Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Maswa Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu siku ya leo. Naanza kwa kusema naunga mkono hoja iliyoko mbele yetu, Hoja ya Wizara ya Mipango na Uwekezaji, pamoja na Hoja ya Wizara ya Fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hasa kwenye Jimbo langu la Maswa Magharibi kwenye mradi mmoja wa maji. Mheshimiwa Rais ametupatia fedha kwenye maeneo mengi; elimu, afya, kilimo na barabara, na vitu vingi tumepewa. Pia namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kipekee kabisa kwenye mradi huu wa maji kwenye jimbo langu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mkoa wetu wa Simiyu tuna mradi mkubwa wa kutoa maji Ziwa Victoria kwa Wilaya zote tano, lakini kwenye Wilaya ya Maswa upande mmoja ndiyo ulikuwa ule mradi wa maji unaishia. Kwa hiyo, ule upande wa pili ambao mimi niko, hatukuwa na chanzo cha maji kutoka Ziwa Victoria, lakini nachukua nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kuwa juzi juzi mkataba wa kutoa maji Ziwa Victoria kuyaleta kwenye Mji wa Malampaka na hatimaye Mji wa Malya na Vijiji vilivyo karibu umesainiwa, na mkandarasi yuko site. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu, ameniondoa kwenye uyatima wa maji ya Ziwa Victoria kwenye Jimbo langu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara hizi mbili. Hawa mimi naweza kusema tuwaite Singida Boys. Kwa kweli, wamejitahidi, wameweka juhudi kubwa kwenye mpango na kwenye bajeti yenyewe. Juhudi mliyoweka ndani yake kwa kweli matunda yake tumeyaona na ni kazi nzuri. Pia nawapongeza Manaibu wao, Mheshimiwa Chande, Naibu Waziri wa Fedha; Mheshimiwa Stanslaus Nyongo, mdogo wangu, Naibu Waziri wa Nchi kwenye Wizara ya Mipango na Uwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini mambo haya mliyoyapanga yakitekelezwa tunaweza kabisa kupiga hatua pamoja na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge watakaotoa. Naamini kabisa sisi kama nchi tutapiga hatua ya kimaendeleo zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na kilimo kwa sababu na mimi ni mtu wa kilimo na jimbo langu lote kazi kubwa wanayofanya wananchi wangu ni kilimo. Naanza kwanza kwa kuishukuru Serikali kwa miradi ya umwagiliaji kwenye jimbo langu; Mradi wa Umwagiliaji wa Masela, Mradi wa Umwagiliaji wa Bukangilija, naambiwa unapata fedha kwenye bajeti hii tunayoijadili. Basi namshukuru sana Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Bashe, kwa kufikiria kupata miradi ya namna hiyo kwenye Jimbo langu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa letu kwa sababu, mpaka leo Watanzania tulivyo tunapata chakula kutoka kwenye kilimo, mpaka leo tunapata malighafi za viwandani kutoka kwenye kilimo, pia tunapata fedha za kigeni kutoka kwenye kilimo, na tunapata ajira kubwa ya Watanzania kutoka kwenye kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa sana ambacho kwenye taarifa za Waheshimiwa Mawaziri tunaojadili hoja zao wametaja mchango wa sekta ya kilimo kwenye ukuaji wa pato la Taifa kuwa ni mkubwa kuliko mchango mwingine wowote. 26.5% ni mchango mkubwa sana, lakini tujaribu kuangalia sasa kibajeti sekta hii kwa upana wake kwa maana ya kilimo cha mazao na mambo mengine, lakini ukaleta mifugo pia, na uvuvi. Bajeti iliyopangwa hapa ni ndogo sana. Nimejaribu kufanya hesabu, ni kama asilimia nne tu ya bajeti ambayo tunaijadili hapa ndiyo inaenda kwenye kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Taifa nilidhani tungefikiria kukipa kilimo rasilimali fedha nyingi zaidi kuliko maeneo mengine kwa sababu mchango wake ni mkubwa. Kwa kuweka asilimia nne tuliyoweka sasa hivi na huku nyuma ilikuwa ipo chini asilimia tatu na kidogo, lakini bado mchango wake kwenye ukuaji wa Taifa ni asilimia kubwa zaidi, 26.5%. Sasa tungeongeza asilimia nne nyingine kwa mfano, nadhani mchango wa sekta hii ungekuwa ni mkubwa zaidi na hivyo sekta hii ingeweza kuchangia zaidi kwenye fedha za kigeni, kwenye ajira za Watanzania, kwenye chakula kwa ajili yetu kama Watanzania, pia kwenye viwanda kwa malighafi za viwandani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani kama Taifa tuanze kufikiria huko tunapoelekea mbele, tunafanyaje na sekta hii ambayo inatupatia maziwa mengi zaidi kwa kuipa majani kidogo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie juu ya suala la bei za mazao. Mwenzangu Mheshimiwa Kapinga aliyemaliza kusema kabla yangu anashukuru kwa ajili ya bei za mazao anayolima kwenye eneo lake, lakini mimi bei ya zao la pamba kwenye eneo langu bado ni kidogo. Kusema kweli bei za mazao yetu ya kilimo tunabahatisha, kwa sababu tunategemea soko lile la nje. Sasa soko likiwa zuri bei zinapanda, soko likiwa chini, basi bei zinaanguka. Sasa ndivyo ilivyofanyika kwa zao la pamba. Mwaka huu bei ni shilingi 1,060 imepandapanda kidogo nimeambiwa ni shilingi 1,200 mpaka 1,300 sasa hivi kwa sababu ya ushindani bei, lakini bado ipo chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa tunaloambiwa ni kwamba kwa sababu tunauza mazao yetu nje, tunategemea soko la nje. Sasa hii ni sababu kongwe mno kwa Taifa letu. Toka zamani tunaambiwa ni kwa sababu ya kuanguka kwa bei ya soko la dunia, basi mazao yetu pia yanaanguka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sasa Serikali ikaja na mpango wa namna ya kuwazawadia wakulima wa nchi hii ambao wanatusaidia katika mambo mengi. Kuna haja ya kuja na Mfuko wa Kilimo ambao ndani yake tutakuwa na Mfuko wa Fidia ya Bei za Mazao za Wakulima wa nchi hii. Kwa sababu tusipofanya hivyo, tutaendelea kuishi na soko la dunia. Sasa ili tuishi nalo vizuri, sisi kama nchi tufikirie namna ambavyo tunaweza kuwazawadia wakulima wetu kuliko kuiachia dunia ifikirie namna ya kuwazawadia wakati ndio hao wanatulisha, wanatupatia ajira na wanatupatia fedha za kigeni. Kwa mfano, tuna Mfuko wa Reli, REA, Maji, tumeshindwaje kuwa na Mfuko wa Sekta ya Kilimo? Mimi nadhani inawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nitoke hapo kwenye kilimo niende kwenye suala la pili. Sekta isiyo rasmi katika nchi yetu sijaona imetajwa sana kwenye mpango, na hata kwenye bajeti. Sekta isiyo rasmi kwenye nchi yetu kwa mujibu wa utafiti wa Timu yetu ya Takwimu ya Taifa inachukua 46% ya shughuli zinazofanywa na Watanzania. Sasa hii ni kubwa mno na kwa Mkoa wa Dar es Salaam 58% ya kaya zilizopo Dar es Salaam zinajihusisha na sekta isiyo rasmi. Nini maana yake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba, hii sekta isiyo rasmi haijasajiliwa, hatujaitambua sana na pengine shughuli zake zinaweza kuwa zina mtaji mkubwa. Kwa mfano, utafiti uliofanyika Dar es Salaam mwaka 2019 unaonesha kwamba, mtaji uliowekezwa kwenye sekta isiyo rasmi kwa Dar es Salaam ni shilingi bilioni 901.7. Hizo ni pesa nyingi. Hii ni fedha ya kutosha kabisa. Sasa bado tunapokuwa na sekta isiyo rasmi kubwa namna hii, siyo afya kwa uchumi wetu na kwa mapato ya Taifa letu kwa sababu kuna mapato ambayo hatuyapati kutoka kwenye mtaji mkubwa wa namna hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nafikiri Serikali ije na sera zinazovutia sekta isiyo rasmi, iwe rasmi. Serikali ije na sheria na taratibu zilizo rahisi za usajili wa biashara hasa mpya ili kwamba sekta hii isiyo rasmi ambayo inahusisha gereji, bodaboda na vitu vingi mbalimbali ambavyo tunaona kama vina faida ndogo, lakini ni kubwa vikijumuishwa kwa pamoja. Sekta hii isiyo rasmi iwe rasmi na iweze kuchangia mapato ya Taifa letu kama ambavyo sisi wote tunatamani tuwe na kipato kikubwa kama Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mikakati ya kimsaada kwa ajili ya mafunzo na mikopo kwenye sekta hii. Mikakati mingine ni pamoja na motisha za kikodi. Motisha za kikodi zinaweza zikafanya hawa watu wanaokimbia kuwa rasmi wakaja wakawa rasmi. Sasa tofauti na ilivyo sasa hivi, mtu akionekana tu kidogo ana biashara yake ndogo tayari halmashauri na TRA wanaenda pale. Sasa tuje na motisha za kikodi ambazo zitasababisha hawa watu wapende kuwa rasmi badala ya hali walionayo ya kutokuwa rasmi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala lingine la tatu juu ya ajira. Ajira bado ni tatizo kwenye nchi yetu. Watoto wetu wengi wanaomaliza vyuo hawajaajiriwa na kwa hili kila mmoja hapa ni mwathirika kama familia na pia kama Taifa. Takwimu nilizonazo zinaonesha ajira za kudumu zimeajiri Watanzania 18% tu, ajira za muda wa kati zimeajiri Watanzania 10%, pia ajira za muda mfupi zimeajiri Watanzania wengi zaidi kama 72%. Sasa hizi ajira za muda mfupi ni ajira ambazo hazina uhakika kwa sababu ni miezi mitatu, sita au mwaka mmoja.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni juu yetu kuhakikisha sekta zile zinazoajiri watu wengi zinapata rasilimali fedha ya kutosha ili ziweze kutengeneza ajira ya kutosha kwa ajili ya watu wetu. Naona Mwenyekiti umewasha microphone yako. Vinginevyo tutazungumza habari ya ajira, lakini kama tusipokuja na mkakati ambao ni sahihi kwa ajili ya kutibu tatizo la ajira, bado tutaendelea kulia na hili tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru ahsante sana kwa kunipa nafasi, nakushukuru sana na nirudie tena kusema naunga mkono hoja iliyopo mbele yetu. (Makofi)