Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Karagwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa nyingine ya kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuhitimisha hoja ya Bajeti ya Wizara yetu ya Ujenzi ambayo niliwasilisha jana. Pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kupita salama katika kipindi kigumu cha mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya. Nitumie nafasi hii niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa ushirikiano ambao mlitupa kipindi hiki ambacho kilihitaji subira na ushirikiano. Pia, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge katika majimbo yenu mlitupa ushirikiano mzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa namna ambavyo unaongoza Bunge letu Tukufu kwenye mjadala wa bajeti yetu kuanzia jana tumekuwa pamoja nawe. Pia, nitumie nafasi hii kuwashukuru Wenyeviti, Mheshimiwa Deodatus Mwanyika pamoja na Mheshimiwa Dkt. Joseph Mhagama kwa namna ambavyo walikusaidia katika mjadala ambao umekuwa wa siku mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia kumshukuru sana rafiki yangu, ndugu yangu Mheshimiwa Mhandisi Godfrey Kasekenya - Naibu Waziri wa Ujenzi kwa kazi nzuri ambayo anaifanya ya kunisaidia katika majukumu ambayo Mheshimiwa Rais ameniamini kumsaidia kama Waziri wa Ujenzi pale ambapo ninafanya vizuri ni kwa sababu nina Naibu Waziri ambaye ananipa ushirikiano wa dhati kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru mbele yako pamoja na Waheshimiwa Wabunge wezangu, Mheshimiwa Mhandisi Kasekenya nakushukuru sana na niendelee kuwaomba wananchi wa Jimbo la Ileje wamepata jembe kweli kweli. Mheshimiwa Mhandisi Kasekenya tunamuamini ni mchapakazi na ni mzalendo; nawaomba wananchi wa Jimbo la Ileje waendelee kukulea na kukutunza na mwakani wakurejeshe hapa Bungeni ili kazi iendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile nimshukuru kaka yangu Mheshimiwa Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwa ufafanuzi mzuri ambao amenisaidia kutoa kwenye hoja hii. Mheshimiwa kaka yangu Mheshimiwa Waziri wa Fedha nakushukuru sana.
Mheshimiwa Spika, vilevile, niwashukuru wasaidizi wetu ndani ya Wizara. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri Kasekenya lakini niendelee kumshukuru Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Wakurugenzi wa Idara, Wakuu wa Taasisi na Watumishi wote ndani ya Wizara na taasisi zake kwa namna ambavyo wanaendelea kuchapa kazi ili kutusaidia kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kusimamia Dira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ndani ya Wizara ya Ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwashukuru pia Waheshimiwa Wabunge wenzangu. Wale ambao mmechangia kwa kuzungumza mlikuwa 77 na wale ambao mmechangia kwa maandishi mlikuwa wa nne kwa hiyo jumla hoja yetu imechangiwa na Wabunge 81. Naomba nitumie nafasi hii kuwashukuru sana, hata wale ambao hamjapata nafasi ya kuchangia tunawashukuru kwa ushirikiano wenu, ahsanteni sana Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia niishukuru sana Kamati ya Kudumu ya Bunge letu ya Miundombinu inayoongozwa na kaka yangu Mheshimiwa Selemani Kakoso, akisaidiwa na Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti mama yetu Mama Anne Kilango Malecela na Wajumbe wa Kamati kwa ushirikiano mkubwa sana ambao wanatupatia Wizara ya Ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninyi ndio think tank ya Wizara yetu, mnatushauri vizuri, mnatuelekeza vizuri, tunashirikiana vizuri, tunawashukuru sana na tunawahidi tutaendelea kuwapa ushirikiano. Maoni na ushauri wa Kamati ambao mmetupatia tunakwenda kuutekeleza. Ahsanteni sana Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati pamoja na Wajumbe wote wa Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi niungane na Waheshimiwa Wabunge ambao wamepata fursa ya kuchangia na kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anafanya kazi kubwa. Hata kipindi kigumu cha mvua za El-Nino na Kimbunga cha Hidaya. Mheshimiwa Rais na sisi Wizara ya Ujenzi tuendelee kushukuru kwa kuwekeza na kuwezesha Taasisi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa kuwa ya kisasa, kwa sababu uwezo wa taasisi hii umetuepushia madhara makubwa ambayo yangetokea kwa mvua hizi kubwa ambazo tumezipa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Taasisi hii ya Mamlaka ya Hali ya Hewa imeweza kuwa inatoa utabiri sahihi na kutusaidia kuchukua tahadhari. Kwa hiyo, tunaendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa uwekezaji huu kwa Mamlaka ya Hali ya Hewa. Tunamshukuru pia kwa shilingi bilioni 72 ambazo alituwezesha ili kuweza kuwanusuru Watanzania pale miundombinu ilipoharibika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa hiki ambacho Mheshimiwa Waziri wa Fedha amekisema. Mheshimiwa Rais aliagiza Wizara ya Fedha wakae na sisi tubainishe mahitaji ya kurudisha barabara ambazo zimeharibika baada ya mvua kwisha. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha nimeona ametupa habari njema. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelee kuwatoa wasiwasi Waheshimiwa Wabunge, tulipopata madhara ya Covid hakuna aliyejua kwamba Serikali hii bunifu yenye Mheshimiwa Rais mwenye vision tungepata shilingi trilioni 1.2 za IMF. Kipindi hicho tofauti na nchi nyingine ambazo zilitumia mabilioni ya pesa kwenye kununua vitakasa mikono na barakoa, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa dira yake aliona fedha hizi tuzitumie kwa kujenga miundombinu ambayo inadumu kizazi hiki na vizazi vijavyo na akaelekeza tujenge shule za msingi, sekondari, vituo vya afya na tununue vifaa tiba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hizi fedha za dharura ambazo Mheshimiwa Rais ameelekeza Wizara ya Fedha watafute fungu, sisi tumewasilisha shilingi trilioni moja ya kurudisha miundombinu, Mheshimiwa Waziri wa Fedha amesema hapa. Sisi tumejipanga kwamba fedha hizi tutakazozipata hatutakwenda kukwangua barabara na kuziba mashimo, kwa sababu baada ya mwaka mmoja, miaka miwili ukiuliza mabilioni haya ambayo tutapata yametumika wapi? Itakuwa ni ngumu ku-point mahali ambapo fedha hizi zimetumika.
Mheshimiwa Spika, tunakwenda kurudisha madaraja na makalavati katika maeneo ambayo yamekatika ili hata mwakani Mwenyezi Mungu azuie, ikitokea tumepata mvua kubwa tunakwama, kwa sababu mvua ikisomba daraja huwezi ukalirudisha ndani ya wiki moja wala ndani ya mwezi. Kwa hiyo, fedha hizi ambazo Wizara ya Fedha inaziandaa kwa ajili ya kurudisha miundombinu ambayo imeharibilka Wizara ya Ujenzi tumejipanga kuhakikisha tunazipeleka kwenye kujenga madaraja na makalavati na itakuwa ni nchi nzima kulingana na uharibifu ulivyotokea.
Kwa hiyo, tunamshukuru Mheshimiwa Rais, sisi kile ambacho Mheshimiwa Waziri wa Fedha amekisema tayari tumeanza kujiandaa kwa ajili ya fedha ikipatikana na kiangazi kinapoingia basi tuingie katika kurudisha miundombinu ambayo imeharibika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitakwenda kujibu hoja za jumla, lakini nimeona, Waheshimiwa Wabunge tunaomba mtupitishie bajeti hii kwa sababu tunazo barabara ambazo zipo juu ya 70% katika utekelezaji, haziwezi zikaishia njiani. Hii hii hela ambayo tumewezeshwa tunaomba mtupitishie ili tukaweze kukamilisha barabara 12 ambazo utekelezaji upo juu ya 70%. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, barabara ya Noranga – Itigi – Mlongoji kilometa 25 ipo 72%, Ruangwa – Nanganga kilometa 50 ipo 76%, Tanga - Pangani kilometa 50 ipo 72%, Kidatu – Ifakara kilometa 66.9 ipo 88%, Itigi – Township Road kilometa 10 ipo 98%, Kanyani Junction – Mvugwe, kilometa 70.5 ipo 78% na Mvungwe – Nduta Junction kilometa 59 ipo 73%, Nduta Junction – Kibondo Junction – Kabingo kilometa 62.5 ipo 97%, Lot I Nala – Veyula – Mtumba – Ihumwa Dry Port kilometa 52.3 ipo 71%, Muheza – Amani kilometa nne ipo 98%, BRT I Improvement kilometa 20.3 ipo 99% na BRT II ipo 99%. Kipande cha bajeti ni kwenda kukamilisha hii miradi 12 ambayo ipo juu ya 70% kwenye utekelezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna JP Magufuli Bridge lipo 89%, tunahitaji sehemu ya bajeti hii tukakamilishe daraja hili ili Disemba kama tulivyowaahidi Watanzania tuweze kulikamilisha daraja hili. (Makofi))
Mheshimiwa Spika, tuna viwanja wa ndege; Kiwanja cha Ndege cha Iringa kipo 86%. Miradi ambayo ipo kwenye utekelezaji chini ya 70% inabidi tuitoe ilipo tuipeleke kwenye kuikamilisha 100%. Tuna barabara Ntendo – Muse – Kilyamatundu sehemu ya Tendo – Kizungu kilometa 25 ipo 44%, kuna barabara ya Matai – Kasesya Road, Lot I, Matai - Tatanda kilometa 25 ipo 34% na kuna barabara ya Isonje - Makete Road sehemu ya Kitulo – Iniho kilometa 36.3 ipo 4.2%, kuna barabara ya Itoni – Lusitu kilometa 50 ipo 22%, kuna barabara ya Mogabiri – Nyamongo kilometa 25 ipo 41%, kuna barabara ya Uvinza-Malagarasi kilometa 51.1 ipo 51%, kuna barabara ya Kumnazi – Kasuro – Bugene – Kyaka – Mtukula (Lot II), Bugene – Burigi – Chato kilometa 60 ipo 31%.
Mheshimiwa Spika, kuna barabara ya Mnivata – Mnitesa kilometa 100 tupo kwenye maandalizi ya ujenzi, kuna barabara ya Mitesa – Masasi kilometa 60 tupo kwenye maandalizi ya ujenzi, kuna barabara ya Tamko – Mapiga kilometa 13.59 tupo kwenye maandalizi ya ujenzi kuna barabara ya Iringa – Ipogolo – Kilolo kilometa 33.61, Mheshimiwa Nyamoga nimekusikia, tumeanza maandalizi ya barabara hii, Kagera Sugar Junction – Kakunyi kilometa 25 tupo kwenye maandalizi ya ujenzi, Tarime – Mogabiri kilometa 61, tupo kwenye maandalizi ya ujenzi Sabasaba – Sepuka – Ndago kilometa 77.4 tupo kwenye maandalizi ya ujenzi, Amani – Makoro – Luanda kilometa 35 utekelezaji tupo 25%, Mheshimiwa Benaya nimekusikia, tutakuja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumechukua hatua mkandarasi huyu ameharibu mahali pengine, barabara ambazo alikuwa ameshasaini tumemnyang’anya tumewapa wakandarasi wengine ambao wanaweza wakafanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Barabara ya Tungamaa – Mkange kilometa 95.2 tupo 31.3%, barabara ya Mianzini – Ngaramtoni kilometa 18 tupo 42%, barabara ya Ifakara – Mbingu kilometa 62.5 maandalizi ya ujenzi (advance payment), Mheshimiwia Kunambi nimekusikia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, barabara ya Mbulu – Garbabi kilometa 25 tupo 28%, maandalizi ya kujenga barabara ya Labay – Haydom kilometa 25 tupo kwenye maandalizi, Lusahunga – Rusumo kilometa 92 tupo asilimia tano, Utete – Nyawage kilometa 33.7 tupo asilimia mbili, Kasulu – Manyovu na Kasulu town links kilometa 68.67 tupo 63%, Ihumwa Dry Port – Matumburu – Nala kilometa 60 tupo 60%, Kikombo Junction – Chochoro – Mapinduzi – Ntyuka Junction – Mvumi – Makulu kilometa 25 tupo 47%, Sanzate – Nata kilometa 40 tupo 44%, Vikonge – Luhafe kilometa 25 tupo 57% na Luhafe – Mishamo kilometa 37 tupo kwenye maandalizi ya kuanza ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Kibaoni – Mlele kilometa 50 tupo 14%, Nduta Junction – Kibondo Town – Kibondo Junction kilometa 25.9 tupo 63%, Kibondo – Bambamba kilometa 47.9 tupo 10%, Itigi – Mkiwa kilometa 31.6 tupo asilimia mbili, Handeni – Mafuleta kilometa 20 tupo 41%, Iringa By Pass kilometa 7.3, inakwenda kwa awamu lakini tumeanza, Uyole – Ifisi kilometa 29 tupo 12.5%, kwa Mheshimiwa Spika, lakini tunakwenda kuongeza kasi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, BRT III kilometa 23.3 tupo 26.5%, BRT IV kilometa 30 maandalizi ya ujenzi kuanza.
Mheshimiwa Spika, kuna Sengerema – Nyehunge kilometa 54.5, mkandarasi yule ambaye ameshindwa kwa kina Mheshimiwa Kinanasi tumefuata hatua za kimkataba, tumemnyang’anya barabara hii. Tumeweka mkandarasi ambaye atakwenda kufanya kazi na kule Sengerema – Nyehunge vivyo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, rehabilitation ya Ibanda – Kajunjumele, Kajunjumele – Kiwira Port na rehabilitation ya Kajunjumele – Itungi Port kilometa 32 kwa asilimia mbili, Kizota – Zuzu – SGR kilometa 14 tupo 25%, Maneromango – Kisarawe kilometa 3.1 tupo 30%, Goba – Matosa – Temboni kilometa tatu, tunaanza maandalizi ya ujenzi, Kimara – Bonyokwa – Kinyerezi kilometa 3.7 tunaanza maandalizi ya ujenzi, Chanika – Mbande kilometa 3.8 tupo 55% hatua hiyo, Morogoro – Bigwa – Mvuha kilometa 78, tunaanza maandalizi ya kujenga, Nachingwea – Ruangwa kilometa 57.6, tunaanza maandalizi ya ujenzi, Kibada – Mwasonga kule Kigamboni kilometa 26.7 tunaanza maandalizi ya ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Ubena Zomozi – Ngerengere kilometa 11.6 tunanza maandalizi ya ujenzi, Luanda - Ndumbi Port kilometa 50 tunaanza maandalizi ya ujenzi, Mbingu – Chita kilometa 37.5 tunaanza maandalizi ya ujenzi, Kizengi Weight Bridge Tabora kule Nyahua Chaya maandalizi ya ujenzi wa daraja na Kogwa Junction – Nghambi – Mpwapwa kilometa 32 tunaanza maandalizi ya ujenzi. Kagwila – Kasekese kilometa 54 tunaanza maandalizi ya ujenzi, Kasekese – Ikola kilometa 56.9 tunaanza maandalizi ya ujenzi, Ndungu – Mkomazi kilometa 36 tunaanza maandalizi ya ujenzi, Isongole Two - Ndembo kilometa 46.5 tunaanza maandalizi ya ujenzi. Katumba – Lupaso kilometa 35.3 tunaanza maandalizi ya ujenzi, Mbaka – Kibanja kilometa 20.7 tunaanza maandalizi ya ujenzi, Kyerwa – Murushaka kilometa 50 tunaanza maandalizi ya ujenzi Ntyuka – Mvumi Hospital – Kikombo kilometa 53 tunaanza maandalizi ya ujenzi, Kahama – Bulyanhulu – Kakola kilometa 73 tunaanza maandalizi ya ujenzi na Tatanda – Kasesya kilometa 25 tunanaza maandalizi ya ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, hizi ni barabara ambazo zipo katika hatua mbalimbali utekelezaji wake upo chini ya 70%, lakini kipande cha bajeti hii ni kwenda kuendelea na kazi. Tunaomba mtu-support Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa madaraja, Daraja la Pangani – Tanga tupo 23%, Mbambe – Pwani tupo 15%, Simiyu – Mwanza tupo 15%, Lowa – Mpiji (Dar es Salaam) tupo asilimia mbili na mkandarasi huyu ameshindwa kazi kwa hiyo tunafuta hatua za kimkataba kumuondoa tumuweke mkandarasi mwingine. Daraja hili kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi mto umepanuka, hivyo nimeelekeza tufanye usanifu mpya ili mkandarasi tutakayempata atujengee daraja ambalo litakuwa na kizazi hiki na vizazi vijavyo. Mheshimiwa Subira Mgalu nimekusikia, kile kipande cha kwenda Mapinga tutafanya utaratibu ili kije TANROADS ili barabara hiyo yote iweze kuhudumiwa na TANROADS. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, barabara nyingine ambazo zinaingiliana, unakuta kipande hiki kipo TARURA na kipande kingine kipo TANROADS, Mheshimiwia Waziri Mchengerwa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha kaka yangu tumekubaliana, tumeunda timu ipitie barabara hizo tuangalie ni barabara zipi ziwe za TARURA na barabara zipi ziwe za TANROADS kulinga na uhalisia na uhitaji, tunafanya hilo kwa nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna Daraja la Milumba kule Katavi tunaanza maandalizi ya ujenzi, Kibakwe hapa Dodoma tunaanza maandalizi ya ujenzi, Kelema Maziwa Dodoma tunaanza maandalizi ya ujenzi na Sukuma kule Mwanza tunaanza maandalizi ya ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunavyo viwanja vya ndege ambavyo vipo katika hatua za ujenzi chini ya 70%; Msalato Airport, Musoma, Tabora, Shinyanga, Sumbawanga na Kigoma. Vilevile tuna miradi iliyosainiwa ambayo inahitaji malipo ya awali (advance payment) Mheshimiwa Waziri wa Fedha amesema hapa, lakini kuna vifungu vimeshikilia ili advance tutakavyoipata kupitia bajeti hii ambayo tunaomba tukatekeleza miradi ya barabara 26 ambazo tayari tumesaini.
Mheshimiwa Spika, muda ungekuwa unatosha ningezisema barabara hizi ili kila mmoja wenu aone kazi kubwa ambayo Waheshimiwa Wabunge mmefanya katika kufuatilia barabara hizi zikafanyiwa upembuzi yakinifu, usanifu wa kina zikaingia kwenye manunuzi mpaka hatua za kusainiwa. Ni hatua kubwa ninaomba niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge kwa kazi nzuri ambayo mnaifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa barabara ni hatua na miaka yote barabara hatujazijenga kwa wakati mmoja…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa Waziri dakika tatu malizia. Muda wetu umekwenda.
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, zipo barabara ambazo mmepambana zimefika hatua tumemaliza upembuzi yakinifu, tumefanya usanifu wa kina na sasa zipo kwenye hatua ya kuingia kwenye manunuzi. Kadiri tunavyopata fedha kila mwaka wa fedha, kile kinachopatikana wakandarasi wanajenga katika awamu tofauti. Huyu ana-raise certificate, huyu anasaini. Hivyo hivyo TRA wanakusanya na Serikali inaongea na wafadhili wa maendeleo. Mtandao wote wa barabara za TANROADS ambao tumeujenga, tumeujenga kwa utaratibu huu. Kwa hiyo, niwaombe mtuamini na ninawashukuru kwa pongezi.
Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa kupambana katika kusimamia ujenzi ninaona mna imani na sisi. Kwenye suala la upatikanaji wa fedha Wizara ya Ujenzi, niwape mfano, Road Fund kwa mwaka inapokea takribani trilioni moja, lakini cash flow hiyo tunaongea na Wizara ya Fedha na Wizara ya Mipango, ukichukua hela hiyo kwa wakati mmoja labda hela ya miaka mitano hizo ni kama trilioni tano.
Mheshimiwa Spika, kuna benki, Wizara ya Fedha na Wizara ya Mipango wakiridhia tutaangalia namna ambavyo tunaweza tukapata hiyo future cash flow ya Road Fund tukaipata sasa hivi. Tukajenga barabara kwa wakati mmoja, halafu kwa vile TRA ikikusanya hela ipo kwa mujibu wa sheria inaenda kwenye Road Fund, basi hiyo hela, kama ni infrastructure bond inakuwa inatumika hiyo ambayo inakusanywa kila mwaka kwenda kuhudumia ile bond ambayo tayari tuliipa future cash flow, tukapata lump sum moja, tutajenga barabara zetu zika-support uchumi, tukatekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, haya yote Waheshimiwa Wabunge Wizara ya Ujenzi, tumepeleka proposal yetu Wizara ya Fedha, Wizara ya Uwekezaji na Mipango. Kwa hiyo, mtuamini tuendelee na hatua hizi ambazo tumewaletea huku mengine tuliendelea kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Spika ninakushukuru kwa kunipa nafasi na ninaomba sasa nitoe hoja. (Makofi)
SPIKA: Hela tunachukua hizi zilizopo kwenye kitabu. Toa hoja Mheshimiwa, sema natoa hoja.
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)