Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia fursa hii ya kuchangia hoja ya Wizara ya Ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwatumikia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme katika pongezi zangu hizi nilikuwa natafuta maneno ya kumwambia kaka yangu Mheshimiwa Jerry, lakini kati ya maneno nitakayompa kama zawadi leo akitoka hapa naomba aende akasome Kitabu cha 1Wafalme 3:16 – 24 akaangalie Hekima za Suleiman. Kila tukikaa tukimtafakari kwa umri wake, Mwenyezi Mungu amempa zawadi kubwa na kitu kikubwa. Amempa zawadi ambayo aliwahi kupewa Suleiman, zawadi ya hekima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya vitu ambavyo viongozi tunapaswa kuwa navyo ni pamoja na kuwa na hekima. Mungu hugawa kwa mafungu na mipango. Kati ya mipango aliyoifanya na katika fungu alilompa, kampatia fungu kubwa. Dada yangu Mheshimiwa Hokororo alisema mvi za Mheshimiwa Waziri ni hekima. Nampa jibu lake kwamba amempa Hekima za Suleiman. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo hekima nazo zitunzwe, zifanyiwe kazi kwa maslahi ya Watanzania. Ndani ya Bunge na Tanzania amekuwa Suleiman wetu. Akawasaidie Watanzania na awatendee haki, asiwe muoga, asiogope, sisi tunamwombea ulinzi. Tunamtegemea sana. Ili kazi ziende ndani ya Tanzania, ni lazima tukubali kama viongozi kuwa kafara, lazima kama viongozi tukubali kujitoa Watanzania wapone. Mama Dkt. Samia amekubali kujitoa kwa ajili ya Taifa la Tanzania. Amekuballi kubeba mazito, msalaba wa chuma na kuelemewa, lakini anasema Tanzania lazima iwe salama, Watanzania lazima wapone na matatizo yao lazima yatatuliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kaka yangu Mheshimiwa Waziri Jerry namwomba akubali kubeba ambacho Watanzania wanakitegemea kwake. Yeye kwetu amekuwa Isaka. Kati ya kondoo aliowaangalia Mama Dkt. Samia akaona kwamba, nani atakayekuwa kafara, yeye ndio amekuwa kafara ya Watanzania kwenye suala la ardhi. Ardhi ya Watanzania ili watu wagawane vizuri, Watanzania wanyonge wapate haki, Mtanzania asiyekuwa na fedha apate haki, lazima utoke kaka, lazima uwe kafara. Usiogope, hili ninakuhakikishia hakuna kitakachokudhuru, chozi la mnyonge ndiyo uponyaji wako, shukrani ya mnyonge ndio uzima na ulinzi wako ndani ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watakulinda kupitia maombi yao na shukrani zao, awatendee haki. Mfikirie mtanzania aliyekuwa mnyonge kila anapokwenda kwenye Mahakama na anaitafuta haki anaikosa. Yeye leo akawe mkombozi wake, Mungu atamlinda. Mwenyezi Mungu atampigania, hakuna kitu kitakachomdhuru wala mwiba utakaomtoga katika kutafuta haki ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo zilikuwa salama zangu kwake za kumpa moyo. Nina mambo manne ambayo nataka nizungumze siku ya leo katika mchango wangu. Jambo la kwanza, hapa nilikuwa nasoma message, kuna watu baada ya kusikia jina langu limetajwa wanatoka katika Halmashauri ya Ilala, wameniambia Mheshimiwa Tauhida sahau kila kitu, tunakuomba utusaidie. Tusemee kuhusu Kliniki ya Ardhi iendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mambo ambayo niliyoyapanga kuyasema ni pamoja na Kliniki ya Ardhi. Ile Kliniki ya Ardhi wakati inawekwa kuna watu wanatoka Zanzibar ambao waliolewa, walioa, wazee wao wanaishi Tanzania Bara, wamedhulumiwa wakati wazee wao wamefariki, unapoweka Kliniki ya Ardhi wanakuja kutafuta haki zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri atafute mzunguko wake endelevu kuona kila muda kipindi fulani kila mkoa, jimbo ikiwezekana na wilaya kuwe na hii Kliniki za Ardhi, kwani ni majibu tosha ya Watanzania. Hatuna njia rahisi ambayo tunaweza kutatua. Hii Kliniki ya Ardhi ndiyo imeenda kuleta majibu fasaha kwa Watanzania, maana matatizo yao yanatatuliwa papo kwa papo na haki yao inapatikana papo kwa papo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, mipango mizuri ya ardhi na matumizi mazuri ya ardhi ni kitu ambacho kitaenda kuondoa migogoro ndani ya Tanzania. Migogoro ili iweze kuondoka, Waziri lazima akubali kuwa na matumizi mazuri ya ardhi, na ili mipango yetu iende vizuri, lazima kuna Wizara zikubali kushirikiana ikiwemo TAMISEMI, Kilimo na Mifugo. Wekeni mipango mizuri ambayo itaenda kumkomboa Mtanzania ili tuweze kwenda vizuri na tuweze kupata majibu mazuri kwenye matumizi mazuri ya ardhi. Ni lazima tuwe na mipango mizuri ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii angalia mifumo ya vijiji vyetu vilivyo, hata maendeleo kwenda kwao vinakawia. Kijiji kimoja kipo huku kingine kipo kule. Kufikiwa na miundombinu inakuwa kazi ngumu, Tanzania tunajipa mzigo mkubwa kwa sababu hatujipangi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, umri wa Mheshimiwa Waziri ni mdogo, anaweza kukimbia, anaweza ku-trot. Akiona muda unakwenda, aache kwenda kwa miguu, a-trot, akimbie, ili Watanzania wapate majibu kazi ipate kwenda vizuri. Kwenye mifumo ya upangaji wa ardhi, hii itaenda kutupatia jibu pia itaondoa migogoro, kwani migogoro mingi inasababishwa na kutokujipanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza wenzetu waliotangulia kwenye Mji wa Dodoma, kwa sehemu kidogo wamejitahidi kupanga panga kidogo, lakini kuna maeneo mpaka leo, hivi vyote tunavyozungumza hakuna Afisa wa Ardhi anaona umuhimu wa kupanga mipango mizuri ya matumizi ya ardhi ndani ya halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri aangalie namna bora ambayo itaenda kuleta majibu endelevu. Hatutaki majibu ya muda mfupi. Wewe leo upo hapo, kesho unaweza ukapelekwa kwingine na kesho ukafanya mengine, bado Tanzania inakuhitaji kwenye sehemu tofauti. Sasa pale tukiweka mipango endelevu kwamba ili ardhi itumike, na wananchi waweze kufanya kazi zao na kutumia ardhi katika shughuli zao, lazima tuhakikishe mipango mizuri ya ardhi inapangwa na inafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niomba Mheshimiwa Waziri aimarishe kitengo chake cha utoaji wa hati. Kiimarishwe na kipewe nguvu. Kama hakina fedha, kipelekewe fedha, kama hakina gari kipatiwe magari, kama hakina kompyuta kipatiwe kompyuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro mikubwa ya wananchi wa Tanzania katika suala la ardhi ni pamoja na kutokupata hati kwa wakati. Muda anavyokawiza mtu kupata hati yake kwa wakati ambao yeye amemiliki kiwanja, hicho ndicho kinachosababisha hao madalali waliokuwepo ndani ya Wizara, hao makanjanja wanaotumika, ndio wanaobadilisha matumizi ya mtu mmoja kwenda mtu mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ana uwezo wa kutoa maamuzi magumu, amsaidie Mheshimiwa Rais wa Tanzania, kwani anapambana, anatafuta fedha kwa ajili ya bajeti zetu, anaweka kila namna ya mipango kuona kila Wizara inafanya vizuri. Waziri kazi yake ni kupanga na kumshauri Rais ili tuweze kutoka hapa tulipokuwepo. Kama kuna wafanyakazi wabovu watolewe, tunataka tuone anaondoa wafanyakazi wabovu.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyakazi wanalalamikiwa wabovu wapo chungu mzima...
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha tafadhali.
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja, namtakia kila la heri Mheshimiwa Waziri, tuna matumaini na imani kubwa juu ya ufanyaji wake wa kazi. (Makofi)