Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza wawasilishaji wetu wawili kwa taarifa zetu hizi mbili za leo za Kamati tunazozijadili. Ninazipongeza Wizara zote zinazosimamia sekta mbalimbali katika Kamati zetu hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianzia na Sekta za Kilimo, Mifugo, Viwanda na Biashara tumegundua kwamba, kuna sheria nyingi ambazo zinakinzana kati ya sheria za sekta na sekta nyingine. Pia, sheria hizi zimepitwa na wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuna sheria ambazo haziendani na teknolojia ya sasa. Naomba sana hatua zichukuliwe kurekebisha sheria hizi ili twende na kasi ya maendeleo na ukuzaji wa uchumi katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya kilimo ninasisitiza kama ushauri wa Kamati ulivyosema kwamba, huduma za ugani, ule uwakala uharakishwe ili uanze kazi. Sambamba na hilo, kuajiri zaidi Maafisa Ugani wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea, kuna Vituo vya Rasilimali vya Kilimo vya Kata. Vituo hivi vipo kwenye kata zetu na maeneo yote ya nchi, lakini ukweli ni kwamba havifanyi kazi inayokusudiwa. Vituo hivi vinafanya kazi nyingine ambazo hazimsaidii mkulima kama lengo lililokusudiwa kuanzisha kwa vituo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ushauri wa Kamati unavyosema, vituo hivi vimebadilishwa matumizi. Kama Kamati ilivyoshauri, nami ninaongezea hapo kwamba vipelekwe kwenye Wizara ya Kilimo ili vikafanye kazi iliyokusudiwa na Wizara ya Kilimo ifanye kazi ya kuviendeleza zaidi, kuviwekea miundombinu na vifaa vya kisasa ili vitoe huduma za ugani na mafunzo ya kilimo kama ilivyokusudiwa. Uwekezaji mkubwa umefanyika, lakini kazi iliyokusudiwa haifanyiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kwenye huduma hizi za kilimo cha umwagiliaji maji, ni muhimu sana. Ninashauri kama ilivyosema Kamati, tuongeze kuajiri wataalamu wa umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatenga fedha nyingi kwa ajili ya umwagiliaji, kujenga mabwawa, lakini tuna uhaba wa wataalamu wa elimu ya umwagiliaji. Hapa tutaokoa fedha nyingi za Serikali kuona miradi hii inafanya kazi iliyokusudiwa na inatoa huduma za kilimo bora kwa wakulima na wananchi wetu ambao tuna hamu ya kujifunza kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta ya mifugo, hamasa kubwa iwekwe kwenye kuongeza viwanda vya usindikaji maziwa, ili tuweze kunusuru upotevu wa maziwa tulionao hivi sasa. Pia, tutaongeza ajira kwa vijana wetu na pato la Taifa kwa kupunguza uagizaji maziwa kwa fedha za kigeni ambazo tunazo hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto, tunampongeza mwekezaji wa ndani Ndugu Asas kwa kuanzisha kiwanda kikubwa sana cha usindikaji wa maziwa ya unga, lakini changamoto iliyokuwepo maziwa ya unga na bidhaa ambazo zinazalishwa na maziwa, kwa mfano jibini na vitu vingine, inaonekana kama ni maziwa ya anasa au ya kujistarehesha. Kwa hiyo, kodi imekuwa kubwa sana, ambapo uzalishaji na uunzaji wa maziwa unakuwa changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maziwa ya unga ni chakula kama maziwa mengine, kwa sababu wananchi wetu, sio wote wana majokofu ya kuhifadhi maziwa ya kawaida. Wakinunua maziwa ya unga wakayaweka ndani, wanaweza kuyatumia mwezi mmoja mpaka mitatu. Kwa hiyo, ile hali ya kuwa na lishe bora itakuwa inakwenda sambamba na yule ambaye anatumia maziwa ya maji na unga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa hivi dunia imefunguka, wananchi wetu wanajua kutumia hivi vitu; jibini na vitu vingine. Sasa kodi inapokuwa kubwa, wanashindwa kumudu na hii itasababisha wawekezaji wengine washindwe kuja kuwekeza kwa sababu ya changamoto hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najielekeza kwenye uvuvi na hasa uvuvi wa Bahari Kuu. Naipongeza Serikali kwa dhati kabisa kwa kufikia hatua kubwa ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi kule Kilwa. Ni fahari kwa Tanzania, tutawekeza sasa kwenye uvuvi wa Bahari Kuu na tutapata fedha za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari yetu ya uvuvi inakaribia kukamilika, lakini bado meli za uvuvi hazijawa tayari. Ni vyema basi mambo haya yaende sambamba; meli za uvuvi na bandari yenyewe ya uvuvi, ili tuweze kufikia yale malengo tuliyoyakusudia na tunayoyatarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, Shirika la TAFICO liwekewe miundombinu na vitendea kazi vya kutosha ili liende sambamba na uvuvi wa Bahari Kuu kwa maana vitu vyote vitakuwa vimekamilika. Shirika hili limeanza zamani kufufuliwa, lakini bado uwekezaji wake unakuwa taratibu. Hofu yangu ni kwamba, tunawekeza fedha nyingi, lakini hatukamilishi. Kuna hatari sasa na vile vya mwanzo vikaharibika kabla hivi vya mwisho havijatokea. Tunachohitaji ni uzalishaji, tuwekeze hapa kwenye uvuvi wa Bahari Kuu, tuingize fedha za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo chetu cha Mbegani Bagamoyo kinakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo uchakavu wa majengo na miundombinu, na uchakavu wa vifaa vya kufundishia zikiwemo meli. Kwa hiyo, ni vyema chuo hiki kikapatiwa miundombinu hiyo ili wanafunzi wetu wapate ile fursa tunayoisema ya kujiajiri ili kupunguza changamoto hii ya ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, kwenye Chuo chetu cha Mbegani wanafunzi wapatiwe mikopo kama vyuo vingine vya kati. Sasa hivi kwenye chuo kile, wanafunzi hawawezi kupata mkopo, wanajifunza ujasiriamali wa kuvua na kufuga Samaki, lakini kwa sababu ya uwezo mdogo wa wazazi wao, wanashindwa kuomba kusoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, chuo hiki kinatakiwa sasa kiwe sambamba na vile vyuo vingine vya kati. Wapatiwe mafunzo hawa vijana waweze kujisajili na wakasome haya mafunzo ya ujasiriamali wa uvuvi na mambo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najielekeza kwenye sekta ya viwanda. Kuna Kiwanda chetu cha Kibaha cha Viuadudu. Uwekezaji mkubwa umefanyika, lakini bado kinakabiliwa na changamoto za madeni na vitu vingine. Nashauri tuendelee kuishauri Serikali kama maazimio ya Kamati, madeni yale yalipwe. Pia kipanuliwe zaidi ili kuzalisha dawa za viuadudu nyingine kwenye mazao ya kilimo, ili tuweze kuzitumia badala ya kuagiza vitu kutoka nje, kwani vingine vinakuja havina ubora, wakulima wetu wanapata hasara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna taasisi zetu kama CAMARTEC, TEMDO, KMTC, SIDO na TIRDO. Hizi ziongezewe bajeti kwa sababu tumeziona na tumezikagua. Tumeona utekelezaji wake, na hamu waliyonayo wafanyakazi wa sekta hizi, ni kutaka kuhakikisha kwamba Tanzania tunajitegemea kwa vifaa vyetu mbalimbali ambavyo tunavitumia humu nchini vikiwemo vya kilimo na viwanda vidogo vidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesikia hivyo viwanda vya sukari wanatengeneza majokofu. Sasa hivi wana mpango wa kutengeneza majokovu ya kuhifadhia barafu kwa ajili ya samaki wengi watakaovuliwa wakati wa uvuvi wa Bahari Kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwekeza hapa, tutarejesha fedha mara tatu au nne ya hizo ambazo tumewekeza na itatupunguzia Tanzania kutumia fedha zetu za kigeni za ndani kuagiza vifaa hivyo ambavyo wananchi wetu wana ujuzi na uwezo wa kuzalisha hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tuongeze bajeti na vifaa vya kutosha kwenye hizi sekta. Pia tuongeze wataalamu wa fani mbalimbali wa kutosha ili waweze kumudu kazi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nazipongeza Wizara zote hizi: Kilimo, Uvuvi na Viwanda. Serikali imeongeza bajeti kubwa katika sekta ya uzalishaji, lakini tumeona mafanikio na faida ya fedha hizo zilizowekezwa. Kilimo sasa kinakua, uvuvi unakua na ufugaji unakua pia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha na ninaunga mkono hoja. (Makofi)