Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyerwa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuongea kuchangia Wizara hii. Kwanza namshukuru Mungu ambaye amenipa nguvu na afya ya kuendelea kuwatumikia Wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu na timu yake kwa kazi nzuri wanayoifanya. Mheshimiwa Waziri kwa kweli umeanza vizuri. Umeanza kuleta matumaini ambayo yalikuwa yamepotea kwa Watanzania walio wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze kuongelea kliniki ambayo Mheshimiwa Waziri ameianza. Kliniki hii imeanza kuleta matumaini makubwa. Tumeona Watanzania wengi wakitatuliwa migogoro yao kwa uwazi na kwa uhuru na hii kwa kweli imeondoa ile mianya ambayo ilikuwa wakati mwingine inaleta mazingira ya rushwa. Kwa hiyo, tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri katika hili ameanza vizuri. Ila tunachomshauri, hizi kliniki zisambae, ziende mpaka vijijini, tumeona anaishia maeneo ya mikoani, tunataka tuone zinaenda vijijini ambapo kuna shida kubwa sana na huko ndiko kuna wananchi wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri hawezi akafanya hii kazi peke yake, atengeneze timu, tunapomwona yuko Arusha, tuone timu nyingine iko Kagera, tuone timu nyingine iko Dar es Salaam. Hautaweza kufika kila eneo, waengeneze timu, wawape mafunzo ili watatue migogoro kwa wananchi, kwa hiyo, ninamshauri katika hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo linguine, niongelee kupanga, kupima na kumilikisha ardhi, jambo hili ni jambo ambalo ni zuri sana na linaenda kuondoa kero na migogoro mingi ambayo imekuwepo kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia maeneo mengi yakiwa na migogoro, lakini pia tumeshuhudia katika maeneo mengi wananchi wanajenga maeneo ambayo ni hatarishi; kwenye mabonde na inapofika kipindi cha mvua, hali inakuwa mbaya sana. Kwa hiyo, tuombe sana Mheshimiwa Waziri wanapoenda kwenye halmashauri hizi ambazo zimepewa fedha lazima watafute mbinu ya kuwabana kwa kurejesha hizi fedha ili ziende kwenye halmashauri zingine ambazo bado hazijapimwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaamini tutakapopima maeneo yetu, tunaenda kuinua Uchumi wa Watanzania na tunaenda kuwaletea maendeleo. Nitoe mfano, ukipima kama Kagera na Kyerwa ambako kuna wakulima wengi wa kahawa, unaenda kuwainua wananchi hawa ambao wamekumbwa na biashara mbaya sana ya Butula. Wanafanya biashara ya Butula kwa sababu hawana fedha, hawana kitu ambacho wanaweza wakakipeleka benki wakapata mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sana na hili namwomba sana Waziri pamoja na Katibu Mkuu, niwaone kwa kweli wamefika maeneo ya Kyerwa, namwomba sana. Kule kuna wateja wengi na wanamsubiria sana Mheshimiwa Waziri ili na wao wapimiwe maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tutakapokuwa tumepima haya maeneo, tumeshuhudia taasisi za Serikali zimejengwa mpaka kwenye njia ambazo zilikuwa ni njia za wanyama, lakini haya maeneo yatakapokuwa yamepimwa, kila mmoja atajua eneo lake ambalo ni sahihi na kuondoa hii migogoro ya wakulima na wafugaji iliyopo na migogoro ya wananchi na Serikali kuingiliana kwenye maeneo ambayo siyo sahihi. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri na ninamkaribisha sana, aje awapimie Wanakyerwa ili Wanakyerwa wanufaike na fedha hii ambayo imetolewa na Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine niongelee Mabaraza ya Ardhi; mabaraza haya yameundwa kwa nia ya kutatua migogoro, lakini maeneo mengi siyo yote, maeneo mengi imekuwa ni kinyume. Maeneo mengi yamekuwa ni kutengeneza mianya ya rushwa, hakuna haki inayotendeka. Ninaomba sana Waziri afanye uchunguzi, maeneo haya kama tukibainisha maeneo Mheshimiwa Waziri, mengi hayafanyi vizuri, ni afadhali haya mabaraza yakaondolewa tukarudisha kwenye haki kwenye sheria, mahakama ambayo tunaamini wanaweza wakapata haki, lakini huku hali ni mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilikuwa nashangaa wakati mabaraza haya yanaundwa, yaani watu walikuwa wanapambana na kutumia nguvu kubwa na rushwa, kumbe ni kwenda kuwaibia wananchi. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri alichunguze hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ni la kujiuliza, Mheshimiwa Waziri hivi haya mabaraza wameyawezesha au wameyaunda tu wakayaweka kule ikaishia hapo? Lazima tujiulize, mabaraza haya tumeyawezesha, wana vitendea kazi? Pia, posho zao zile wanazostahili kupewa, wanapewa na ni nani anayewapa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, anapokuja hapa atueleze ni nani anayewalipa hawa? Pia, je, wamewawezesha na kuwapa mafunzo? Maana wengine hata sheria hawazijui. Kwa hiyo, naomba sana uliangalie hili ili haki iweze kutendeka na wananchi wetu waweze kufurahia jambo hili ambalo ni jema. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nilisemee, Mheshimiwa Waziri hawa Wakuu wa Idara za Ardhi, Maafisa Ardhi wa Wilaya pamoja na kuwaondoa kwenye halmashauri bado wako chini ya halmashauri. Naomba sana wawawezeshe hawa watu, siyo wamewaweka pale bado wanaendelea kuomba kule kwenye halmashauri, hawatafanya kazi vizuri. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba sana wawawezeshe, wawape vifaa na mahali ambapo bado hawajawafikia kwenda kuwapimia kupitia Mpango huu wa KKK, waweze kuwapimia wananchi na maeneo yao yatambulike. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaamini tutakapokuwa tumeyafanya haya, wananchi wakapimiwa maeneo yao hizi kero zitaondoka na nchi itakuwa salama. Pia, tujue uchumi wa Taifa letu utakua kwa sababu mwananchi atakuwa na uwezo wa kufanya jambo lolote anaweza kujipatia fedha kupitia ardhi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nampongeza Mheshimiwa Waziri, anafanya kazi nzuri na nimwambie neno moja, kuna jamaa mmoja, Mheshimiwa mmoja alichangia akasema ardhi imelaaniwa, lakini nimpe Neno la Bwana: “Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki na masikio yake husikia kilio chao”. Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya, utakapokuwa umesimama kwenye haki, ukatenda haki...” Nina uhakika Mheshimiwa Waziri atakuwa salama na hakuna kitakachomdhuru. Mungu ambariki, Amina. (Makofi)