Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Vincent Paul Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia taarifa yetu ya Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Kipekee nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuendelea kuviboresha vyombo vyetu vya ulinzi hasa kwa kuendelea kutoa ajira mpya ili kuleta ufanisi ndani ya vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nawapongeza Mawaziri wote wa Wizara tatu: Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Ulinzi pamoja na timu nzima ya Makatibu Wakuu na wataalamu wote kwa kuendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona mambo ya maendeleo wanayoyafanya na yanaonekana kwa macho, kuanzia vyombo vya usafiri ndani ya vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinaboreshwa kwa kasi kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Nkasi Kusini na Mkoa wa Rukwa. Jimbo la Nkasi Kusini Mheshimiwa Rais ametufanyia mambo makubwa sana ya maendeleo. Jimbo la Nkasi Kusini kwa niaba ya wananchi, tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa sababu halikuwa na Kituo cha Afya hata kimoja. Mheshimiwa Rais ametujengea vituo vya afya sita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kata nne hazikuwa na barabara, Mheshimiwa Rais amefungua barabara mpya nane. Shule za Msingi mpya nne, vijiji 32 havikuwa na umeme, kote umeme umefika. Tunasema ahsante sana, 2025 wananchi wanasema wanaenda na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na usalama ndani ya Ziwa Tanganyika. Jimbo la Nkasi Kusini na Mkoa wa Rukwa unapakana na nchi nne: Burundi, Zambia, Congo hadi Mpaka wa Rwanda Kigoma huko. Kuna changamoto kubwa sana ya usalama ndani ya Ziwa Tanganyika. Wavuvi wetu wanaokwenda kufanya shughuli za uvuvi, wanavamiwa na kunyang’anywa nyavu zao, fedha na rasilimali hadi kuvuka upande wa pili wa Tanzania, wanapata hasara sana wanapovamiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Wizara ya Ulinzi. Niliomba ujenzi wa Kambi ya JKT Tarafa ya Wampembe, katika Taarifa yao wameiweka. Naomba Kambi hii ianze kujengwa mapema kwa ajili ya usalama ndani ya Ziwa Tanganyika. Vilevile, Barabara ya Wampembe ipandishwe hadhi iwe barabara ya kiulinzi, ikarabatiwe wakati wote; masika na kiangazi, iweze kupitika ili ulinzi Ukanda wa Ziwa Tanganyika ufanyike kwa sababu kuna uhalifu wa mara kwa mara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Wizara ya Mambo ya Ndani, niliomba ujenzi wa Kituo cha Polisi Kata ya Kala Kijiji cha Mpasa. Kituo cha Polisi Kata ya Mpasa kimejengwa vizuri, changamoto inakuja kwenye vifaa. Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani aliniahidi kupeleka boti Ukanda wa Ziwa Tanganyika, Kituo cha Polisi Mpasa, lakini mpaka sasa bado hazijafika. Naomba Mheshimiwa Waziri Bashungwa apeleke boti kwa ajili ya patrol ndani ya Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa yetu imegusia Jeshi la Polisi pamoja na Jeshi la Zimamoto. Kuna changamoto kwa Jeshi la Zimamoto kutokuwa na ofisi vijijini, na kwa sasa kuna ukuaji mkubwa sana wa vijiji pamoja na maendeleo yanayokuja na kasi ya ujenzi wa nyumba za umeme. Kwa hiyo kuna majanga yanayotokea mara kwa mara. Kuna majanga ya asili na majanga yasiyo ya asili. Upande wa umeme kuna majanga ambayo yanatokea ya moto. Jeshi la Zimamoto halina ofisi mpaka vijijini. Kwa hiyo, elimu kufika vijijini bado ni changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwenye vile vituo vya Polisi vya kisasa vilivyojengwa, Jeshi la Zimamoto lipewe nafasi na ofisi ili liweze kwenda kutoa elimu vijijini. Pamoja na hayo, Jeshi la Zimamoto liongezewe fedha ili lianzishe Kitengo cha Zimamoto Jamii, kwa sababu Zimamoto Jamii itaweza kufika hadi vijijini kutoa elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna majanga mengi yanayowapata watoto na vijana kama kuangukia kwenye visima na mito wakati wa masika, lakini elimu ya uokoaji bado kwa sababu Jeshi la Zimamoto ndilo tumelihuisha sasa hivi kuwa idara. Kwa hiyo, bado halijatanua wigo kufika hadi vijijini. Sasa, kupitia Zimamoto Jamii, vile vikundi vitapata elimu na vitaweza kuokoa mapema kabla jeshi halijafika kuokoa maisha ya watu, litafika mapema na jamii itakuwa sehemu husika ya tukio. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo biashara haramu ya binadamu, imekuwa ni biashara kubwa sana, inatishia, na watu wengi wanauzwa kimya kimya. Jamii hasa huko vijijini bado haijapata elimu. Naomba iundwe idara kamili ya kuweza kukabiliana na hii changamoto kwa sababu ni kubwa sana. Taarifa na elimu ya wale waliouzwa wakaokolewa, itolewe kwenye vyombo vya taarifa ya habari, TV na magazeti; na viongozi wapewe elimu na ishuke chini mpaka kwa Madiwani ili wananchi vijijini wapate elimu kwamba kuna biashara haramu ya binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya kata zipo kwenye mazingira magumu ambapo zinatakiwa zijengewe vituo vya Polisi. Kwa mfano, Kata ya Kate, wananchi wamejitolea, wamejenga lakini bado. Naomba Wizara hii itenge angalau shilingi milioni Hamsini hamsini kwa kila kata, ipelekwe ikaunganishe nguvu za wananchi kwenye hivi vituo vya Polisi ili wananchi wapate ulinzi katika vijiji vyao, kwa sababu uhalifu upo mara kwa mara kutokana na jiografia ngumu ya kata zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)