Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwapongeze viongozi wote wa Wizara ya Nishati na Madini katika kufanikisha uandaaji mzuri wa hotuba ya bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Nishati na Madini ni muhimu katika mpango wa Serikali wa maendeleo na kufanikisha nchi yetu kuwa ya viwanda, kwa kuwa nishati ni kiungo muhimu katika viwanda vyetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, REA; kwanza naomba Waziri aendelee kuwa imara katika Wizara hii na kuwezesha umeme vijijini kufikia malengo. Katika Jimbo la Nsimbo Mkoani Katavi, jimbo lina kata 12, lakini kata nne tu ndiyo zilizopata umeme wa REA. Sambamba na hilo, umeme umepita Kijiji cha Kapalala bila kuwekewa transformer. Tunashauri Wizara ikamilishe umeme katika kijiji hicho tukizingatia kuna wananchi wahitaji. Vile vile, tunahitaji, majibu ya Waziri ni lini kata zilizobaki nane zitakamilika kupata umeme?
Mheshimiwa Naibu Spika, gridi ya Taifa; Mkoa wa Katavi ni moja ya mikoa hapa Tanzania, ambayo haina umeme wa uhakika, yaani wa gridi ya Taifa. Hivyo, tunatumia umeme wa jenereta ambazo zilitolewa Shinyanga na tayari ni chakavu hazifanyi kazi kulingana na uwezo. Hivyo basi, tunahitaji Serikali ikague umeme uliopo Wilaya jirani ya Kaliua kwa kuwa ni jirani sana na Jimbo la Nsimbo. Hivyo, tunahitaji kauli ya Serikali ni lini itafanya upembuzi yakinifu wa kuleta umeme Jimbo la Nsimbo kupitia Kata ya Ugala?
Mheshimiwa Naibu Spika, madini; mradi wa wachimbaji wadogo wa Benki ya Dunia, Jimbo la Nsimbo ni mojawapo lina vijiji 11 ndani ya kata sita zina wachimbaji wadogo. Hivyo, tunaomba Serikali kuchagua maeneo ya mfano kati ya hayo saba. Naomba na Jimbo la Nsimbo tuna sehemu mbalimbali. Kwa mantiki hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri atoe tamko la Nsimbo kuwa kati ya vituo saba vya mfano.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la wachimbaji wadogo; wachimbaji wadogo, ambao wana uwezo wa kuwa na leseni, waweze kupata leseni kwa mujibu wa Sheria (Primary Licence) na waweze kurahisisha wananchi wasio na leseni kuchimba katika maeneo yao na kuweza kuuza dhahabu na kupata mapato kuwasaidia kujikimu wao na familia zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Wizara ikitoa leseni kubwa mining licence (ML) wenye uhalali huo wanakataza wananchi kuchimba. Mfano mzuri ni kampuni ya SAMBARU, Kata ya Ibindi iliingia katika mgogoro na wananchi na hali siyo shwari. Pia, eneo la Dirifu, Kata ya Magamba nako kulitokea vurugu Januari, 2016. Kwa mantiki hiyo, tunahitaji Serikali kutoa tamko vijiji vifuatavyo viwe kwa ajili ya wachimbaji wadogo.
Jimbo la Nsimbo, Kata ya Machimbi, Kijiji cha Katisunga na Kapanda; Kata ya Ibindi, Kijiji cha Ibindi, Kapandamu na Kasherami; Kata ya Sitalike, Kijiji cha Mtisi; Kata ya Urwira, Kijiji cha Urwira, Usense; na Kata ya Itenka, Kijiji cha Msangama. Jimbo la Mpanda Mjini, Kata ya Magamba, Kijiji cha Dirifu Society.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni muhimu sana maeneo ya vijiji hivyo kuwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo kwa kuwa eneo la awali ni Wilaya ya Tanganyika, eneo la Kipalamsenga, ambako kuna madini zaidi ya aina ya shaba. (Copper)
Mheshimiwa Naibu Spika, gharama za maliasili kwa wachimbaji madini utafutaji wa madini kuna wakati wananchi au kampuni huingia katika hifadhi za misitu. Wananchi hutozwa gharama za uharibifu wa misitu. Tatizo lililopo ni tozo zipo kwa ukubwa wa eneo badala ya kuangalia idadi ya miti na kupelekea watu wengi kushindwa kumudu gharama hizo. Hivyo, tunaomba, Wizara hizi mbili zikae pamoja na kuangalia gharama hizo, zipitiwe upya.
Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti wa mafuta Lake Tanganyika kwa kuzingatia maendeleo ya nchi tunahitaji Serikali kupitia Wizara isaidie utafiti wa mafuta katika eneo la Ziwa Tanganyika. Hivyo, taarifa ni muhimu nasi wananchi kujua maendeleo ya utafiti huo na vyema kuwasilisha Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maelezo hayo juu, naunga mkono hoja.