Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie hii Bajeti Kuu ya Mipango. Cha kwanza, nawashukuru Mawaziri wote wawili, Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo na Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba; pili, nawashukuru Makatibu wote wa Wizara hizo na Naibu Mawaziri; Mheshimiwa Chande na Mheshimiwa Nyongo na viongozi wote wanaofanya kazi katika Wizara hii. Wanafanya vizuri sana kwenye maeneo yetu, tunawaona, tunawapongeza kwa kazi nzuri wanayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijawahi kusoma hotuba ndefu kama hii niliyoisoma ya Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba. Nilivyoiangalia nikaona ni kama hawa jamaa walikuwa wamejikita kama maswali ya questionnaire fulani hivi. Tukijibu hivi itakuwaje? Tukijibu hivi itakuwaje? Kila kitu kibaya na kizuri kimeandikwa kwenye hii bajeti. Sijui mmeiona vizuri jamani! Kila kitu kimeandikwa. Kwa hiyo, nasi kwa kuiona bajeti hii, tunafanyaje kwenye hili jambo ambalo tunaweza kulizungumza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya yote hapa mimi nizungumze maombi maalumu. Bahati nzuri kuna Mipango na Fedha hapa. Jimbo la Bunda ambalo ni jimbo langu, limekatwa mwaka 2015 na limekatwa kwenye mazingira magumu sana. Wananchi wanasafiri kilomita 240 kwenda kutafuta halmashauri na kila siku humu ndani wapo watu wanaomba halmashauri, wanaomba na maeneo mengine kwa maana ya kuongezeka kwa mipaka ya maeneo na majibu ya Serikali yanasema kwamba, tumekuwa na utawala wa muda mrefu au tumekuwa na halmashauri nyingi tumeanzisha, tunazijenga upya ili mje kwenye hizi ambazo zina matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najiuliza, hivi kama Bunda majengo yaliyokuwa Halmashauri ya Bunda yapo wazi, yaani kuteua Mkurugenzi akae pale, wananchi waende kumwona, imekuwa kazi hiyo! Itakuwa na maana gani? Hivi tunasaidia nini? Kwa hiyo, naomba kwenye hili jimbo la Bund,a kweli kabisa tuangaliane. Wakati fulani Mbunge akisimama humu ndani akitetea wananchi wake kwenye jambo nyeti huwa tunakuja na lugha kwamba, huyu anatafuta kura. Hivi wananchi gani wanateseka kwenye nchi hii? Watu waende kilomita 240 kutafuta halmashauri, majengo yao yapo pale Bunda. Kwa nini, msiteue Mkurugenzi akae pale? Kuna ubaya gani? Mkurugenzi tu akae pale Watumishi tugawane tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haiwezekani, kwa nini iwe Jimbo langu la Bunda? Tusiunganishe na Halmashauri ya Mji? Tukaenda. Kwa nini watu wasafiri muda mrefu hivyo? Wanatesekea nini hasa? Tumeandika sera kwamba, tunapeleka huduma karibu na wananchi. Kwa hiyo, naomba hiyo Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, na bahati nzuri yeye kule wale ni watu wake, na nikisema hivyo wanamsikiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi la pili, Mheshimiwa Waziri amesema mwenyewe kwenye hotuba yake vizuri sana, sitaki kuisema zaidi. Amesema, sometimes tunakopa hizi fedha na fedha nyingine kwa kuangalia mikoa ambayo ipo nyuma kimaendeleo. Sasa nijiulize, pale Bunda bahati nzuri Mama, Mheshimiwa Dkt. Samia ametusaidia kuleta mradi wa Mgango – Kiabakari. Mradi ulikuwa umekwama, ametusaidia upo 99%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka Butiama kuja Jimbo la Bunda; Nyamuswa pale ni kilomita tisa. Sisi hatuna maji ya Ziwa Victoria. Yaani leo maji yanasafiri kutoka Ziwa Victoria yanakuja Dodoma. Sisi ambao tuna kilomita 20 hatuna maji. Sasa equal distribution ipo wapi? Ipo wapi kugawana keki? Kwa hiyo, nawaomba kwenye haya maombi maalum wafanye hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna barabara ya Sanzati – Nata. Sasa ni miaka 11, nimeona certificate za mkandarasi C 13 hazilipwi. Barabara imeshalimwa ipo, madaraja yamejengwa, haikamiliki. Kwa hiyo, naomba Halmashauri ya Wilaya, Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria kwa vijiji 33 na barabara ya Sanzati iwekwe kwenye orodha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, alipokuwa anaongea rafiki yangu hapa Mheshimiwa Mwijage, nilikuwa nasoma bajeti yake yam waka 2017/2018, nikahesabu alivyokuwa amemsifia Marehemu Dkt. Magufuli kama mara 70 hivi, lakini nimeona bajeti hii pia Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ulivyomsifia Mama kama mara 100 hivi, nikasema haya mambo yanategemea na mapenzi ya kila mtu na kile anachokiona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niweke record, leo mniandike vizuri hapa, kwamba Mungu akimsaidia Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia akamaliza vipindi vyake viwili, atakuwa Rais bora katika nchi ya demokrasia. Haitatokea, atakuwa Rais anayevumilia watu, Rais anayejenga watu, haitatokea na atakuwa Rais bora zaidi. Mama ni mvumilivu kiasi. Watu hapa tupo tofauti sana. Wapo watu wana mambo mengi sana hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu imepatwa na ugonjwa wa kusema fulani anatafuta Urais, sijui kutafuta Urais ni dhambi? Yaani ni ugonjwa ambao umekua, lakini Mama amevumilia kwa kiasi chote. Kuna watu hapa wanamsema vibaya Mama na hao anawavumilia. Kuna watu wengine alienda hata kuwasalimia na kuwaona; Mama anavumilia, atakuwa Rais mwenye demokrasia kubwa hapa duniani kama alivyokuwa anafanya hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimeona juzi watu wanauliza, CCM wajifunze kutoka South Africa. South Africa sisi ndio tunawapa dawa, sisi ndio waganga wao. Tuliwaambia msigeuke nyuma, wakageuka nyuma. Tunachosema, haya maneno yanayokuja hapa, mara mna vikaratasi, sijui vikaratasi mtu amefanya nini? Sijui amekodisha sukari, sijui amefanya nini? Mgawanyiko huu tunapoelekea kwenye uchaguzi ndiyo unaua chama. Huu mgawanyiko, watu wanatoa, kila mtu ana vikaratasi vyake, kila mtu anagombana, huo unaua chama. CCM miaka yote tumeheshimu Marais wote waliokuwepo, tumeheshimiana na watu wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwombea Mama, hii timu yake aliyonayo ya Mawaziri, Mawaziri hawa wanaochapa kazi usiku na mchana aende nayo na amalize nayo. Kwa hiyo, mgawanyiko wa Chama cha Mapinduzi kwa kuoneana wivu, kwa kutaka Madaraka, ndio unaua chama, na chama hiki kwa sasa kipo vizuri mno, na hao wanaotembeatembea huko barabarani mwasubiri waingie king. Wataingia tu haina shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumzia equal distribution Mkoa wa Mara. Sasa nilikuwa nazungumza ya Jimbo la Bunda; sasa nije ya Mkoa wa Mara. Katika bajeti hizi, lazima mkumbuke Mkoa wa Mara. Leo watu wanazungumza reli iende mpaka Burundi iende wapi, lakini sisi reli inayotoka Tanga – Moshi – Arusha - Mara haijulikani hata ipo wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo bandari iliyokuwepo Mkoa wa Mara - Musoma haipo, viwanda vya pamba havipo, viwanda vya Samaki havipo, ginneries za Kibara na Kosasi hazipo, hata kiwanja cha ndege tulichoanza kujenga juzi hela haiendi vizuri. Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ina majengo mawili; jengo moja limekamilika, moja bado.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mama na vitita hivi kupeleka fedha, ajitahidi tumalize lile jengo angalau hata Hospitali ya Wilaya ionekane. Mkoa wa Mara umerudi nyuma sana. Tunaomba katika bajeti hii na mnapoenda mtufanyie vizuri ili mkoa wetu nao uonekane kwamba una maana kwenye nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni walipa kodi ya mifugo. nimeiona amezungumza Mbunge wa Ngorongoro, nami nikawa naangalia, hivi Mheshimiwa Dkt. Mwigulu huyu, mbona niliwahi kuona ka-statement kamesema ni mtoto wa mkulima na mfugaji. Hii lugha ya kuonekana kwamba wafugaji hawalipi kodi, hawakai vizuri inatoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaeleze, katika nchi kwenye chemistry kuna kitu kinaitwa catalyst, kama ukitengeneza soda, unaiweka inachochea. Katika watu wanaochochea maisha ya Watanzania hapa Tanzania ni wafugaji. Kilimo cha Tanzania 65% kinategemea Plau; ni ng’ombe hiyo hiyo; ni ngo’mbe ndio wanaolisha watu; mazao yanayozalishwa mnakata kodi, ni ng’ombe inazalisha. Leo vinywaji mnavyowekea kodi kubwa mtu anywe pombe vizuri lazima ale nyama inatoka wapi hiyo nyama? Anaitoa wapi? Leo minada yote mnayoenda kutafuta mbuzi na ng’ombe mnaitoa wapi? Maziwa yanatoa kwashakoo, Serikali haitoi hela; kwashakoo ni ngo’mbe. Mnaitoa wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu leo mfugaji unasema ana ng’ombe 900, ana ng’ombe 9,000. Hata angekuwa nazo 10,000, eneo analoishi analipia kodi. Wafugaji wote wenye ngo’mbe 1,200 tunalipa kodi. Sisi kodi kubwa, kilometa moja unaweza kulipa shilingi 2,000,000 mpaka shilingi 3,000,000 halafu mnaenda kuongeza sijui iwe shilingi 31,000, sijui elfu ngapi? Hapana mzee, punguza hapo. Punguza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujue hawa watu, ni watu wanaishi. Wanakaa katika maeneo ambayo yana changamoto za ufugaji; maeneo ya malisho na maji. Wafugaji hali yao sio nzuri. Kwa hiyo, tunawapa nafuu ili waendelee kuwepo. Hivi mnaongeza kufanya nini? Kwa hiyo, nawaomba kwenye mambo ya mifugo, Mzee wewe nimekuona na statement yako ninayo, umetokana na hao watu. Angalia kwanza tabu zao ni kubwa, msiongeze tabu juu ya tabu. Watapata shida sana watu hao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo leo ninalo ni mifumo. Nimesoma bajeti hii vizuri sana. Mifumo eti siku hizi kuna robot inaitwa mifumo. Sasa hivi unaweza kusema sekondari fulani imepata shilingi milioni 340; saa nne hesabu inasomeka zipo pale benki shilingi 340. Saa nane mfumo umetembea umerudi hela haipo. Siku hizi kuna mifumo kama robot. Sasa nchi hii unaweka hela kwenye akaunti za maendeleo, hela zipo ataiona asubuhi. Kuna Kituo kimoja cha Polisi, tunajenga, nimepewa shilingi milioni 50, RPC ananiambia hela iliingia jana, imetoka juzi. Imeingia sijui lini na imetoka, yaani kuna mifumo inatembea. Leo tunamaliza bajeti tarehe 26, tutaanza mwezi Julai, mifumo inaanza kufungwa mpaka mwezi wa Septemba. Hivi ni nini hiki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunatunga sheria ya kufanya bajeti itumike, lakini mifumo itafungwa, haifunguliwi. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, bahati nzuri wewe ni mzalendo unaishi na Bendera ya Taifa. Tazama vikwazo vinavyotokana na fedha. Ni bora fedha iwe haipo kuliko fedha ipo haifanyi kazi. Kwa hiyo, kwenye suala la mifumo, hiyo mifumo inayotembea kama robot uione uanze kuidhibiti. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa unaweza kuhitimisha, tafadhali.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Naam!

MWENYEKITI: Unaweza ukahitimisha, tafadhali.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya sawa. Nahitimisha kwa deni la Taifa, sasa huwa najiuliza, hivi deni la Taifa au ni wajinga, waliliwa? Hivi deni la Taifa linahusu Afrika tu au?

MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda umeisha.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake mimi nimeona madeni ya Taifa ya nchi zinazoendelea ni makubwa mno, makubwa, 240%, asilimia tatu, 160% na asilimia ngapi? Hivi Afrika ndio sisi wajinga, tunasema madeni, madeni! Madeni ya wapi? Ahsante. (Makofi)