Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Mohammed Said Issa

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Konde

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai na uzima na kusimama kwenye Bunge lako Tuku hili. Pia nakushukuru wewe kwa kunipa nafasi ili nami niweze kutoa mchango wangu katika taarifa za Kamati hizi mbili ambazo zimewasilishwa leo asubuhi mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze mchango wangu kwenye Wizara ya Viwanda. Kwanza naipongeza kazi nzuri wanayofanya TRA katika ukusanyaji wa mapato. Tumeona kwamba kila wakati mapato yamekuwa yakiongezeka. Nampongeza sana Mkurugenzi Mkuu au DG wa TRA kwa mbinu ambazo anakuja nazo, ambazo siyo za kulazimisha, lakini kodi inaongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote hayo, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Viwanda, Biashara, Kilimo, Uvuvi na Mifugo na nilibahatika kutembea katika sehemu mbalimbali. Tulitembelea kule Horohoro Tanga, tumekuta utendaji kazi siyo mzuri kutokana na kazi nyingi ambazo zinafanywa manually. Tuliona hamna scanner pale, na Horohoro ni mpaka mkubwa sana. Sasa tukaona kuna mambo mengi ambayo yanadumaza uchumi wetu pamoja na ukosefu wa mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili kwanza ni hatarishi kiusalama kwa sababu wale ambao wanakagua, hatujui kama ni waaminifu kiasi gani, lakini pili linatukosesha mapato kutokana na mambo ambayo yanaweza kufichwa pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo mipaka mikubwa 18, lakini mipaka ambayo ina scanner hizi kubwa ni mipaka mitano tu ambazo ni zile bandari zetu. Pia kuna scanner hizi ndogo ndogo ambazo wanapitia abiria, pia nazo ni tatizo. Sehemu kubwa ambazo zinahitaji scanner kubwa na ndogo, hamna nchini. Kwa hiyo, jambo hili lilitakiwa lipewe upeo wa hali ya juu kwa sababu linadumaza uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kutokuwepo kwa scanner, baadhi ya sehemu ni bugudha kwa wananchi. Nitoe mfano, siku moja niliuliza swali hapa kwa Wizara ya Uchukuzi kuhusu suala la ukaguzi wa mbwa kuwa ni wa kawaida pale bandarini Dar es Salaam; kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar. Nilijibiwa vizuri tu na Mheshimiwa Waziri, na akatoa agizo kwamba ukaguzi ule unatumika pale ambapo utahitajika, lakini ukaguzi mwengine ndiyo unatakiwa kufanywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha, watendaji wa bandarini pale Dar es Salaam wamekuwa wakilazimisha kukagua kwa mbwa. Sasa Mheshimiwa Waziri nataka atoe pia tamko, kwa nini katika jambo hili, Bunge linadharauliwa? Kwa nini Maazimio ya Bunge yanadharauliwa? Mbwa wale wanaendelea kubughudhi watu, wananusa chakula, wananusa nguo za ibada na watu wanashindwa kufanya ibada siku nzima. Huo ulikuwa ni mchango wangu wa kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, niende kwenye upungufu wa sukari. Mwaka 2024 tulikuwa na upungufu wa sukari na tulipata shida kubwa sana, na ilisababisha kutungwa sheria hapa, ili kuwapa mamlaka NFRA kuweza ku-control upungufu wa sukari. Jambo hili mimi sitaki nilizungumze kwa ukubwa sana, lakini napenda kutoa angalizo kwa Waziri wa Kilimo kwamba jambo hili liliichafua nchi, ilifikia mahali wananchi wakanunua sukari kwa kilo moja shilingi 10,000/=.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo tuliyoyachukua, muda unakaribia huu, tunapofika mwezi Mei, Juni na Julai viwanda vitafungwa. Uzalishaji wa sukari kwenye viwanda vyetu bado hautoshelezi. Maana yake ni nini? Tutahitajika kuwa na sukari ya ziada. Kwa hiyo, tusije tukaona kwamba sukari tena imepungua, tujiandae mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo alisema kwamba kutakuwa na bei elekezi. Bei hizi elekezi wanazijua wafanyabiashara tu, wananchi hawazijui. Tunaomba Wizara hii iweke wazi ili wananchi wajue bei elekezi, kwamba anakwenda kununua sukari dukani kiasi hiki. Siyo muuzaji tu, kwa sababu wauzaji kule wanaweza wakauza na mwananchi akaona kuwa ni sawa. Hii iwe public, watu wote wafahamu kwamba bei elekezi ni hii, ndipo italeta tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee na suala la upungufu wa fedha za kigeni. Kumekuwa na upungufu mkubwa wa fedha za kigeni. Katika jambo hili ningependa hasa huyu Mheshimiwa Waziri wa Fedha ajibu ni kwa nini fedha za kigeni zilishuka kwa muda wa wiki moja na zikapanda kwa muda wa wiki moja? Ni uchumi wa aina gani huu? Maana jambo hili sijui hata lilitokeaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi katika maisha yangu sijawahi kuona, lakini sijui ni terminology gani tunaweza tukau-term huu uchumi wa namna hii, kwamba wiki moja ilishuka kutoka 2,800 mpaka 2,360, lakini wiki moja ikapanda mpaka 2,600. Jambo hili linakuwaje? Nini kilitokea? Vyombo vya ulinzi na usalama vinatakiwa kuchunguza jambo hili, kwani suala hili siyo la kawaida. Hadi sasa hivi fedha za kigeni ukienda benki unakuta umeandikiwa bei za ununuzi na uuzaji, lakini hakuna. Kwa nini? Waziri wa Biashara hapo anaweza kutueleza ni kwa nini hakuna?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nije kwenye suala la mifugo. Kwanza naipongeza Serikali kwa kuweka mkazo kwenye suala la chanjo. Jambo hili ni zuri na litatusaidia kupata fedha za kigeni kwa kuwa tutauza nyama yetu nje. Tunajua kwamba nyama haiuzwi nje. Wananchi huwa wanakataa kuchanjwa mifugo yao kwa sababu ya elimu, lakini siyo elimu tu, hata watendaji wetu wanaochanja kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukisikiliza wadau mbalimbali; mtu unakwenda kuchanja mfugo ambao tayari ulishaathirika na magonjwa. Maana yake ni kwamba unauongezea dozi na hivyo unakwenda kufa. Mwananchi hatakubali. Au mfugo ambao una mimba, ule hauwezi tena kuendelea. Matokeo yake wananchi wanaona kwamba chanjo hizi ni shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi ombi langu kama Mjumbe wa Kamati ni kwamba Serikali iende hatua kwa hatua kwenye kutekeleza jambo hili, wasikurupuke tu kwamba yoyote tu achanjwe Iende na elimu nzuri ya kuwasaidia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusiana na uvuvi haramu. Tumezungumza kwenye Ripoti ya Kamati hapa. Suala la uvuvi haramu Serikali ijikite kuuzuia kwenye deep sea. Tumeelezea kwa upande wa Zanzibar, Serikali inashirikisha vyombo vya KMKM, Kikosi cha Kuzuia Magendo pamoja na Navy lakini pamoja na Uchumi wa Bluu. Hili ni jambo zuri kwa sababu Serikali ni moja, ni Serikali ya Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwetu Zanzibar hili jambo halikueleweka. Mimi jimboni kwangu asilimia kubwa ni wavuvi, ni bahari, lakini jambo la kushangaza ni kwamba, wananchi ambao miaka nenda miaka rudi wanavua katika uvuvi wa kawaida, wamezuiwa kuvua sasa hivi, na hivyo hawana kazi. Hatujui kazi gani za kufanya. Halafu CCM wanatafuta kura kule, watazipata wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwetu hawawezi kupata kura kwa sababu huu uchumi ambao wanatuletea siyo rafiki. Wao wakiwa na nia ya kupata kura, labda waje watupige bakora, lakini kura kule kwetu Jimbo la Konde na Pemba yote CCM hawana kura kwa sababu hii.

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, otherwise, waweze kujisahihisha. Acheni, tulieni, sisi tunaendelea.

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Asha.

TAARIFA

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nimfahamishe msemaji kwamba kura tutapata, tena za kishindo. (Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mohamed Said Issa, unakubali na unaipokea taarifa hiyo?

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa yake siipokei, na huyu Mheshimiwa ni mama yangu, lakini huo ndiyo ukweli. Ni kwamba kule sera zao CCM ni mbovu. Kwa hiyo, hawatapata kura. Waniache niendelee, otherwise, wabadilishe sera. Wakibadilisha sera hizi za kuwashirikisha wananchi, kwa sababu tunajua kwamba kwenye huu uvuvi nyavu zinanunuliwa wapi na wapi; mishipi, na uvuvi ni ule ule wa kawaida.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba dakika moja nizungumze kuhusu vitambulisho vya NIDA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vitambulisho vya NIDA vimekuwa ni shida, na vinasababisha watoto wetu ambao wanataka kupata mikopo ya elimu ya juu kushindwa kuvipata. Sasa jambo hili ni la kuwekewa mkazo. Hili ni tatizo lingine ambalo pia litasababisha matatizo kwenye uchaguzi wetu. Kwa sababu kule Zanzibar, hii Tume ya Uchaguzi inatumia vitambulisho hivi, lakini kwa kumpa Mamlaka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar yenyewe haijitambui, inatoa vitambulisho. Kule Jimboni kwangu vitambulisho vya Tume ya Uchaguzi zaidi ya 380 havisomi kwenye mfumo. Sasa ni Tume ya Serikali hiyo au Tume tu ni kikundi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, jambo hili Serikali ya Muungano imekasimu…

MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. MOHAMED SAID ISSA: …madaraka yake kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inaharibu kabisa uchaguzi wetu wa Zanzibar.

MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ACT tumejipanga kushinda uchaguzi huu, lakini kwa ghiliba hii itakuwa na shida.

MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Rashid.

TAARIFA

MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa kwamba Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ni Tume inayojitambua, ina wafanyakazi weledi, watendaji weledi. Kwa hiyo, naomba achukue taarifa hiyo kwamba Tume inajitambua. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mohamed Said unakubaliana na taarifa?

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sikubaliani na taarifa. Mimi nimetoa data, na akitaka twende nimkusanyie watu hao ambao vitambulisho vyao havijasoma kwenye mfumo. Kwa hiyo, ile Tume haiwezi kufanya kazi zake kwa weledi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)