Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa na mimi fursa niseme maneno yangu machache kuhusu ajenda hii iliyopo mezani kwetu hapa. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan, ambaye kusema kweli kwa kipindi kifupi hiki cha uongozi wake tumeona akiboresha maeneo mengi sana ya huduma, kuboresha miundombinu, kuboresha kila eneo ambalo tunawapata wananchi wetu wakimhitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeona hata michango ya Wabunge humu ndani kila Mbunge anayesimama anasema jambo fulani limefanyika kwenye eneo lake, haya ni maono ya Mheshimiwa Rais wetu na tunahitaji kuendelea kumpa moyo na kumwombea ili aendelee kututumikia wananchi wenzake wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa sijatenda haki kama sijawapongeza pia Waheshimiwa Mawaziri, Mheshimiwa Mwigulu pamoja na Profesa Kitila kwa taarifa zao nzuri ambazo wameziwasilisha na hivyo na mimi niweke mchango wangu mahususi kwenye hotuba zao hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia maeneo manne kwa haraka haraka kwa ufupi. Nataka nizungumzie kilimo, mifugo, viwanda pamoja na miundombinu ya usafiri na usafirishaji. Ninapokwenda kuzungumza maeneo haya hasa kwenye maeneo haya ya sekta za uzalishaji ambayo ni kilimo, mifugo iweze ku-link na viwanda kwa maana ya kwenda kusindika, tuzalishe kwa wingi ili tuweze kwenda kusindika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la kilimo ninampongeza sana Mheshimiwa Rais pamoja na Waziri Bashe kwa kuweka kipaumbele na kuongeza bajeti kwenye eneo hili la kilimo. Kule kwangu ameniletea mradi mkubwa sana wa umwagiliaji pale Msange na ninataka kusisitiza hapa kwamba kipindi hiki ili tuweze kuukomboa uchumi wetu, tuondokane na uchumi huu tunaosema unaochechemea tuweze kuusogeza uende huko kwenye uchumi ambao ni endelevu, lazima tuwekeze kwenye hizi sekta za uzalishaji hasa kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema tunaenda kuwekeza kwenye kilimo lazima tuondoke kwenye kile kilimo cha kizamani, kilimo cha kutumia jembe la mkono. Kwa mazingira hayo lazima tuwekeze sana kwenye zana za kilimo zile zinazotusaidia kulima kwa maana ya matrekta, teknolojia lakini pia na miundombinu yenyewe kwa maana ya umwagiliaji pia lazima tuwekeze kwenye tafiti, hatuwezi kujikomboa hapa kama hatujawekeza kwenye utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kwenye utafiti tuna taasisi zetu zinazofanya utafiti. Kuna hii taasisi ya CAMARTEC na kuna TEMDO mbazo ni mahsusi kwa ajili ya utafiti, lakini hizi taasisi hazijawezeshwa, zenyewe zipo kwa ajili ya utafiti kwenye zana za kilimo, lakini hazina nyezo, hazina fedha. Zitengewe bajeti ya kutosha ili sasa ziweze kufanya kazi ya kutuletea mbinu bora za namna gani tunaenda kulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la mbegu, hatuwezi kulima. Msingi hasa wa kilimo ni mbegu, unapokwenda shambani msingi namba moja ni mbegu. Ukikosea tu kwenye mbegu ina maana mwaka mzima umepotea na resource zote unaweza kwenda kuziwekeza kwenye kilimo zimepotea. Sasa ni muhimu sana, tunapoongeza kwa kiwango fulani kuna juhudi fulani zimefanyika lakini bado tupo nyuma mno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitolea mfano Singida tunalima sana alizeti na hapo mwanzo kulikuwa kuna juhudi za kuhakikisha kilimo cha alizeti kinakuwa ni zao la kimkakati la kitaifa kwa ajili ya kuzalisha mafuta, lakini mbegu tulizozipata hazijatusaidia. Wakulima wetu wanahitaji hybrid seeds ambazo zinatoa mafuta mengi angalau gunia moja lenye kilo 60/70 litoe dumu moja na ziada. Sasa hivi hata hilo gunia moja haliwezi kutoa hata galoni tatu. Pia hapo hekta moja haiwezi kutoa hata gunia kumi. Kwa hiyo, tunampotezea mkulima muda, anaenda anafanya kazi kubwa lakini hakuna anachovuna. Kwa hiyo, ninasisitiza hapa ni lazima tuhakikishe tunatazama eneo la mbegu bora za kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la teknolojia pia nimesema tafiti lakini lazima tu-link na teknolojia yetu. Teknolojia yetu tunatumia bado duni mno, tuondoke huko. Ni lazima tuweke kipaumbele kwenye teknolojia yetu, tuondoke kwenye kile kilimo cha kutumia zana za zamani za kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia pia eneo la ugani. Ni kweli tumewekeza sana hapa na ninampongeza Mheshimiwa Rais. Maafisa Ugani tumewapa vitendea kazi kwa maana ya pikipiki, vile vifaa vya kupima udongo vya kutosha lakini hapa bado tunahitaji kuwasimamia na kulisimamia eneo hili ipasavyo. Mheshimiwa Waziri Bashe kama yupo hapa ndani ninamwomba awekeze sana kwenye usimamizi. Hizi rasilimali zilizopelekwa huko zitumike ipasavyo ili zimfae mkulima, kwa sababu zile zimepelekwa kwa ajili ya kumsaidia mkulima. Kwa hiyo, zisimamiwe ili ziweze kuleta tija ambayo ilikuwa inakusudiwa na iliyokuwa inatarajiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo pia kuna eneo la masoko, tutazalisha, lakini bila kuwa na masoko imara ili mkulima wetu aweze kuona tija ya kilimo, alime auze bei nzuri, alime alizeti aone bei yake nzuri anayoenda kuuza.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kengele nyingi hapo! Nikienda kwenye eneo la mifugo…
MWENYEKITI: Mheshimiwa kengele ya pili.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, aah! Basi kwenye eneo la miundombinu nisisitize hizi Barabara, trunk roads, pia na zile zinazounganisha Mikoa na Wilaya. Sisi kule tuna barabara ile ya kutoka Singida - Ilongero kwenda Haydom hii barabara inakwenda inaunganisha Mkoa wa Manyara, Mkoa wa Simiyu na Mara, mtu hatahitaji kwenda Mwanza, atakatiza.
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante, kaa chini.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa fursa. (Makofi/Kicheko)