Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2

Hon. Jacquline Andrew Kainja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2

MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia taarifa hii ya Kamati ya Afya na Masuala ya UKIMWI. Kwanza, kabisa napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya na uzima. Vilevile, nampongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Afya na Masuala ya UKIMWI kwa kuwasilisha vizuri taarifa ya Kamati. Nawapongeza sana Wanakamati wote wa Kamati Afya na Masuala ya UKIMWI. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii vilevile kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa namna anavyofanya kazi katika Sekta ya Afya, amehakikisha anaboresha huduma. Vilevile, tuzo ambayo ameipata mchana wa leo, ambapo amepunguza vifo kutoka 556 mpaka 104, hiyo imekuwa ni dhima yake kubwa kuhakikisha vifo vya mama na mtoto tunafikia kwenye asilimia sifuri. Kwa hivyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuchangia taarifa ya Kamati, naomba nianze kwa kuchangia katika Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania. Ni wakati sasa wa Serikali kuhakikisha inatekeleza kikamilifu mpango wa utekelezaji wa kukamilisha afua za UKIMWI ambao waliuzindua Tarehe Mosi Disemba, 2024 na mpango huu ulikuwa ni shirikishi katika sekta zote nchini, kuhakikisha tunatekeleza rasilimali za ndani ya nchi ili kuweza kudhibiti na kupambana na VVU pamoja na UKIMWI. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi binafsi nipende kuipongeza Serikali kwa namna ambavyo imeona tuna haja kubwa ya kuwa na mpango madhubuti ambao ni wa ndani wa kujiwezesha sisi wenyewe, kama Taifa, ili tuweze kujisimamia sisi kama sisi, kuhakikisha afua hizi za UKIMWI tunajisaidia kwanza, kabla ya kupata fedha kutoka kwa wafadhili.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi kabisa tunaelewa Tume yetu ya Kudhibiti UKIMWI inategemea asilimia kubwa ya fedha kutoka kwa wafadhili wa nchi za nje na hususani Serikali ya Marekani, kwenye mfuko wa dharura wa Rais wa Marekani, vilevile Mfuko wa Dunia wa UKIMWI, Malaria pamoja na Kifua Kikuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Bajeti ya 2024/2025 katika Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) 86% ilikuwa ni fedha za nje ambazo ni sawa na shilingi bilioni 11.336 ukilinganisha na fedha za ndani ambazo ni 14%, sawa na shilingi bilioni 1.880. Kitu ambacho unaona kwa uwiano huo na tukiangalia sasa hivi wenzetu wa Marekani, Rais ametangaza anasitisha huduma katika mfuko wake huo wa dharura. Sasa hatujajua mfuko ule utasimamishwa kwa muda gani. Kama Taifa tunajipangaje?

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuishauri Serikali mpango ule ambao tuliuzindua Tarehe Mosi Disemba, 2024 wa kuhakikisha tunajisimamia tuendelee kuusimamia uweze kufanya kazi, ili kuondoa sintofahamu kwa wananchi ambao wana VVU, ambao wanatumia dawa na ambao hawatumii dawa. Inakuwa ni taharuki katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi ambao unafanyika katika nchi yetu; naipongeza sana Serikali, nampongeza Mheshimiwa Rais, kwa kuendelea kuhakikisha huduma za afya bora zinapatikana nchini. Huduma ambazo tulikuwa tunazifuata nchi za nje, kama upandikizaji wa figo, zinapatikana nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu, huduma hizi zinapatikana Muhimbili, hasa za uoteshaji, utunzaji na upandikizaji wa chembe za viungo vya binadamu, zinapatikana Muhimbili pamoja na Hospitali yetu ya Kanda, ya Benjamini Mkapa. Sasa ni takribani miaka nane, lakini huduma hii inatolewa bila kuwa na sheria; hatuna sheria ya huduma hii hapa nchini ambayo itaweza kumlinda mtoa huduma na mpokea huduma ili kuondoa athari za wasiwasi wa mpokea huduma kulingana na uhakika wa afya yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali iweze kuja na Muswada, ili tuweze kutunga Sheria itakayoisimamia huduma hii ambayo inaendelea kutolewa nchini na imeshafika miaka nane kama ambavyo nimesema. Vilevile, tukiwa na Sheria itaweza kutusaidia kuepukana na biashara ya viungo vya binadamu, tunasema chembe za viungo vya mwili wa binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, kutunza haki za kibinadamu. Tumekuwa na matukio mengi ya kutisha ya ukatili ambapo viungo vya binadamu vinatolewa. Kwa hiyo, naiomba Serikali iweze kuja na Muswada tutengeneze sheria, ili tuweze kufanya matibabu haya ambayo Mheshimiwa Rais ameruhusu na amegharamia madaktari bingwa, pamoja na vifaa ambapo inatolewa ndani ya nchi yetu katika hospitali zetu mbili za Taifa na kanda. Sheria pekee ndiyo itaweza kumlinda daktari na kumlinda anayeweza kupatiwa huduma hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)