Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Zainabu Mussa Bakar

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na kuniwezesha kutoa mchango wangu kwa njia ya maandishi. Hivyo, naanza kutoa mchango wangu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wananchi haturidhishwi na mwenendo wa utolewaji wa fedha za bajeti zinazoidhinishwa kwa ajili ya utekelezaji wa REA. Takwimu zinaonyesha kwamba, katika miaka mitatu ya fedha iliyopita 2013/2014 hadi Aprili, 2015/2016, wastani wa REA umekuwa kwa asilimia 60 tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, wananchi hawaridhishwi na uwekezaji wa vinasaba katika mafuta. Ili hali, TRA wana vituo njiani vya ukaguaji wa mafuta ni kupoteza pesa za walipa kodi wa Tanzania, ni kuwanyanyasa walipa kodi na kutajirisha mtu binafsi anayetengeneza vinasaba. Hivyo, Waziri atueleze ni kwa nini wanaona tabu kuondosha vinasaba kwani havisaidii?
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, mgodi wa makaa ya mawe, Kiwira, utaanza uzalishaji utaongeza umeme na uzalishaji huu utaboresha sana upatikanaji wa umeme wa kufikia malengo tunayotarajia kuliko kutofanya. Aidha, kudharau au kujali maoni ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, kupeleka fedha, zinazoidhinishwa kwa wakati na kupelekwa kama vile zilivyoidhinishwa badala ya kupeleka pungufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, Serikali itueleze kuhusu madini ya Tanzanite, inakuwaje yanauzwa India, Kenya na Afrika Kusini kwa wingi zaidi ya Tanzania na Tanzania, inachukua nafasi ya nne na India nafasi ya kwanza ilihali, madini hayo yanapatikana Tanzania peke yake?
Mheshimiwa Naibu Spika, hii hatuoni kama ni uharamia unaofanywa na wawekezaji na hata wachimbaji wadogo kuuza holela madini haya? Serikali haina udhibiti wa kutosha kwani Serikali haioni umuhimu wa kufunga mgodi mpaka ijipange kuliko kumalizika kwa madini bila Tanzania kupata faida yoyote na badala yake kuambulia aibu na kukosa Pato la Taifa na kuwapa umaarufu nchi nyingine na Tanzania kuendelea kuwa maskini na kutajirisha nchi nyingine ilI hali madini yale yanatoka Tanzania pekee.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, kwa kuwa, Serikali haina dhamira ya dhati ya kudhibiti madini yanayotoroshwa, ambayo ni ghafi kwani haitoi kauli yoyote. Hivyo, tunaomba, na tunaishauri Serikali, usimamizi wa migodi hii, uangaliwe na Taifa letu lipate pato la kutosha kuliko kunufaisha Mataifa mengine ambayo hayazalishi madini haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la gesi ni muhimu na litasaidia Tanzania kupata umeme mwingi na kusaidia viwanda kuimarika. Vile vile iuzwe, itumike majumbani katika shughuli mbalimbali kuliko kuendelea kununua kwa makampuni mengine ya kuuza wakati, Tanzania tunayo gesi ya kutosha. Pia, Serikali iandae mpango mkakati utakaoweza kusimamia vizuri gesi asilia pamoja na kutafuta masoko madhubuti na ya uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali iwekeze katika miundombinu na utalaam wa madini ya vito ili kuwezesha ukataji na uuzaji wa Tanzanite kufanyika hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, Serikali isimamie kwa umakini wa hali ya juu ukamilishwaji wa miradi na vipaumbele vya uzalishaji vya umeme ili kutuwezesha kupata umeme wa kutosha hapa nchini ili tuwe na viwanda vya kutosha vyenye kukidhi mahitaji ya Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa Serikali ijipange kutekeleza haya kwa moyo wa dhati na sio kuwarubuni Watanzania. Tunapenda kuona Tanzania inaneemeka na rasilimali zake na kuipata Tanzania tuitakayo, iliyoimarika na kupiga hatua za maendeleo mbele zaidi na siyo kila siku tukawa watu wa kurudi nyuma tu na ku-enjoy mafanikio ya wengine tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia nawatakia kila la kheri Serikali na naiombea iwe na moyo wa dhati na kutekeleza yale tunayowaelekeza na kuyafanyia kazi kwa wepesi zaidi ili kuleta maendeleo ndani ya Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha maoni ya wananchi wangu. Ahsante sana.