Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbogwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi mchana wa leo ili niweze kuchangia hoja iliyoko mezani, Mpango wa Mwaka 2025/2026. Awali ya yote nipende kumshukuru Mungu muumba wa mbingu na nchi kwa kuweza kupata fursa na nafasi hii ya kuweza kuishauri Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nikupongeze Mheshimiwa Waziri kwa huu Mpango uliouleta hapa Bungeni tuujadili, lakini yapo maeneo tunapenda tuishauri Serikali. Kwa kuwa sisi Wabunge tunaishi na watu na tunajua maisha ya watu jinsi wanavyopata taabu na ninaomba unisikilize sana hapa Mheshimiwa Waziri. Unaweza ukatupeleka sana kwenye mipango ya juu sana ukaacha yale maisha yetu ya kiuhalisia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza lipo suala la maboma hapa nchini. Nikizungumzia maboma tunaweza tukasema kila Mbunge ana kilio huko kijijini. Kwa hiyo, kwenye huu mpango ninaomba hili suala lipewe kipaumbele ili nguvu za wananchi walizozifanya zikaweze kuokoka au wanufaike na rasilimali zao ambazo wao wenyewe walichanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la miundombinu; Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ninakumbuka mwaka 2022/2023 tulizungumza hapa Bungeni na wewe ukanikubalia kwamba nilete mpango wangu na nikaleta. Niliandika barua kwa kuomba kwamba kila halmashauri tuweze kununua vifaa vya ujenzi. Hii shida mpaka sasa hivi inatusumbua sana majimboni. Tunajua tumepitisha trilioni kwa ajili ya ujenzi wa Barabara, lakini haviji kwa wakati muafaka. Tukiangalia sasa hivi huu ni mwezi Novemba, tunaelekea mwezi Desemba kwenye masika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tungekuwa na vifaa kila halmashauri au kila mkoa kama tulivyoshauri kwenye Sekta ya Maji tusingekuwa tunasubiriana. Sasa hivi mifumo ni mingi ya kisomi na kitapeli wala NeST haitoki, pesa hazitoki wakandarasi hawalipwi. Kwa hiyo tunakwama tunakuwa na mambo mengi lakini utekelezaji ni hewa. Kwa hiyo, ninaomba kwa mpango huu mwaka 2025/2026, Mheshimiwa Waziri unikubalie, nitaleta tena mpango wangu wa kutaka kununua vifaa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hasa kwenye jimbo langu kwa sababu tukiwa na vifaa halafu sisi wenyewe ni mafundi wa kutengeneza hivyo vifaa hakuna shida ya kuweza kutengeneza miundombinu yetu sisi wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, wakandarasi wanaofanya kazi hasa wa ndani simu na meseji ni nyingi sana kwa kila Mbunge. Wamefanya kazi na bado wanaidai Serikali, ili sasa Serikali iweze kusifiwa na kupewa sifa za kweli ni vyema wakandarasi wa ndani waweze kulipwa kazi walizozifanya hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la ajira, nchi yetu imebahatika kuwa na wasomi wengi sana. Mheshimiwa Waziri, nimeangalia kwenye mpango wako sijaona dhamira kubwa ya kuweza kuwasaidia wasomi ambao wamesoma wana vyeti, wameshaweka vyeti vyao ndani na kila ajira mkitangaza, kila nafasi zikitoka wana-apply lakini mwisho wa siku wanafanya interview hawaajiriwi. Kwa hiyo, kwenye huu Mpango ninaomba mjaribu kulipa kipaumbele hili suala ili kusudi watu waweze kuajiriwa kwa sababu walitumia pesa nyingi kuweza kusomesha watoto wao pamoja na mambo mengine na wengine walifilisika kabisa wakiwa wanasomesha shule za international na mpaka sasa watoto wao hawana ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la watu waliyoitumikia Serikali, mafao. Tunao wanajeshi, tunao wazazi wetu ambao wameitumikia Serikali ila hawalipwi mafao yao kwa wakati. Ninaomba kupitia mpango huu hao watu wakaweze kupewa kipaumbele. Wengine wapo wamemaliza wana miaka miwili, mitatu, mitano, wengine miaka kumi lakini hawajalipwa. Kila siku wanaambiwa nenda ukalete vielelezo hivi, uliajiriwa lini? Ulizaliwa wapi? Maswali yanakuwa mengi mwishowe wanaona Serikali kama vile imewatelekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ushauri wangu mwingine hapa, ninapenda niishauri sana Serikali yangu ya Awamu ya Sita. Kwa kuwa sisi ni washauri wakuu wa Serikali, hasa tunapopata nafasi kusimama hapa Bungeni, Waheshimiwa Mawaziri pamoja na wataalam wote ambao wanahusika kutusikiliza kama Wabunge, watusikilize, ipo shida ambayo hata mwaka jana ilinipata kwenye jimbo langu. Mvua zilinyesha nyumba zikaanguka, wapo walioporomokewa na nyumba, hata juzi hali hii imetokea Jimboni kwangu kule Masumbwe, watu wameumizwa na majumba, lakini kwenye bajeti zetu huwa tunapitisha bajeti ya maafa na huo Mfuko huwa unakaa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, lakini ukweli ni kwamba hao watu huwa hawapati huduma kwa wakati muafaka. Ninaiomba Serikali iweze kuangalia fungu hilo ili waathirika wa mafuriko wanapopata mafuriko, pale mafuriko tu yanapotokea Serikali iweze kuwasaidia watu hawa ili waweze kunufaika na Mfuko huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninapenda nishauri hapa kwa siku ya leo, ni suala la askari wetu ambao wanatulinda kila mji hawana nyumba za kuishi kabisa, lakini hata ofisi sisi kama wananchi tunajitahidi kuwawekea makao ili waweze kuendelea kufanya kazi zao za kipolisi. Kwenye Mpango huu wa 2025/2026 ninaomba hili suala na lenyewe liweze kupewa kipaumbele ili askari hawa nao waweze kufanya kazi kwa morali na mambo mengine ili yaweze kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo sula lingine la hii mitandao ya mawasiliano. Kwenye Jimbo langu nina uhitaji wa mitandao mitano. Zipo kata ambazo hazina mawasiliano kabisa, wananchi wangu wanateseka sana. Ninaomba Serikali iweze kuliangalia, Waziri wa Mawasiliano uweze kulipa kipaumbele na uweze kuboresha kwenye eneo hilo kwa upande wa mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye huu ulimwengu huu wa kidigiti, tunapoteza pesa nyingi kwenye hizi electronic machine, hata juzi tumeona hapa wakati tunapitia Ripoti za CAG, vitu vingi vinapotelea kwenye POS na hili suala ni vyema tukawa tunaenda upande upande huku tunatumia manual huku tunatumia electronic ili kuhakikisha fedha zinazokusanywa na Serikali kuanzia kwa yule mwananchi wa kawaida awe anafahamu kwamba amekusanya shilingi ngapi na zimeenda kufanya nini. Ni vyema kila mwananchi akawa na uelewa na mambo haya kuliko kuambizana tu mifumo ya kifedha imebadilika halafu fedha haziji. Wakati mwingine wananchi wanachangia michango yao kwa ajili ya ku-support Serikali, lakini pale zinapoingia kwenye akaunti hapo ndiyo mifumo inaanza ku-scratch na kuleta matatizo makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala linatunyima heshima na sisi kama wawakilishi wa wananchi kwa kweli linatupa taabu sana na hatupendi yaje yatutokee yale yaliyotokea Kenya kwa sababu ilifika sehemu Wakenya wakaona Bunge lao haliwasaidii wakaamua kabisa kufanya fujo na kuwafanyia vurugu Wabunge wao. Sasa sisi hatupendi hili suala liweze kuja hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, ninapenda niwashukuru tena wananchi wangu wote kwa kuendelea kuniamini na ninasema nitakuwa ninasimama kama Balozi wao ama kama Mwanasheria wao mkubwa na niwatoe wasiwasi hakuna jambo litaharibika. Kulingana na hali hii ni mwaka wa nne nipo hapa nitazidi kufanya kazi kwa hali na mali kwa sababu nimeshayazoea sasa maisha ya hapa, suti zinanienea vizuri na kazi tunafanya na Serikali wananielewa pale ninapowaomba wananisaidia. Kwa hiyo, wazidi kunipa ushirikiano na tuweze kulisongesha Taifa letu kuhakikisha tunatoka hapa tulipo tunaenda sehemu nyingine nchi ya ahadi ambayo tuliahidiwa na Mwenyezi Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine tunalotaka tuliombe hapa kwenye upande wa maendeleo ya Taifa letu kwenye huu Mpango, nimwombe Mheshimiwa Waziri, …
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante! Mheshimiwa.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, mengine nitaleta kwa maandishi. Ahsante sana. (Makofi)