Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia Taarifa za Kamati mbili; hivyo, kwa sababu ya faida ya muda, nitachangia sekta za kiuzalishaji kilimo na mifugo. Nikijaliwa kidogo nitajikumbusha kama bado biashara naifahamu.

Mheshimiwa Spika, nami nitajikita kwenye kuungana na Kamati, lakini nitaungana nao baada ya kufanya marekebisho. Sitaungana nao kijumla jumla, lazima nitoe mapendekezo yangu. Hata hivyo, kuna uandishi mzuri uliyoonyesha mafanikio na changamoto. Nianzie kwenye mafanikio. Binafsi, nafarijika kwa mafanikio tuliyoyapata kama nchi kutokana na zao la kahawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulizoea kuuza kahawa nje ya nchi na kupata dola bilioni 240, lakini kwa mujibu wa taarifa za Kamati, tumepata dola milioni 791. Hii ni kazi kubwa imefanyika, na nitaelezea tumefikaje hapo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kilichokuwa kinaniuma zaidi, siyo kupata mapato zaidi, ila mafanikio ya jirani yetu nchi ya Uganda, wamepata dola bilioni 1.14. Sasa namwambia Mtumishi wa Bwana, hawa watu unawakamata, huhitaji muda mrefu. Uganda tutafika huko, kwa sababu, mwaka 2024 walipata dola milioni 800, na mwaka huu wamepata dola bilioni 1.14. Hivyo, nawe unaweza ku-leapfrog na kufika huko ndani ya miaka miwili, au mitatu. Mtumishi wa Bwana, unajua nilikuwa silimi kahawa, lakini mwaka huu nimepanda miche 2,600, na kufika Desemba tapanda miche 5,000. Hivyo, nitakuwezesha kufika hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumefikaje hapo? Tumefika hapo baada ya Mheshimiwa Rais, kwa juhudi zake binafsi, kuweza kufungua soko la China. China sasa wanakwenda kunywa kahawa ya Tanzania, kutoka Kagera, Muleba.

Mheshimiwa Spika, hivyo, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa jambo hilo alilotutendea. Pia niwaeleze kuwa nimeyasikia mapendekezo ya Kamati. Baada ya bei ya kahawa kuwa nzuri, hakuna cha uhamasishaji. Mtu asichukue fedha yako kwamba anakwenda kuhamasisha. Bei ambayo Mheshimiwa Rais aliwezesha kupatikana, ni hamasa tosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine niliyoyaona sijui hayajaandikwa vizuri! Hapa ni haya yanayo-trend leo kwamba sisi tumezalisha tani milioni 11 za mahindi kutoka tani milioni sita tulizokuwa tunapata. Pia, tumekuwa tukijadili kama Bunge, tukiongozwa na Kamati hii. Mojawapo ya maeneo yaliyotuletea mafanikio, ni ile ruzuku ya mbolea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nami mapendekezo yangu kwa Serikali kwamba tusiishie kuwa wa pili, hoja yangu siyo kuwa wa pili. Kwa imani yangu, nimeshamwambia Mheshimiwa Waziri anayehusika, tunaweza kuzalisha tani milioni 30, inawezekana.

Mheshimiwa Spika, tani milioni 30 inawezakana, na hapo ndiyo tutatengeneza synergy ya kufungamanisha mifugo na kilimo, kwa maana ya chakula, kwamba wananchi wanaweza kula hayo mahindi, lakini tunaweza kutumia mahindi na by-product za mahindi kulisha mifugo yetu. Hivyo ili tu-take advantage ya kuweza ku-export mifugo katika nchi za Ghuba ambazo zinahitaji nyama ya Tanzania ya wanyama wadogo wadogo kama mbuzi, kondoo, na ng’ombe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimewahi kusema na ninarudia kusema potential ya soko la nyama Ghuba ni dola bilioni tisa. Kama Tanzania, tungeweza kupata nusu yake, tungefika pale tunapopaswa kuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nazungumzia Sekta ya Sukari na natumia fursa hii kuipongeza Wizara kwa kile kitendo cha kuihamasisha TEMDO. TEMDO, kile kiwanda chao siyo kiwanda kidogo. Vile tulikuwa tunaviita Viwanda Ngazi ya Tarafa, yaani mnaweza kuwanacho kwenye yale maeneo oevu yanayoweza kulima miwa, na kila tarafa inakuwanacho hicho kiwanda. Hiyo ndiyo mojawapo ya sekta ambazo unaona zitatupeleka kuwa na utoshelevu wa sukari ya kutosha.

Mheshimiwa Spika, potential ya sukari Tanzania ni tani milioni mbili tuki-explore shughuli zote. Mwenyekiti wa Kamati amekaa mbali nami, alijua nitazungumza naye. Hoja ya white sugar na Industrial sugar ni tofauti. Hoja ya Industrial Sugar siyo miujiza, ni kwamba hatuna sukari ya kutosha. Kwa hiyo, huwezi ku-refine sukari kwanza ili kupata industrial sugar.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, suluhisho ni kuzalisha sukari nyingi kama tulivyozungumza, Viwanda vya TEMDO, hivi vya kuzalisha tani 4,000, au 5,000. Tulianza na Manyara ambapo walikuwa na tani 2,000 kwa mwaka. Leo wameshapanda. Kwa hiyo, Serikali sasa tuwasukume hawa watu. Ili kumsukuma, lazima umlinde. Kama una msukuma, lakini humlindi, utamuua kwa pressure, yaani atapata kiharusi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lazima mtu unapomwambia kajenge kiwanda, umhakikishie kwamba utamlinda. Kama unataka kumuua mtu, usitafute sumu, mwambie anzisha kiwanda, halafu usimlinde. Atakufa immediately na atajuana na Mungu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo ninalowaambia kuhusu viwanda vya sukari. Nimefurahishwa huu Mpango wa Sukari wa Miaka Kumi na Mbili, tunakaribia kufika pale tulipopaswa kuwa. Pia, nafurahi kazi ya Rufiji, wameanza kulima. Nafurahi tumeanza kufanya kazi Songea, nafurahi Kigoma Sugar ya Kasulu inaanza kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumze kidogo kuhusu uvuvi. Imesemwa changamoto ya uvuvi, lakini nyingine Mwenyekiti hakuziandika. Changamoto yetu sisi wavuvi ni magugu maji, na mnajua nina square kilomita 7,200 za Ziwa Victoria na Uvuvi wa Samaki ni Ziwa Victoria. Hivyo magugu maji yanaua samaki kwa kiwango kikubwa na haijaandikwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napendekeza uwatume Wajumbe wa Kamati weekend hii waende wakaangalie magugu maji, tunakwisha! Hakuna samaki, hakuna navigation, tunakwisha na magugu maji. Mwenyekiti unapohitimisha, uombe Spika akuruhusu ukaangalie magugu maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la uvuvi haramu, Kamati imependekeza udhibiti. Nani anadhiti uvuvi haramu Tanzania hii? Hakuna anayedhibiti, na sisi wanasiasa ni wahanga. Kila unapojaribu kusema udhibiti, unakuwa mhanga.

Mheshimiwa Spika, tulipendekeza kwamba ianzishwe Mamlaka ya kudhibiti ziwa, tudhibiti magugu. Nchi jirani kwa Mjomba, ziwa linalindwa kwa bunduki na kofia zao zimeandikwa UA. Huwezi kugusa samaki. Samaki wa Uganda ukiwekewa kwenye sahani, inabidi uwaambie watu wafiche simu zao wasipige picha, samaki ni mkubwa. Lazima tulinde Ziwa ili tulinde viwanda vyetu. Viwanda vyetu havina kazi vinavyofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu Sekta ya Chai. Mheshimiwa Waziri, nenda kwenye niche bucketing, soko la chai huko duniani limeharibika, lazima hawa watu uwasimamie, lakini uwalinde waende kwenye niche marketing. Wakienda ovyo kwenye Soko la Dunia, wanakwenda kutafuta stroke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nipongeze shamba letu la Binengo, mwekezaji aliyeletwa anaelewa na amekuja kwangu, nimemshauri namna ya kufanya, lakini niche marketing ni muhimu. Bila kwenda kwenye niche marketing soko la dunia haliko salama sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuzungumzie mazingira mazuri ya biashara. Kweli nawapongeza Kamati kwa kuzungumzia cargos scanner, na nilizungumza hapa juzi na Waziri wa Fedha, alisema cargos scanner inataka kujengwa Mtukula, lakini tumechelewa. Pamoja na mizigo kutafuta ushuru, lakini wepesi wa kufikisha mzigo kwa mteja ndiyo unafanya Tanzania tuweze kupendwa, watu wapende Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mtumishi anajua, hata Rais wa nchi fulani ameamua kuwa promoter wa mchele wetu, akisema mchele mzuri duniani uko Tanzania. Sasa, kama unapigiwa kampeni na mtu mkubwa namna hiyo, basi ondoa urasimu, ondoa vikwazo kusudi bidhaa iende sokoni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hayo mawili, naunga mkono hoja kwa marekebisho hayo niliyoyatoa. (Makofi)