Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Amb. Liberata Rutageruka Mulamula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. BALOZI LIBERATA R. MULAMULA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia kwenye Taarifa ya Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kama ilivyowasilishwa vizuri na kwa ufasaha na Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Vita Kawawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aidha, naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna anavyoikuza diplomasia yetu ya Tanzania. Pia, napenda kumshukuru kama Amiri Jeshi Mkuu kwa kuhakikisha kwamba nchi yetu iko salama na imara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuchangia taarifa ya Kamati hii kama Mjumbe, naomba nikushukuru wewe binafsi kwa kunipangia Kamati hii ambayo inahusika na masuala ya diplomasia, masuala ya usalama na ulinzi, eneo ambalo nimehudumu kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natambua umuhimu wa Kamati hii katika kusimamia utekelezaji wa kazi za Wizara husika, katika kukuza mahusiano ya Kimataifa, kulinda amani na usalama wa nchi yetu na watu wake.

Mheshimiwa Spika, bila kupoteza muda, naomba kwanza niunge mkono hoja ya Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Pia, nakubaliana na taarifa na mapendekezo kama yalivyowasilishwa na Mwenyekiti wetu.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuongeza mchango wangu kama Mjumbe wa Kamati, katika maeneo matatu. Moja, inahusu diplomasia yetu ya Uchumi; pili, amani na usalama kwenye kanda yetu ya maziwa makuu; tatu, muda ukiruhusu nitagusia masuala ya mtangamano wa kikanda, yaani Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC kwa ajili ya tafakuri ya Bunge na kuishauri Serikali yetu ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba kuipongeza Serikali na Wizara husika kwa taarifa walizotupatia kwenye Kamati pamoja na ziara za mafunzo na semina zilizotolewa na taasisi mbalimbali za Wizara hizo tatu, katika kutuelimisha kuhusu utekelezaji wa majukumu yao na mipango ya maendeleo katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, niseme tumepata wasaa wa kupokea taarifa za Wizara hizo tatu na kuzichambua. Niseme katika utekelezaji wa Maazimio ya Bunge, hatua mbalimbali zimechukuliwa na inaashiria kuna mwitikio mzuri wa kuyatekeleza na pia kuna changamoto kama zilivyoainishwa na Mwenyekiti wetu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu diplomasia ya uchumi, naomba kwanza nimpongeze sana kwa dhati Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, mwanadiplomasia namba moja kwa kuipaisha diplomasia yetu ya uchumi kwa maono yake, kwa wepesi wake wa kufanya ziara mbalimbali nje ya nchi, kwa kujenga na kukuza mahusiano na nchi mbalimbali duniani na mashirika ya Kimataifa, pamoja na kuhamasisha uwekezaji na kujenga mahusiano mazuri ambayo yamechochea kupata misaada mingi sana katika kujenga uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aidha, naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuvutia mikutano mikubwa ya Kimataifa nchini, ikiwemo Africa Energy Summit iliyomalizika juzi ambayo ilihudhuriwa na viongozi wa juu wa nchi kutoka Bara la Afrika na duniani kote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii imeonyesha kutambulika na kuheshimika kwa Rais wetu, na kukubalika ulimwenguni kote. Hakika mwenye macho haambiwi tazama, kama Waingereza wasemavyo, “it is economic diplomacy at its greatest height and at its best.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba pia niwapongeze Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo na Manaibu wake, Mheshimiwa Cosato Chumi, Mbunge; namwona na Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo pamoja na Mabalozi wetu na Watumishi wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuendeleza diplomasia yetu ya uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo, tathmini ya Kamati kutokana na taarifa tulizopokea zinaonesha wazi kwamba, bado kuna uelewa mdogo kwa wadau hususan sekta binafsi na wanaNchi kwa ujumla kuhusu manufaa ya diplomasia ya uchumi na fursa nyingi zinazotokana na mtangamano na mahusiano yetu ya Kimataifa.

Mheshimiwa Spika, tumeona kwamba, Wizara kwa kweli inahitaji kufanya mawasiliano makubwa kuweza kuhamasisha hasa sekta binafsi kuweza kuchangamkia hizi fursa. Kwa mfano, utakuta kwamba, pamoja na kuwa Sudan ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, lakini wengi hawajui kwamba huku nako kuna soko. Pamoja na matatizo yao, kuna soko kubwa la mchele na mahindi, lakini wanafikaje?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sisi kama Kamati tumeshauri kwamba Wizara ikishirikiana na Wizara nyingine za kisekta, zije na mkakati wa kuweza kuelimisha wananchi wetu kuhusu hizi fursa zilizopo.

Mheshimiwa Spika, pia, tumesikitishwa na vikwazo visivyo vya kikodi vinavyoendelea, pamoja na kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki imetoa mwanya na soko huru, lakini juzi tulikuwa mpakani Mtukula tumekuta mlundikano wa malori ya mizigo na magari mapya ambayo yametoka bandarini kwetu kwenda Uganda hayajavuka. Kwa kweli tunasema kwamba, pamoja na kuwa na One Stop Center au Border Post, lakini bado kwa kwa kweli kuna changamoto nyingi sana.

Mheshimiwa Spika, vikwazo ni vingi na ukipita kwenye barabara ya kutoka Mtukula mpaka kwenda Bukoba utakuta kwamba bado kuna vizuizi vingi sana ambavyo vimekuwa ni kero sana. Kwa hiyo, niseme pia kwamba pamoja na juhudi za Mabalozi wetu kuimarisha diplomasia ya Uchumi, lakini wengi bado wanalalamika sana kutojibiwa wanayopeleka kwenye Wizara mbalimbali na Serikalini. Kwa kweli inawakatisha tamaa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nami nasema kwamba Diplomasia ya Uchumi haitekelezwi na Balozi zetu peke yake au Wizara ya Mambo ya Nje, bali inahitaji ushirikiano wa sekta zote, na Wizara zinazohusika kama vile Wizara ya Viwanda na Biashara, Uwekezaji na Mipango. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nihitimishe kwa kusema kwamba Diplomasia ya Uchumi ni muhimu kuanzia ndani kwanza, kana kwamba wasemavyo, foreign policy is an extension of domestic policy. Kwa hiyo, nashukuru sana kwa fursa hiyo na ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)