Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuwa mchangiaji wa kwanza.
Mheshimiwa Spika, ninaanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa uhai na uwezo wa kusimama hapa leo. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa juhudi anazofanya kwenye sekta hizi tatu za viwanda, kilimo, mifugo na uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia ninawapongeza Mawaziri wanaosimamia Wizara hizo; Mheshimiwa Dkt. Jafo na Msaidizi wake Mheshimiwa Kigahe; Mheshimiwa Hussein Bashe na Msaidizi wake Mheshimiwa Silinde; Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji na Msaidizi wake Mheshimiwa Mnyeti, wamefanya kazi ya kubeba maono ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaanza kwa kuichangia hoja ya Liganga na Mchuchuma. Huu ni mfupa uliomshinda fisi, lakini tunapokwenda Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan chini ya Serikali yake ya Chama cha Mapinduzi anaenda kuutafuna na kuumaliza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye Kamati, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na wataalam wake walikuja na taarifa ambayo tangu tuwe kwenye hiyo Kamati hatujawahi kupata taarifa ya aina hiyo. Hiyo ilitokana na nini? Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda Dkt. Hashil hakuwa mchoyo alipopewa Naibu Katibu Mkuu ambaye ni Dkt. Suleiman kumpa mawazo na nafasi ya kusimamia zile taasisi muhimu ndani ya Wizara ya Viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika wetu, Dkt. Tulia Acksson, yule kijana ni mahiri wa sheria, nimemlinganisha na wewe. Pia ni mahiri wa uchumi, na alichoongeza pale ni mahiri wa lugha ya watu ambao tunaenda ku-negotiate nao kuhusu mikataba ya Liganga na Mchuchuma. Kwa hiyo, sasa hawana kona ya kupindapinda. Wakipinda kwa lugha yao, anao. Kwa hiyo, Liganga na Mchuchuma inaenda kufika mwisho. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, tulitoa maelekezo kwa Mheshimiwa Waziri Jafo kwamba, hii taarifa tuliyoipata Kamati, akuombe kibali na ninajua wewe unavyopenda Waheshimiwa Wabunge wako waende kwa pamoja, hutakataa. Hii taarifa ije kwa Waheshimiwa Wabunge wote, ili wote twende na uelewa mmoja kwenye Liganga na Mchuchuma. Tungekuwa na uelewa mmoja, juzi Mheshimiwa Mbunge wa eneo husika asingeweza kuuliza swali la msingi kwamba sasa tunaenda wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina imani kabla ya Bunge hili kuahirishwa, ruhusa itatoka na Mheshimiwa Jafo atajipanga na wataalam wake hao waje wawape Waheshimiwa Wabunge ile taarifa ya Liganga na Mchuchuma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia niiongelee SIDO. Nchi yoyote iliyoendelea ni lazima iwe na taasisi kama SIDO. Hata hivyo, SIDO ya kwetu Tanzania ndiyo tunaitegemea iandae viwanda vidogo vidogo kusaidia akina mama na vijana. Hata hivyo, inahemea kwenye oxygen. Kwa sababu gani? SIDO inatakiwa iwe na wafanyakazi 456 lakini sasa hivi ina wafanyakazi 277, pungufu ya wafanyakazi 179.
Mheshimiwa Spika, hili linaenda na taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Viwanda; TIRDO, TEMDO, KMTC, CAMARTEC na NDC yenyewe inayowasimamia. Vile vile Suala la watumishi inabidi Serikali iliangalie kwa mapana zaidi. Pia, SIDO wanakabiliwa na madeni ya pango la ardhi kwenye sehemu ambazo ofisi zao zipo.
Mheshimiwa Spika, sasa nilichoshangaa, hawa hawafanyi biashara. Hizi ni taasisi za Serikali, lakini zina madeni lukuki kwamba ni pango la ardhi. Wanapata wapi mapato ya kulipa pango la ardhi? Naiomba Serikali ifute yale madeni yaliyopo na iende ikachakate sheria za kodi, taasisi za Serikali ambazo hazifanyi biashara zisiwe zinalipa pango la ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia kuna uchakavu wa miundombinu kwenye hizi taasisi zetu, na lenyewe liangaliwe kwa sababu tunategemea hawa ndio watengeneze mitambo, vifaa lakini hawana vifaa vya kuwasaidia.
Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine iliyopo ni kwamba, bado Serikali hatujaamini zana zinazozalishwa na hizi taasisi zetu. mfano mzuri ni TEMDO, wanazalisha mpaka majokofu ya kutunza maiti, lakini Wizara ya Afya bado haijachukua jukumu sahihi kununua hayo majokofu ili tu-save fedha za kigeni. Ni Wizara ya Ulinzi tu ndiyo imeanza kununua yale majokofu. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali kupitia viwanda na Wizara ya Afya wachukue mkakati thabiti wa kuweza kununua hivyo vifaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hawa TEMDO wameweza kutengeneza viwanda vidogo vidogo vya sukari. Tunawapongeza Wizara ya Kilimo kwa sababu wao waliweza kuwekeza fedha za kusaidia TEMDO kuunda mitambo hiyo ya viwanda vidogo vidogo vya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naenda kwenye kilimo. Nawapongeza sana Wizara ya Kilimo, leo hii tumeona kwenye magazeti Tanzania tumekuwa wazalishaji wa pili Afrika kwa zao la mahindi. Hili siyo jambo dogo. Kwa hiyo, waliokuwa wanabeza nguvu anazoweka Mheshimiwa Dkt. Samia kwenye kilimo, wameanza kuona matokeo chanya. Naamini itachukua muda kidogo, baada ya umwagiliaji kukaa sawa, tutakuwa namba moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, twende kwenye uvuvi na mifugo. Nawapongeza sana Wizara ya Uvuvi na Mifugo, mmeweza kufanya, mnataka kuja na chanjo. Nampongeza Mheshimiwa Waziri, tulipomwambia kwenye Kamati kwamba Halmashauri sasa zinataka kuitumia chanjo ya mifugo kuifanya chanzo cha mapato, mara moja ametoa tangazo na tumeliona, kuwaambia kuna bei elekezi iliyoelekezwa na Wizara ya Mifugo. Kwa hiyo, halmashauri wasiweke bei elekezi za kwao wanazojua. Hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia kuna maabara ya uvuvi wa Kitaifa. Hii ndiyo maabara kubwa katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini lakini maabara hii bado inasuasua. Haijapewa bajeti ya kutosha na vifaa vya kisasa, kwa hiyo, tunakosa soko la Samaki. Hao wanaotaka kuja kupima samaki wao, hatuna vifaa vya kutosha kuweza kupima Samaki. Kwa hiyo, tunapoteza mapato kupitia hapa. Sasa Serikali iweke juhudi ya kuwapa vifaa vya kisasa, teknolojia ya kisasa na watumishi wa kutosha ili tuweze kuitumia hii maabara kwa malengo ambayo tumejiwekea wenyewe.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, niseme tu kwamba kilimo, viwanda na uvuvi, washirikiane, wao ndio sekta mahiri za kuendeleza uchumi wa Tanzania, waweke maono ya Mheshimiwa Rais, waweze kuungana na hizi sekta zao zifanye kwa pamoja ili tuweze kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)