ujenzi, kwa upande wa TARURA zinahitajika takribani shilingi bilioni 300, kwa hiyo uhitaji huu Wizara ya Fedha tumeushapokea na tunaendelea kuongea na wadau wenzetu ili tuweze kupata fedha hizo ambazo zitakuwa mahsusi kwa ajili ya kurejesha miundombinu hii ambayo imeharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, uwekezaji ambao umefanyika kwenye miundombinu hii ni takribani shilingi trilioni 40. Serikali haiwezi ikaacha tu uwekezaji wa aina hiyo ukapotea hivi hivi. Kupoteza miundombinu hii ni kuangusha uchumi, hatuwezi tukaruhusu jambo la aina hiyo. Kwa hiyo, kipengele cha kwanza ambacho tunakifanyia na tutatoa tamko kinahusisha fedha ambazo zinahitaji kurejesha miundombinu iliyoharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni nyongeza ambayo inazingatia chanzo kipya mahsusi. Tunao upande wa mahitaji na tunao upande wa upatikanaji wa fedha. Mmeongelea mahitaji na sisi tunafanyia kazi upande wa upatikanaji wa fedha. Hili nalo tutakuja na chanzo, tutaleta pendekezo, Bunge lako litupitishie pendekezo la chanzo kipya mahsusi ambacho tutaenda kuongeza kwenye bajeti ya Wizara ya Ujenzi. Tunaangalia uwezekano, ikiwezekana kianze kufanya kazi mwaka huu lakini miaka mingine kitumike kama chanzo cha kushughulikia masuala ya dharura. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata mimi ninamwonea huruma Mheshimiwa Waziri mwenzangu Mheshimiwa Bashungwa, anafika site barabara imeharibika wananchi wamekwama, anasema Waziri wa Fedha niletee fedha lakini fedha hizo ambazo zinatakiwa zipatikane kimsingi si za dharura, tunalazimika kukata kutoka maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimwa Spika, sasa hii ambayo imetokea na kwa kuwa imekuwa ikijirudia, itupe funzo kwamba tunahitaji chanzo ambacho kitakuwa kinajilimbikiza wakati wa amani, wakati wa dharura kiweze kutumika kwa ajili ya dharura. Kwa hiyo, hilo la lenyewe ni eneo lingine na tutakuja na pendekezo. Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge, mpitishieni Mheshimiwa Bashungwa bajeti yake lakini tutakuja kujadiliana kwenye bajeti ambayo itakuwa inaongelea vyanzo, tujadiliane vyanzo na mapendekezo mengine yote haya tumeyapokea na tutayajadili kwa upana tutakapokuwa tunajadiliana kuhusu Finance Bill. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ni EPC+ F, tuliongea vizuri kuhusu jambo hili la EPC + F na wala hatujakurupuka. Ni jambo ambalo hata kwenye reli tunafanya, ni hivyo hivyo na kwenye reli. Mkandarasi anakuja, anakuja in pair, anakuja na financier wake, anakuja na mtoa fedha ambaye watafanya naye kazi pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumefanya hivyo kwenye reli, lot ya Kwanza ilikuwa na mkandarasi na mtoa fedha na kwenyewe ilikuwa EPC + F lakini tulipofika hapa, ukianzia Lot 3, Lot 4 na Lot 5, mkandarasi na mtoa fedha ni Standard Chartered pamoja na CCCC.

Mheshimiwa Spika, hata hiyo Lot 3, Lot 4 na Lot 5 alivyoenda sokoni amekutana na tatizo, yule mtafuta fedha ambaye amesaini pamoja na mkandarasi amekutana na tatizo kwenye soko la fedha, yule financier wa mkandarasi amekutana na tatizo. Ndugu zangu ukiambiwa ni EPC + F, ile ‘F’ siyo fedha za familia ni fedha za mabenki, uchumi wa dunia umeyumba, amekutana na shida kule. (Makofi)

Mheshimwia Spika, wanasema kwa nini tumesainiana mkataba, sasa angempata wapi Financier bila yeye kupata kazi kwanza? Ni lazima apate kazi na wanaleta in pair, wamekuja in pair. Tumeangalia financial terms zao ziko sawa. Kwa hiyo, mkandarasi amemleta Standard Chartered Bank, kwamba ndiyo atakaye-mobilize. Jamani, hizi kilometa zaidi ya 2,000 ni kama lot ya reli. Ni fedha nyingi, hizi hazitoki kwenye familia moja, zinatoka kwenye mabenki, tena siyo benki moja ni syndication. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wameenda kule wenzetu yule financier ameenda kwenye dunia ambayo na sisi tunaishi hiyo, amekutana na shida ya fedha. Sasa tunafanyaje? Tumwambie lete za urithi wa Babu yako? Hapana! Atasubiri uchumi utengemae, atafanya syndication halafu ujenzi utaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata sasa tulikwama kwama kwenye reli kwa sababu ya shida hiyo, wakati UVIKO iko juu sana, wakati masuala ya siasa zile za Russia na Ukraine yako juu sana lakini sasa hivi ameanza ku-mobilize resources hizo. Haya ndiyo mambo ya kiuchumi yanavyofanyika na kwa sababu ni soko la dunia limeharibika, siyo sisi tu! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninadhani hawa wenzetu wanaochangia wanatakiwa wamtie moyo Mheshimiwa Rais kwa courage yake kwamba, licha ya msukosuko wa uchumi duniani, alisema miradi iendelee. Nchi zingine kwa ajili ya sababu hiyo hiyo wame-withdraw miradi, wameacha kutekeleza miradi lakini sisi miradi yote imetekelezwa katika kipindi hicho hicho ambacho dunia iko kwenye msukosuko. Tumetekeleza katika kipindi hicho hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Bwawa la Mwalimu Nyerere linakamilika, msukosuko tu ungetosha kusema hatuwezi kutekeleza bwawa kwa sababu soko la dunia la masuala ya kifedha limeharibika lakini Rais akasema hapana, hakuna mradi utakaosimama! (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, dakika moja malizia.

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, kwenye reli hivyo hivyo. Sasa hivi imefika hapa na kule kwingine inaendelea na soko linaenda linafunguka, hata hili la barabara patakapoimarika huo ndiyo taratibu wa EPC + F.

Mheshimiwa Spika, sasa niambieni, kama tumesaini EPC+ F, ndiyo mkataba uliopo na soko limeharibika, ninyi mnashaurije? Kwamba tubadilishe tuende kuchukua kwenye bajeti ya Wizara ya Afya? Mnataka tukachukue kwenye bajeti ya Wizara ya Elimu? Mnataka tukachukue kwenye bajeti ya Wizara ya Maji? Huu siyo utaratibu. Hautakuwa utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wale ambao tumesainiana mikataba kuna siku wanaweza wakatushtaki, wakasema no, tulishaingia mkataba, ninyi mnataka kuchukua fedha kutoka kwenye bajeti ya afya huku tulishaingia mkataba au tulishaweka lining benki. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana.

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninawaomba Waheshimiwa Wabunge ninawaomba, pana mambo ambayo ni ya dharura tunayafanya kwa dharura, pana mambo ambayo ni ya kidunia na sisi tunaishi kwenye dunia hiyo hiyo inabidi tuyaelewe, lakini si nia mbaya ya Serikali kwenye jambo hili, si nia mbaya ya Serikali, Serikali nia yake ni hiyo hiyo njema na tutaendelea kukaa na wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivi sasa hivi nimepokea barua, ninakaa nao wale watu wa Standard Chartered, inawezekana watasema sasa hali inafunguka. Kwa hiyo, tuendelee nalo na tumuunge mkono Mheshimiwa Bashungwa bajeti yake ipite na tutaendelea kupeana taarifa katika mambo haya na yale yote ya madeni tunaendelea kulipa.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, ahsante sana.

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, ana sehemu kwenye bajeti yake na sehemu nyingine iko Mfuko Mkuu wa Serikali, hivyo ndivyo ambavyo huwa tunafanya.

Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja. (Makofi)