Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kutoa mchango wangu kwenye Kamati zetu hizi mbili. Kwanza, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya na kuweza kukutana tena hapa kwa ajili ya lengo la kuendelea kulipigani Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, naomba nianze na Wizara ya Kilimo kwenye Kamati ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo. Natamba juhudi kubwa ambazo zinafanywa na Serikali kwenye suala lote la kuboresha sekta yetu ya kilimo kwenye taasisi zake mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, bado tuna changamoto kubwa sana kwenye sekta ya kilimo, kwa mfano kwenye umwagiliaji, tulijiwekea malengo ili tuweze kulisha Afrika, na tukasema ili tuweze kutimiza lengo hilo ni lazima tutoke kwenye kilimo cha kutegemea mvua ya Mungu na badala yake twende kwenye kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hali ni ngumu kwenye sekta ya umwagiliaji, fedha bado ni changamoto. Wizara imetangaza miradi mingi ambayo yote imebaki, haiendelei, hakuna mradi unaotekelezeka kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Sasa kwenye suala la utoaji wa fedha, naiomba Serikali kwa maana ya Wizara ya Fedha wasaidie kutoa fedha kwenye sekta ya umwagiliaji ili tufikie hilo lengo.
Mheshimiwa Spika, leo tumetangazwa kwamba ni nchi ya pili kwenye suala zima la uzalishaji wa zao la mahindi. Laiti Serikali ikiiona sekta ya umwagiliaji na ikatoa fedha hizi tukajenga miradi yetu ya umwagiliaji, Tanzania tutaongoza, tutakuwa wa kwanza kwenye uzalishaji, siyo wa mahindi tu, itakuwa ni mazao yote ya chakula pamoja na mazao mengine ya biashara. Kwa hiyo, naomba sana Wizara ya Fedha iweze kutusaidia hizo fedha ili tuweze kwenda kutimiza hayo malengo yetu.
Mheshimiwa Spika, pia fedha hizi zinapotoka, naomba Wizara ya Kilimo, tusiende na miradi mingi kwa wakati mmoja. Tuchague miradi ya kipaumbele, iende itolewe fedha ambazo zitakamilisha miradi ile ili ianze kuzalisha na kuleta fedha kwa Watanzania badala ya kwenda na miradi mingi ambayo mwisho wa siku kunakuwa na miradi yote isiyotekelezeka.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ninalotamani kulisema siku ya leo ni kuhusu suala la uanzishwaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Kilimo, hususan masuala ya ugani. Tumeona tija kubwa iliyotokea kwenye taasisi kwa mfano RUWASA, baada ya kuanzishwa. Leo tunaona namna ambavyo angalau kwenye maeneo machache, maji yanaanza kupatikana; pia TARURA hali kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana Serikali ione umuhimu wa kuanzisha mamlaka hii ili iweze kutusaidia kusimamia kule chini kwenye halmashauri zetu. Hii itawezesha, kwanza, hawa wataalamu wetu kuwa karibu na wale wakulima. Pili, Wizara, kama msimamizi wa sera atakuwa yupo pale, anaweza kusimamia na kuona ni namna gani shughuli zake za kilimo zinavyokwenda na kutekelezeka. Pia litasaidia kwenye suala la uchukuwaji wa hatua kwa wale viongozi ambao watakuwa hawatimizi wajibu na majukumu yao kwenye maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana, suala hili la uanzishwaji wa mamlaka ya kilimo liwe ni kipaumbele ili tuweze kuisaidia sekta ya kilimo kwa wakulima wetu wadogo kule chini.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo natamani kulisema ni suala zima la usimamizi wa sekta ya sukari. Pamoja na kwamba hali imetulia, lakini ni ukweli kwamba bado hali siyo shwari sana kwenye sekta ya sukari.
Mheshimiwa Spika, bado tuna changamoto ya uzalishaji wa miwa kwenye mashamba tuliyonayo. Bado mashamba tuliyonayo yanazalisha chini ya kiwango, hayafikii lengo. Hata hivyo, viwanda tulivyonavyo bado havizalishi vizuri kwenye hiyo miwa tuliyonayo kwenye viwanda vyao.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Wizara watafute namba ya kutengeneza mkakati madhubuti wa kuweza kuwasimamia hawa watu wa tasnia ya sukari. Mashamba au maeneo waliyonayo, moja yazalishe kama walivyojiwekea malengo yao. Pili, na viwanda vyetu pia viweze kupata material na viweze kuzalisha ili tupunguze fedha nyingi tunazoendelea kuagiza sukari nje ya nchi na kuendelea kupoteza fedha nyingi za kigeni.
Mheshimiwa Spika, tunatakiwa tuzalishe sisi wenyewe tuweze kuuza kwa majirani zetu nasi tuweze kuongeza hizo fedha za kigeni, lakini pia tuweze kujitosheleza na bei iweze kushuka kwa Watanzania wetu hapa ndani ili wote waweze kutumia sukari.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine pia ni kwenye sekta ya mafuta. Serikali ilikuja na mpango mzuri sana wa kuhamasisha wakulima kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu za uzalishaji wa mafuta. Wananchi walihamasika wakalima kwa msimu mmoja. Baada ya hapo, msimu wa pili bei iliporomoka. Baada ya bei kuporomoka Serikali ikatoa fursa ya kupunguza kodi kwenye uagizaji wa mafuta nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, leo tunapozungumza, wananchi wamekata tamaa kulima mchikichi, kulima alizeti kwa sababu bei imeporomoka. Pili, wale waagizaji wa mafuta au watu wenye viwanda vya mafuta ambao wanapewa fursa ya kuagiza wameona, ni rahisi kuagiza mafuta nje kuja kuyaleta humu ndani na kuyachakata na kuuza badala ya kununua mazao yaliyomo humu ndani.
Mheshimiwa Spika, sasa kama Taifa tukiendelea na hali hii, hakika hatutafikia lengo ambalo tulikuwa tumejiwekea kama nchi, la kuhakikisha kwamba tunatamani tuzalishe vya kwetu, kwa sababu uwezo tunao, ardhi tunayo, nguvukazi tunayo. Ni kwa nini Serikali tuendelee kuagiza mafuta nje, huku tukiwa tunatumia fedha nyingi kuagiza mafuta nje? Kwa hiyo, naomba Wizara ya Kilimo irudi kwenye mkakati wake na malengo yake ya kuhakikisha kwamba tunapata mbegu zilizo bora. Pili, tunahakikisha kwamba zao hili linasimamiwa na linakuwa na bei, na tunahakikisha wanunuzi wanakuwepo na tuweke bei elekezi, hususan kwenye zao la alizeti.
Mheshimiwa Spika, leo zao la alizeti limekuwa kila mmoja anakwenda kununua kwa bei yake. Kwa hiyo, naiomba sana Wizara ya Kilimo watusaidie kwenye hili ili tuweze kuondokana na adha kubwa ya upatikanaji wa mafuta kwenye Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, sasa nihamie kwenye Wizara ya Viwanda, ambayo hii pia itakuwa na Wizara ya Kilimo. Suala la Stakabadhi Ghalani, nina mambo mawili kwenye suala hili.
Mheshimiwa Spika, kwanza, ni lazima kwa either ni wadau ama mtu mwingine yeyote, wanapokwenda kujenga maghala haya wasiyajenge mjini, wajenge vijijini ambako ndiko wananchi wanakolima na ndiko mazao yao yalipo, ili tuweze kuwasaidia wakulima wetu kutokupoteza mazao mengi wakati wa usafirishaji.
Mheshimiwa Spika, maghala yakiwa kule, mazao ya hawa wananchi hayatapotea kwa sababu watakuwa wanapeleka eneo ambalo ni karibu, lakini wakiyapeleka huku mjini kwa kweli kusafirisha kutoka mashambani mpaka kuyafikisha kwenye haya maeneo ya maghala gharama inakuwa ni kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Viwanda, wanapokwenda kujenga maghala ama kuhamasisha wadau kutujengea maghala, waende wakajenge maeneo ambayo wakulima wanapatikana.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusiana na suala la mazao yanayokwenda kwa msimu kwenye mfumo wa Stakabadhi Ghalani, ama yatakayouzwa kwa kutumia mfumo wa Stakabadhi Ghalani. Mfumo huu ni mzuri, na tunatamani Watanzania wote leo kwa mazao yote yaweze kutumia mfumo huu ili wakulima wetu waweze kupata tija ama waweze kupata faida.
Mheshimiwa Spika, changamoto iliyopo, elimu bado iko chini sana. Kwa hiyo, tunaomba, Serikali, Wizara ya Viwanda pamoja na Wizara ya Kilimo watusaidie. Kwa mfano, sasa hivi wakulima wetu ndio wako kwenye msimu, wanalima. Tunaomba Serikali ianze kutoa elimu, iwaambie ni mazao gani msimu huu yataingia kwenye mfumo wa Stakabadhi Ghalani.
Mheshimiwa Spika, Serikali iwape elimu, na pia bei zitakazouzwa kwenye huo Mfumo wa Stakabadhi Ghalani badala ya kwamba wakulima wameshajilimia, wamemaliza, wakitaka kwenda kuuza kwa bei fulani, Serikali inakuja kuleta watu kununua kwa bei nyingine. Hiki kitu kinaleta mkanganyiko na inakuwa siyo sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, mtu anakuwa ameshajipangia kwamba naenda kuuza leo, nikafanye mahitaji yangu fulani, wewe unaenda unamzuia ndani ya wiki, wiki mbili, mwezi hujamlipa fedha yake. Inakuwa siyo sawa, na hatuwatendei haki wakulima. Kwa hiyo, naomba Serikali ianze elimu leo, itangaze mazao ya msimu huu yatakayokwenda kuuzwa kwa Mfumo wa Stakabadhi Ghalani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo natamani kulisema ni suala zima la ununuzi wa scanner kwenye mipaka yetu yote. Tuna mipaka mikubwa tisa. Kati ya mipaka hii tisa, tuna mpaka mmoja tu ndiyo wenye scanner, ambapo ni mpaka wa Tunduma. Mipaka yote haina scanner, bandarini hakuna scanner.
Mheshimiwa Spika, ukosefu wa scanner unasababisha moja, kupoteza mapato ndani ya Taifa letu; pili, mizigo, namna ya ukaguzi, tunafungua kontena, tunaanza kufungua kama ni friji tushushe moja moja. Pia, uingizaji wa vitu fake ambavyo vinaweza kuingia unakuwa ni mkubwa sana; tatu, kunakuwa na malipo yale ya wateja wetu ambao wameingiza mzigo kukaa kule bandarini kwa muda mrefu ama kwenye zile yard zilizowekwa kule pembezoni ambapo wao wanatakiwa kulipa baada ya mwezi mmoja.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba pia Wizara ya Viwanda kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, watoe fedha ili twende tukanunue hizi scanner ziweze kusaidia na ziweze kuleta tija kwenye ukusanyaji wa mapato, na urahisishaji wa kazi za viwandani pamoja na bandarini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la ununuzi wa meli kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Tangu nimeingia Bunge hili mwaka 2015 nilikutana na suala zima la ununuzi wa meli za uvuvi zikiwa nane; nne zikiwa zinanunuliwa upande wa Zanzibar, nne Tanzania Bara. Zikaja zikapungua tukaambiwa zitanunuliwa mbili. Leo zimepungua, tuliambiwa zinakuja nne, sasa tumeambiwa ni mbili, lakini hata hizo mpaka leo kimya.
Mheshimiwa Spika, tunaomba Serikali hebu shikeni hili, tusaidieni hizo meli zinunuliwe zije, changamoto ni nini? Kwa nini hizi meli hazinunuliwi? Shida iko wapi? Nunueni meli hizi ili tuweze kupata hayo mafao, tuweze kupata hizo fedha zinazopatikana kwenye hao samaki walioko bahari kuu.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni boti kwa ajili ya doria. Pia, kulikuwa na ununuzi wa boti kwa ajili ya doria kwenye bahari, mpaka leo nazo kimya. Shida iko wapi? Tusaidieni Wizara ya Fedha, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, tunaomba mshirikiane, nendeni kwa vipaumbele, ni kipi kinachotakiwa kuanza ili tuweze kupata nini? Tukinunua meli za wavuvi, tukanunua na boti za doria hakika tutapata mapato mengi na mambo mengine yataenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine nirudie tena kwenye suala la uanzishaji wa mamlaka za mifugo. Pia, tunaomba Serikali ianzishe mamlaka kwa ajili ya mifugo yetu ili tuweze kusimamia masuala mazima yanayohusiana na mifugo yakiwamo majosho na hata elimu kwa wafugaji wetu. Bado tunatamani sana tupate hii mamlaka ili ziweze kusaidia wafugaji wetu.
Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ni chanjo kwa mifugo. Wafugaji wetu wanatamani sana kupata chanjo ama mifugo yao iweze kupata chanjo. Changamoto kubwa zilizopo ni uwepo wa chanjo fake na gharama za chanjo. Sasa naomba kwa wafugaji wetu na Wizara, mtusaidie. Moja, elimu kwa wafugaji. Pia kuwaelimisha kwamba chanjo zinazotolewa ni chanjo zitakazoleta tija kwa hao wafugaji. Pili, ni chanjo zitakazoleta tija kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, leo tunashindwa kuuza nyama nje kwa sababu tu wenzetu hawaamini kwamba mifugo yetu inatunzwa na inapata chanjo kwa namna gani? Kwa hiyo, tukipata chanjo na wananchi wetu wakipata chanjo, tutapata soko la nje. Kwa hiyo, tutanufaika sisi wafugaji, lakini litanufaika Taifa kwa maana ya kupata fedha za nje. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru kwa muda wako, ahsante sana. (Makofi)