Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa nami niweze kuchangia katika taarifa hizi mbili. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha kuwa mahali hapa muda huu, kuweza kufanya kazi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa napenda kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya kama Amiri Jeshi Mkuu wa nchi hii ya kuhakikisha usalama wa nchi yetu uko sawasawa. Kwa hiyo, napenda nimpongeze kwa kazi hiyo na vyombo vya ulinzi na usalama viko sawa na mipaka yetu yote iko salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa, nampongeza Mheshimiwa Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuliongoza Bunge hili, kutuongoza vyema na kuhakikisha kwamba, Kamati zetu zinatoa taarifa ambazo zimefanyiwa kazi. Hongera sana kwa Mheshimiwa Spika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita katika Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, hasa katika kipengele kinachohusu biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu. Biashara hii ni kubwa kabisa duniani, ni biashara ya tatu kwa ukubwa duniani. Ninavyosema hivi ninamaanisha kwamba, kuna biashara nyingine, lakini hii ni kubwa sana na ipo. Watanzania wengi hatuelewi kwamba, ni biashara kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii biashara inatokana na mambo gani? Biashara hii inatokana na umaskini, kutokuwa na uelewa wowote, hali ngumu ya maisha na masuala mbalimbali ambayo mtu huna uelewa nayo, itakukuta biashara hii. Hii biashara hasa inawakuta vijana wengi na vijana wetu wengi wamekwenda wakipotea, wakipata adha, wakitumiwa ndivyo sivyo na kuweza kuhatarisha maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukulie mfano, kuna Watanzania wanaolaghaiwa, wanaambiwa kuna kazi nje ya nchi, kazi nzuri kabisa na anakuja anapewa maelekezo kwamba, hiyo kazi itamsaidia. Bila kujitambua, anaweza akauza vitu alivyonavyo akapata nauli na kwenda kule. Kumbe akifika anaenda kutumikishwa na hatimaye hawezi kurudi nyumbani, anakuwa hana nauli, hana anachoweza kufanya, hana mawasiliano, hana kila kitu. Hii inatokea, na tumeiona kwenye kamati yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara hii inafanyika ndani na nje ya nchi. Kwa ndani ya nchi kuna vijana wanachukuliwa, hata watoto wadogo wanachukuliwa, wanaletwa kwenye maeneo mbalimbali, iwe mijini au maeneo mengine. Wanapoletwa pale wanatumikishwa kazi kwa ujira mdogo sana. Wanapotumikishwa hizo kazi, unafikiri watalipwa kitu kizuri, wanajua wanaenda kupata ujira mzuri, kumbe wanaenda kutumikishwa ndivyo sivyo na yanawakuta madhara makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wenye ulemavu pia, wanaweza wakachukuliwa kutoka ndani au nje ya nchi wakaenda kutumikishwa. Unapoenda labda mtu anaomba, unafikiri unamsaidia, kumbe yule mtu ana watu, maajenti, nyuma ambao ndiyo wanapokea zile fedha baada ya yeye kupata ujira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii biashara ni kubwa mno na inatesa Watanzania walio wengi. Naipongeza Serikali, hasa chombo cha Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu, ikishirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama. Wameweza kubaini zaidi ya wahanga 1,110 ambao walikutwa na biashara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya hao, 902 walikutwa kutoka nje ya nchi, 208 kutoka ndani ya nchi na wahalifu 103 wanaofanya hiyo biashara walipatikana. Kwa hiyo, nawapongeza. Pamoja na kufanya kazi yote hiyo, lakini bado biashara hii imeshamiri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali, pamoja na juhudi kubwa wanazozifanya kwa chombo hiki cha Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Biashara Haramu, waweze kushirikiana vizuri na Wizara ya Mambo ya Ndani kuweza kufanya mambo yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, waweze kushirikiana kutoa elimu kwa jamii, watoe elimu kwenye halmashauri zetu, kwenye Wilaya zetu, kwenye vijiji vyetu, kwenye kata zetu na kwa jamii kwa ujumla iweze kujua. Watoe elimu ili wananchi wajue kwamba, kuna madhara kama hayo yanawakuta ili waweze kuwasaidia wananchi. Serikali iweze kutenga fedha za kutosha kuhakikisha chombo hiki kinatoa elimu, na pia wananchi wapate elimu hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaposema chombo hiki kipate fedha za kujiendesha, ni kwa kuwa kinahitaji kujenga eneo maalumu la hawa wahanga kuweza kupata masuala ya unasihi, kufanyiwa counselling kwa sababu, mtu akikutwa ametoka huko, anakuwa amechanganyikiwa. Kwa hiyo, hilo ni eneo ambalo wataweza kulijenga kusaidia watu kupunguza mawazo na changamoto zile, ili waweze kujiunga na jamii wakiwa salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la Wizara ya Ulinzi na Usalama na Jeshi la Kujenga Taifa. Nalipongeza Jeshi letu, limekuwa likifanya kazi kubwa sana kwa weledi mkubwa wa kulinda nchi yetu na mipaka yake, wanafanya kazi kubwa sana. Jeshi letu la Kujenga Taifa wameweza kufanya kazi kubwa ya kuchukua vijana wetu na kwenda kuwapa elimu hiyo ya kujitegemea katika maeneo mbalimbali, japo haitoshelezi, lakini wamekuwa wakifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, SUMA-JKT inadai mashirika na taasisi za umma na za binafsi shilingi bilioni 40. Pesa hizo ni nyingi sana. Wanashindwa kujiendesha katika mambo na mipango yao ambayo wamejipangia, wanashindwa kutekeleza huduma zao ambazo wameweka ziendelee. Kwa hiyo, deni hili ni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali iweze kuchukulia kwa umakini mkubwa kuhakikisha hilo deni linalipwa. Taasisi hizo zinazodaiwa ziwalipe SUMA JKT; na pia asasi za kiraia ambazo zimeikopa SUMA JKT zilipe hizo fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni miundombinu chakavu katika magereza na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Magereza zetu nyingi ni chakavu, na zilizo nyingi zimejengwa miaka 100 iliyopita ambao ni karibu 85%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaiomba Serikali ihakikishe kwamba, katika bajeti zake nyingi zinazotengwa, kuna fedha za kutosha za kuwasaidia ili Jeshi la Magereza waweze kukarabati majengo ili yaendane na wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri kuwe na mifumo ya TEHAMA na kuwe na maeneo ambayo watatolea urekebu. Kwa sababu, sasa hivi tunataka tutoe urekebu, kwa maana wale wafungwa waweze kupata mafunzo ambayo yatawasaidia wakitoka nje ya Magereza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, naishukuru Serikali, kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Jeshi la Uhamiaji kwa udhibiti wa wahamiaji haramu nchi hii. Wameweza kuanzisha programu inayoitwa mjue jirani yako, inayoendana na mazingira husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii programu imesaidia sana kwa sababu, wahamiaji haramu wamekuwa wakija nchini kwetu, wakijumuika na kuwa kama Watanzania. Kwa hiyo, hiyo ni programu ambayo Mheshimiwa Rais aliisisitiza na Jeshi letu la Uhamiaji limeweza kufanya hivyo. Tunalishukuru limeweza kufanya kazi kubwa sana. (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ni Majeshi ya Polisi na Zimamoto. Tunashukuru Jeshi la Polisi limepata magari, lakini magari hayo hayatoshelezi. Ni magari mazuri, mtawaona wanajeshi wamekuwa katika magari mazuri, lakini pia, wana uniforms ambazo zinaridhisha, lakini bado haitoshelezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lina upungufu wa magari 156, wana upungufu wa maboti 36 na pia, wana uchache wa vituo vya zimamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, lakini nawapongeza Mawaziri ambao wameweza kufanya kazi yao ipasavyo, ahsante. (Makofi)