Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hanang'
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia kwenye taarifa za Kamati zetu mbili. Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na Kamati ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nianze kwa kupongeza Kamati zote mbili kwa jinsi ambavyo wanasimamia Wizara za kisekta na Wizara zinafanya kazi nzuri kwa sababu ya kazi nzuri ambayo Kamati zetu zinafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mara yangu ya kwanza ninasimama hapa Bungeni baada ya kuwa uteuzi umefanyika wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Mgombea wa nafasi ya Urais kupitia Chama cha Mapinduzi kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na Mheshimiwa Dkt. Emmanuel Nchimbi kuwa Mgombea Mwenza, pamoja lakini Mheshimiwa Dkt. Mwinyi kuwa mgombea kwa nafasi ya Urais wa Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza wote kwa sababu hili ni zao la kazi nzuri ambayo imekwishakufanyika. Tunaposema kazi iendelee, na kazi kweli inaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kutoa mfano, kwenye eneo la kilimo wakati Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anashika nchi, bajeti ya kilimo ilikuwa shilingi bilioni 294. Tunapoongea sasa kwa bajeti tunayoitekeleza ni shilingi bilioni 1,248 na kuendelea. Hii ni kazi kubwa; na matokeo tunayaona kwenye ruzuku za mbolea na mbegu, ambako tunatarajia, kwa sababu mwaka huu tulianza kwenye upande wa mbegu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ilikuwepo kidogo, wakulima walikuwa wanalalamika, kwa maana ya upatikanaji na usajili wa wakulima na usajili wa wasambazaji. Ninaamini tunavyoenda kwenye 2025/2026, msimu huo maandalizi yatafanyika ya kina na watu watapata mbegu kwa wakati, watapata mbolea kwa wakati, na kazi hiyo itaenda vizuri na uzalishaji utaendelea kuongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyosema sasa, kwamba uzalishaji wa mahindi umeongezeka kutoka tani milioni 6,000,000 mpaka milioni 11,000,000. Ninaamini baada ya muda tutahakikisha kwamba Afrika yote, sisi ndio tutakaokuwa wazalishaji wakubwa wa mazao yanayolisha wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wananchi wa Hanang’ ni wakulima wakubwa wa mahindi, na tumepata soko la uhakika pale NFRA Babati. Namshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, namshukuru Mheshimiwa Bashe, ametutengenezea mazingira angalau tunajidai. pale ambapo tunakwama, tunapata fedha za kutosha. Hii ni kazi nzuri ya uwekezaji kwenye sekta ya kilimo na ni mambo mazuri ambayo yanafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, nigusie kidogo kwenye Taarifa yetu ya Kamati. Kamati kwenye taarifa yake kwenye eneo la mtazamo na maoni ya jumla, waligusia eneo la chai, kwamba kuna wawekezaji wamechukua mashamba makubwa pamoja na viwanda, lakini utekelezaji na ufanisi wao ni mdogo. Jambo hili halipo kwenye chai pekee yake, lipo mpaka kwenye ngano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Hanang’ tunao wawekezaji ambao wamewekeza kwenye mashamba makubwa. Tunao wawekezaji wawili pale. Mmoja HLH, anafanya kazi vizuri, na ufanisi wake ni takribani 85% na kuendelea. Pia tunao rafiki zetu wa Ngano Limited, ufanisi wao ni mdogo kupitiliza. Kwa sasa mashamba wameyaacha, wananchi wamelima. Wamelima kwa sababu hawakuwa na matumaini kama wao wanaweza kulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hawa kwa miaka yote waliyokaa na hayo mashamba hawajawahi kutoa cess yoyote kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’. Wananchi wamelima. Ninachoomba, Serikali iwalinde hawa wananchi waliolima ili wavune mazao yao iwe sehemu ya cess. Nina hakika baada ya wananchi hao kuvuna, wakilima dengu Serikali itapata cess na tutajenga vituo vya afya, zahanati na madarasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mahindi vivyo hivyo, hawa wananchi wakalindwe ili kuhakikisha kwamba mwakani iwe ni changamoto kwa mwekezaji, ili aanze kulima kwa ufanisi. Akilima mashamba yake yote, Wanahanang’ wala hawana shida naye, ni rafiki yao, wanampenda. Ila wakilaza, ni kawaida tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe kama nyumbani zipo familia mbili, moja watoto wanakula wanashiba, familia nyingine ina njaa; ule familia yenye njaa, ikiona chakula huku, lazima wataanza kuhemea. Wana-Hanang’ wamehemea yale mashamba kwa sababu hao hawalimi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wale Wana-Hanang’ waliohemea yale mashamba walindwe. Uwekezaji walioufanya ulindwe ili mwakani nao wawe makini, walime yale mashamba kwa ufanisi unaotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuongelea ni jambo la Stakabadhi Ghalani. Hili jambo nimeongea na Mheshimiwa Bashe mara nyingi sana. Siyo kwamba mimi ni mpinzani wa Stakabadhi Ghalani. Stakabadhi Ghalani mimi ni muumuni wake na nilitoa elimu kubwa sana kwa wananchi wangu. Mimi baada ya kumaliza Kidato cha Nne kazi niliyoifanya ni kilimo na biashara ya mazao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanahanang wengi wanafanya biashara ya mazao na biashara ya mifugo. Hatupendi mnavyotuita sisi madalali. Sisi ni wafanyabiashara wa mazao, mtuite hivy, mtuheshimu hivyo. Hatupendi mtuite sisi madalali wa mifugo, kwa sababu mifugo tumekuwanayo, tumeishinayo. Mtuite wafanyabiashara wa mifugo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachotaka, kazi inayofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko wajengewe uwezo, wapewe rasilimali, wafanye kazi vizuri. Kazi inayofanywa na Bodi ya Stakabadhi, Ghalani wajengewe uwezo wafanye kazi zao vizuri. Kazi inayofanywa na soko la bidhaa Tanzania, wajengewe uwezo ili wafanye kazi zao vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninao mwongozo hapa, nimeshamwonyesha Mheshimiwa Waziri. Mimi na yeye tumeongea mara nyingi sana. Nampenda yeye kwa sababu ni muwazi, anaongea ukweli na anawapenda wakulima wa Tanzania, lakini nikianza kusoma kuanzia ukurasa wa saba hadi ukurasa wa 23, wakulima na wafanyabiashara wa kawaida wa mazao wamepigwa pembeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ukurasa wa sita hapa wamesema wakusanyaji wa mazao (aggregators), wakulima wakubwa, baada ya hapo wanatuambia kwamba kuna kiambatisho namba moja. Yaani sisi wakulima wa Tanzania ni watu wa viambatisho kweli! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi Mheshimiwa Waziri wa Kilimo amesema kuwa sekta hii ya kilimo ni ya watu binafsi. Tunakwenda shambani, hatulazimishwi; tunakwenda kulima wenyewe mbaazi, tunakwenda kulima wenyewe choroko, tunakwenda kulima wenyewe dengu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa Hanang’ wananiambia, kwa sasa tukalime dengu au tusilime? Tunatakiwa tuwahamasishe wakalime. Awape utaratibu wakulima wa Hanang’ kwamba wakivuna, je, tutakuwa na kila geti kama ilivyokuwa mwaka 2024? Kwenye mchanganuo huu wa bei kuna gharama za usimamizi wa mkoa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wako umekwisha, tafadhali.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: …gharama ya usimamizi wa Wilaya, kwenye kilimo, control zote za nini? Tunaenda kulima wenyewe kwa hiari.
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hili liangaliwe, liwekwe sawasawa ili angalau wakulima wakafanye kazi zao kwa ufanisi, tusifanye kazi kwa kulazimishwa, na mambo yaende na tupate mapato ya Serikali kama ilivyotakiwa. Ahsante sana. (Makofi)