Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwera
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kuchukuwa nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili nami kuwa miongoni mwa wachangiaji.
Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nianze mchango wangu kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, lakini pia nampongeza kama Amiri Jeshi wa Majeshi yetu ya Ulinzi na Usalama kwa kuendelea kuhakikisha kwamba nchi yetu pamoja na majirani zetu wanaendelea kuwa salama. Hilo ndilo jukumu la msingi la kikatiba la Rais wetu. Ninampongeza sana.
Mheshimiwa Spika, vile vile naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuwa kinara katika kuhakikisha pamoja na kwamba analilinda Taifa letu na majirani zetu, lakini pia na ukanda wetu wa East Africa pamoja na SADC. Kwa kweli amekuwa kiongozi kinara anayeonyesha kwamba amekusudia kuwa sehemu ya uongozi bora.
Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo hiyo, utakumbuka kwamba tunayo changamoto. Bado nasema ni changamoto kwa upande wa majirani zetu wa DRC na wenzetu wa Rwanda. Ni changamoto za kimaisha, lakini Mheshimiwa Rais amesimama kinara na kuhakikisha kwamba jambo hili linapatiwa ufumbuzi na ametoa wazo. Vile vile amekubali kuhodhi mkutano huu ili kuweza kulitatua jambo hili kama Rais, kama Tanzania. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, kwenye taarifa yetu tumezungumza mambo mengi sana. Moja katika hayo, naomba nivipongeze nyombo vyetu vya ulinzi na usalama, vyote kabisa, kwa sababu vyenyewe vinafanya kazi kwa kushirikiana na Mheshimiwa Rais ili kuhakikisha kwanza vinafuata Katiba yetu.
Mheshimiwa Spika, pili, vinafuata sheria ili kuhakikisha kwamba haki na wajibu wao unatendekea, lakini vile vile kuwafanya wananchi waendelee kutambua kwamba usalama wao ndiyo suala namba moja. Nawapongeza sana viongozi wetu hao.
Mheshimiwa Spika, taarifa yetu imesema mambo mengi sana, lakini moja ya mambo ambayo ningependa kuipongeza Serikali ni juu ya kuviwezesha vyombo vyetu hivi kutekeleza majukumu yake vizuri kabisa.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tunayo changamoto ya upatikanaji wa fedha, lakini Serikali imeendelea kujitahidi. Sasa kwenye hili, ombi langu ni kwamba, yapo maeneo ambayo ni lazima tuyape kipaumbele. Kwa mfano, taarifa yetu inasema kwa upande wa Magereza, tunayo Magereza yetu ambayo yamejengwa zaidi ya miaka 100 iliyopita. Tumetembelea kwenye baadhi ya Magereza haya, tumeangalia wafungwa walivyo, tumeangalia na hali zao.
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali kwamba, pamoja na kwamba inaendelea kujitahidi, bado hoja ya kuhakikisha kwamba tunaviwezesha vyombo hivi, tunatengeneza miundombinu bora kama tulivyoanza ili tuweze kuondokana na hili kwa sababu sheria pia zinatuhitaji, watu hawa waweze kupatiwa haki zao kama wafungwa, kwa sababu ufungwa ni adhabu, lakini huwezi ukapata adhabu ndani ya adhabu. Kwa hiyo, naomba Serikali iendeleze jitihada zake za kuhakikisha kwamba Magereza haya yanakwenda kwa mujibu wa sheria kwa kadri inavyohitajika.
Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo hiyo, napenda kwenda kwenye upande wa Wizara yetu ya Mambo ya Nje. Naomba niwapongeze wenzetu wa Wizara hii, kwa sababu, kule nyuma tuliwahi kusema kwamba Wizara hii ndicho kioo chetu, inapimwa kwa mazuri na mabaya, ya ndani na nje. Sasa kwa hapa, na kwa haya yanayoendelea ndani ya nchi yetu, ndani ya Afrika Mashariki na ndani ya SADC maana yake kiungo kikubwa ni Wizara yetu ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika, wenzetu hawa wanafanya kazi kubwa sana, kwa kuelewa kwamba sheria zetu na majukumu yao yanawataka kuendelea kuitunza au kutunza majirani zetu ili kuhakikisha kwamba tunaendelea kuishi salama; lakini kwa maana hiyo hiyo ni sehemu inayoweza kutuwezesha kufanya biashara na wenzetu hawa. Kwa sababu pamoja na siasa, lakini hoja ya kuendeleza uchumi ni nzuri zaidi kwa sababu itatusaidia kuweza kuishi na majirani zetu vizuri.
Mheshimiwa Spika, nawapongeza sana Wizara ya Mambo ya Nje kwa hoja ya Wizara hiyo ya kuhakikisha kwamba inamsaidia Rais ili kuweza kupambana na matukio ya ndani na ya nje ili kuhakikisha ukanda wetu wote wa Afrika Mashariki na SADC unabaki salama, na waendelee na hili.
Mheshimiwa Spika, mwisho kuliko yote, tumesikia kuhusu upungufu wa vitendea kazi, taarifa yetu imesema. Naomba tujitahidi kwa sababu sasa tumeboresha jeshi letu. Kwa mfano, katika Jeshi letu la Zimamoto kumekuwa na Idara ya Uokozi. Idara hii ukiitizama ni ndogo, lakini ukweli ni kwamba ina kazi kubwa, kwa sababu inatakiwa kuhakikisha inasimamia uokozi kwenye bahari, pamoja na kusimamia uokozi kwenye mito na maziwa. Bado chombo hiki ni kipya. Nadhani ni mwaka mmoja au miwili tumeweza kukifanya kuwa jeshi kamili. Maana yake ni kwamba ni lazima tuendelee kuviwezesha ili viweze kuwa matumaini kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii ni kwa sababu mvua zinaendelea kunyesha na wananchi wanaishi maisha yao kwa kutegemea maji. Tunahitaji kuviwezesha vyombo hivi ili viweze kuwasaidia, pamoja na kuwaokoa, kwa sababu ajali zinatokea, baharini na angani, lakini kwetu sisi naomba Serikali iongeze jitihada za kuhakikisha kwamba inawapatia watumishi wanaostahili, na vitendea kazi.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, tumezungumza kuhusu boti, helkopta, na ndege, ili iweze kufanya kazi zake vizuri na kuhakikisha kwamba wananchi wanaendelea kubaki salama na kuwa na imani na Serikali yao na Rais wao na Chama chao cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. (Makofi)