Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ukerewe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kuwapongeza Wenyeviti wa Kamati zote mbili kwa uwasilishaji wao mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2025, Sura ya Tano, Ibara ya 105 inaipa jukumu Serikali kusimamia amani na usalama wa Taifa letu. Inatoa jukumu hili kwa sababu kuna uwiano mkubwa sana kati ya amani na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutekeleza vizuri sana Ilani yetu ya uchaguzi. Mheshimiwa Rais amefanya uwekezaji mkubwa sana kwenye vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, ndiyo maana leo Taifa letu lina hali iliyo shwari. Sisi Kamati tumepitia mambo mbalimbali, tumejiridhisha hali ya ulinzi na usalama wa Taifa letu inaridhisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna hatua kubwa sana ya mabadiliko chanya kwenye vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Ndiyo maana siyo ajabu leo hii Mataifa mbalimbali na viongozi wa Mataifa mbalimbali hawaoni kigugumizi kuja Tanzania kutembelea, lakini hata kushiriki mikutano mbalimbali ya Kimataifa inayofanyika kwenye Taifa letu. Nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo mazuri sana yanayofanyika, nalipongeza Jeshi la Polisi, wanafanya kazi kubwa sana. Hii ni kutokana na uwekezaji mkubwa ambao Serikali imewekeza kuhakikisha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinafanya kazi zake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza linafanya vizuri pamoja na changamoto zake; na Uhamiaji wanafanya vizuri. Nimekuwa nazunguka kwa siku kadhaa kwenye mji wetu wa Dodoma, lakini hata miji mikuu mingine naona Jeshi la Polisi watu wake wako kwenye kila kona wakiwa na vifaa kwa ajili ya kuhakikisha Taifa letu linakuwa salama. Niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais na vyombo vyote vya ulinzi na usalama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na haya ambayo ni mazuri, bado kuna changamoto ambazo tunatakiwa tuzifanyie kazi. Majeshi yetu yanafanya kazi vizuri, lakini kuna mabadiliko makubwa sana ya kijamii. Kuna ongezeko la watu, kuna mabadiliko ya teknolojia na mabadiliko mbalimbali ya kijamii yanayotokea. Jambo hili linasababisha kuwe na uhitaji mkubwa wa vifaa vya kisasa na kisayansi kwa ajili ya kufanya upelelezi na kufanya uchunguzi wa kisayansi ili kuweza kukabiliana na uhalifu wa kisasa tofauti na huko tunapotoka.
Mheshimiwa Spika, leo kwa mfano Jeshi la Polisi lina vifaa ambavyo kwa uwekezaji uliofanyika na Serikali, wanafanya shughuli zao, lakini bado vinahitajika vifaa vya kisasa vya kiupelelezi na kiuchunguzi ili kuweza kuendana na mabadiliko ya kisasa na mabadiliko ya kisayansi. Pia, kama nilivyosema, kwa ongezeko la watu, ukosefu wa ajira unafanya kuwe na makosa mengine mengi sana yanayotokana na changmoto kama hizo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sisi Kamati tuliona bado kunahitajika uwekezaji mwingine mkubwa ili kuhakikisha majeshi yetu, hasa Jeshi la Polisi linapata vifaa vya kisasa ili kuweza kukabiliana na changamoto hizi zinazotokana na mabadiliko ya kidunia.
Mheshimiwa Spika, amesema Mheshimiwa Zahor, bado kuna upungufu wa vifaa hasa magari kwenye majeshi yetu. Jeshi la Magareza kwa mfano lina upungufu mkubwa wa magari, Jeshi la Zimamoto lina upungufu mkubwa wa magari, hasa ikiwa ni pamoja na boti za uokoaji, vitu ambavyo ni muhimu sana kwa shughuli zao na ukizingatia kwamba jamii yetu kwenye Taifa letu kuna changamoto kadhaa zinatokea majini na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kupatikana kwa vifaa hivi kutafanya majeshi yetu yaweze kufanya kazi zake vizuri. Kwa hiyo, naomba Serikali pamoja na mipango na mikakati iliyopo, lakini bado kunahitajika uwekezaji mkubwa kwenye majeshi yetu ili waweze kupata vifaa vya kufanyia kazi kwa ubora mkubwa zaidi.
Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuunda Tume ya Haki Jinai. Jambo ambalo limeboresha sana utendaji kazi wa majeshi yetu na kutoa haki kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo, nitoe rai kwa wananchi ili kuweza kufanya vyombo hivi viweze kufanya kazi zake vizuri hasa Jeshi la Polisi, wananchi watoe ushirikiano kwa kutoa taarifa za uhalifu kwa majeshi yetu ili majeshi haya yaweze kufanya kazi yake vizuri na kufikia lengo tulilolitarajia kulingana na maelekezo ya ilani yetu, Mheshimiwa Rais aweze kuendelea kutenda majukumu yake kwa ubora mkubwa ili kuhakikisha kwamba majeshi haya yanafanya kazi yake, yanalinda amani na Taifa letu linaendelea kuwa kinara kwenye ukanda huu na dunia nzima kama kisiwa cha amani.
Mheshimiwa Spika, yangu yalikuwa ni hayo machache, nashukuru kwa nafasi, Mwenyezi Mungu akubariki sana.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)